Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Alex Malasusa
HALI imeendelea kwenda halijojo ndani ya Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, baada ya Mchungaji
Philemon Mollel kufukuzwa kazi na kuvuliwa kutoa huduma za kichungaji
katika kanisa hilo nchini.
Wiki iliyopita, Bodi ya Dayosisi hiyo chini ya uenyekiti wa Israel
Ole Karyongi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa KKKT, ilimtimua kazi Meneja wa
Hoteli ya Corridor Springs inayomikiwa na Dayosisi hiyo, John Njoroge
kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za hoteli hiyo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao kilichofanyika juzi chini ya
Karyongi, zilisema kuwa Mchungaji Mollel ameamuriwa afukuzwe kazi na
avuliwe wadhifa za kiroho za kichungaji.
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya kikao hicho vilieleza kuwa hatua
hiyo ni kutokana na Mchungaji Mollel kushindwa kutekeleza mambo matatu
aliyotakiwa na Tume maalumu ya watu watatu walioteuliwa na Menejimenti
ya Dayosisi hiyo na alipewa siku tatu kuomba radhi, lakini hakufanya
hivyo.
Habari zilieleza kuwa walioteuliwa Desemba 14, mwaka huu na kwenda
kumwona Mchungaji Mollel kutekeleza hayo ni pamoja na Msaidizi wa Askofu
Mchungaji Solomoni Massangwa, Katibu Mkuu wa Jimbo Arusha Magharibi,
Mchungaji Godwini Lekashu na Katibu Mkuu Karyongi.
Taarifa za ndani zilisema Mchungaji Mollel aliandikiwa barua Desemba
17, mwaka huu kufanya mambo matatu kabla ya kufika Desemba 23, mwaka
huu.
Habari zilisema katika mambo matatu aliyotakiwa kufanya ni
kumwandikia barua ya kuomba radhi kwa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini
Kati, Dk Thomas Lazer kueleza ni kwa nini alimkashifu na kumdharau.
Pili, alitakiwa atoe tamko katika Mtaa wa Azimio ibadani Desemba 23,
mwaka huu kuomba radhi kwa yale aliyotamka; na tatu achukue hatua
ifikapo Desemba 23, mwaka huu na kumwarifu Katibu Mkuu kwa barua baada
ya kuyatekeleza na awe amefanya hivyo kabla ya Desemba 24, mwaka huu.
Vyanzo vya habari vilisema kuwa baada ya Mchungaji Mollel kukaidi
hayo, kikao cha watu watatu chini ya Karyongi kiliamua kumfukuza kazi na
kumvua uchungaji.
Hata hivyo, habari za uhakika zilisema kuwa Mchungaji Mollel
hakufanya hivyo kwa madai kuwa yeye ni mtumishi wa mungu aliyetukuka
kufuata maadili na kamwe hawezi kufanya hivyo kwani hakumkashifu mtu
wala kiongozi yeyote, bali alieleza ukweli juu ya nani wa kuwajibika
katika deni la Sh bilioni 11.
Mbali ya uchungaji, Mollel alikuwa Kiongozi wa Usharika wa Ngateu
katika Jimbo la Arusha ni miongoni mwa wachungaji walioamua kuishupalia
katika kikao Bodi ya Hoteli hiyo, kuwajibika kwa kufanya ubadhirifu wa
mali ya kanisa hilo.
Hata hivyo, Mchungaji Mollel alipopigiwa simu kama amepata nakala ya
barua hiyo ya kufukuzwa kazi na kuvuliwa uchungaji, alikiri kuipata,
lakini alisema hayuko katika nafasi nzuri ya kulizungumza kwa sasa.
Mchungaji Mollel alisema uamuzi huo umechukuliwa kwa chuki na fitina,
lakini haukuangalia madhara ya deni la Sh bilioni 11 iwapo kanisa
litashindwa kulipa.
“Nipe muda ndugu yangu, ntakutafuta mimi mwenyewe na nitawaeleza
waumini tatizo liko wapi na nani ni tatizo ndani ya Dayosisi hii na
kwani nini mimi nimefanywa mbuzi wa kafara,” alisema Mchungaji Mollel.
Awali, Mollel alisema kwa nguvu zote kuwa madai aliyotuhumiwa nayo ni
kusema ukweli juu ya madeni ya miradi ya Dayosisi hiyo na ndio chanzo
cha barua ya kutaka ajieleze na huo ndio uliokuwa msimamo wake katika
kikao hicho cha wachungaji na wakuu wa majimbo.
“Niliweka wazi msimamo wangu katika tulichofanya Desemba 15, mwaka
huu kwamba Bodi lazima iwajibike kwa haya yote na kuwataka wenzangu
(Wachungaji na wakuu wa majimbo) tusitafune maneno kwa sababu ukweli uko
wazi na dhahiri,” alisisitiza Mchungaji Mollel na kuongeza:
“Niliwaambia wajumbe wazi kwamba msitufanye wajinga mbele ya washirika,
nikasema sipo tayari kuwaambia washirika ndio kwa jambo lisilowezekana
na hiyo ndiyo sababu ya kuandikiwa barua hii na nitaweka kila kitu
hadharani.”
Kuhusu Njoroge, habari kutoka ndani ya hoteli hiyo zinasema kuwa
alitimuliwa kazi wiki mbili zilizopita kutokana na shinikizo la
wachungaji wa kanisa hilo kutokana na hali mbaya ya kifedha ya hoteli
hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hoteli hiyo, Karyongi alithibitisha kutimuliwa
kwa meneja huyo akidai kuwa ni hatua ya kupisha uchunguzi ili kubaini
ukweli wa ubadhirifu wa hoteli hiyo na mambo mengine.
“Ni kweli Meneja ametimuliwa ili kupisha uchunguzi wa kina ufanyike
kujua ukweli wa hali halisi na sasa timu ya wakaguzi inaendelea na kazi
ya kupitia mahesabu ya hoteli hiyo,” alithibitisha Karyongi.
Hata hivyo, habari za ndani za hoteli hiyo na Dayosisi zinasema,
hatua ya kufukuzwa kwa meneja huyo ni janja ya viongozi waandamizi wa
Dayosisi ambao inasemekana walishirikiana naye kuifilisi kifisadi.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonesha kuwa Njoroge ambaye ni raia wa
Kenya, amefichwa Dubai na viongozi hao waandamizi wa Dayosisi (majina
yanahifadhiwa kwa sasa) ili wasiumbuke kutokana na kadhia hiyo.
Inasemekana hata mali alizokuwa akimiliki Njoroge ikiwamo Klabu ya
usiku inayoitwa Brazil iliyokuwa maeneo ya Nanenane Njiro, ameiuza kabla
ya kuondoka nchini kinyemela.
View detail