Saturday, November 23, 2013

BABU SEYA NA MWANAE WASHINDWA TENA MAHAKAMNI LEO

http://azizicompdoc.blogspot.com/
Nguza Mbangu (kulia) na mwanaye, Papii Nguza wakipunga mikono kwa ndugu na jamaa zao mara baada ya kupanda gari kurejea jela kutumikia kifungo cha maisha baada ya Makahama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa yao jana, jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Jamson 


Jitihada za mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ kujinasua katika kifungo cha maisha jela zimekwama baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kutupilia mbali maombi yao ya marejeo ya hukumu ya rufaa yao.
Hii ni mara ya tatu kwa wasanii hao kugonga mwamba, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa zao za kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyowatia hatiani na kuwahukumu kifungo hicho.
Wafungwa hao, kupitia kwa Wakili Mabere Marando walikuwa wakiiomba Mahakama ya Rufani ifanye marejeo ya hukumu yake ya Februari 11, 2010 iliyothibitisha adhabu hiyo waliyohukumiwa na mahakama ya chini na badala yake iwaachie huru.
Lakini jana, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake uliotolewa na jopo la Majaji, Nathalie Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Salim Mbarouk, lilitupilia mbali maombi hayo na kusisitiza kuwa waendelee kutumikia adhabu hiyo.
Uamuzi huo uliibua machungu si tu kwa wafungwa hao ambao walitoa kauli za kukata tamaa, bali pia kwa wakili wao mwingine, Gabriel Mnyele ambaye alisema kuwa sasa hakuna namna nyingine ya kuwachomoa katika adhabu hiyo isipokuwa kwa miujiza tu.
Wakati wafungwa hao na wakili wao wakitoa kauli hizo za kukata tamaa, ndugu, jamaa na marafiki zao walibaki wakibubujikwa na machozi tu baada ya uamuzi huo kusomwa, hali iliyoendelea hata wakati wafungwa hao walipokuwa wakipandishwa katika gari la Magereza kurudishwa gerezani.
Katika uamuzi wake uliosomwa na Kaimu Msajili wa wake, Zahra Maruma, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali maombi hayo ikisema kuwa waomba marejeo hao hawakuwa na hoja za msingi.
Ilisema hoja zilizotolewa katika maombi hayo ya marejeo si tu kwamba hazikidhi kuifanya irejee hukumu hiyo, bali pia hoja hizo zilishatolewa wakati wa usikilizwaji wa rufaa na kutolewa uamuzi.
Pia Mahakama hiyo ilieleza kuwa waomba marejeo hao hawakuweza kubainisha makosa waliyodai kuwa yalijitokeza katika hukumu iliyowatia hatiani na kwamba hata kama yangekuwapo, hawakuweza kueleza ni jinsi gani yalisababisha haki kutokutendeka.
“Kuhusu upande wa mashtaka kushindwa kuwaita mahakamani mashahidi wanaoonekana kuwa muhimu kuunga mkono ushahidi wa watoto, tunasema kuwa hoja hiyo haina msingi,” ilisema Mahakama katika uamuzi wake na kuongeza:
“Suala la shahidi gani aitwe mahakamani kuthibitisha kesi ya upande wa mashtaka liko mikononi mwa upande wa mashtaka. Zaidi ya yote, idadi ya mashahidi si hoja ya msingi bali kuaminika kwao.”
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Wakili Mnyele alisema: “Huu ndiyo mwisho wa mchakato. Kulingana na hukumu ilivyotolewa, kunahitajika mahakama ya juu zaidi ya hii. Kungekuwapo na ‘Supreme Court’ (Mahakama ya Juu) ambayo ingeweza kusikiliza na kufikia uamuzi wa haki.”
Akisindikizwa na askari kuelekea kwenye gari kurejeshwa gerezani, Papii Kocha alisema: “Sasa tunamuachia tu Rais ndiye anayeweza kutoa uamuzi wa mwisho.”
Lakini Babu Seya kwa upande wake, baada ya kupanda katika gari hilo tayari kurejea gerezani alisema bila ya kufafanua: “Kwa binadamu ni makosa, lakini kwa Mungu hakuna makosa.”
Babu Seya na Papii Kocha waliingia katika viwanja vya Mahakama hiyo saa 2:23 asubuhi wakisindikizwa na askari Magereza huku wakionekana wenye furaha. Baada ya kuingia walisalimiana na watu mbalimbali wakiwamo ndugu zao wachache waliokuwa wameshafika.
Ilipofika saa 4:54 wafungwa hao waliingizwa katika Ukumbi wa Mahakama tayari kusubiri kusomwa kwa uamuzi huo. Saa 5:08 ndipo Naibu Msajili Maruma alipoingia katika ukumbi huo na kuanza kusoma uamuzi huo.
Hukumu ya awali
Awali, Babu Seya na wanawe watatu, Papii, Nguza Mbangu na Francis Nguza, walihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwaka Juni 25, 2004, baada ya kupatikana na hatia ya kuwabaka na kuwalawiti watoto wa kike 10, wenye umri chini ya miaka 10.
Walihukumiwa adhabu hiyo na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Addy Lyamuya baada ya kuwatia hatia ya makosa 20 ya kuwabaka na kuwalawiti watoto hao.
Pia waliamriwa kuwalipa fidia ya Sh2 milioni watoto hao kila mmoja. Watoto hao wote, wakati huo, walikuwa ni wanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mashujaa iliyoko Sinza, Dar es Salaam.
Hata hivyo, kupitia kwa wakili wao aliyekuwa akiwatetea katika kesi hiyo, Hubert Nyange walikata rufaa Mahakama Kuu wakipinga hukumu hiyo pamoja na adhabu, lakini waligonga mwamba baada ya Jaji Thomas Mihayo kutupilia mbali rufaa yao Januari 27, 2005.
Kwa mara nyingine, Februari 11, 2010, Babu Seya na Papii Kocha walishindwa kujinasua katika adhabu hiyo baada ya Jopo la Majaji watatu Kimaro, Massati na Mbarouk, kuridhia waendelee kutumikia adhabu hiyo. Hata hivyo, Mahakama hiyo jopo hilo liliwaachia huru Mbangu na Francis, baada ya kuridhika kuwa hawakuwa na hatia.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About