Wednesday, January 8, 2014

DAWASCO YAKATIWA UMEME, YADAIWA BIL 7

http://azizicompdoc.blogspot.com/
Kibao cha operesheni kata maji kimeligeukia Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) baada ya kukatiwa umeme na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ikidaiwa Sh7 bilioni.
Mmoja wa wafanyakazi katika mtambo wa Ruvu Chini, Mlandizi ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji, alisema kuwa umeme ulikatwa juzi katika mtambo huo kuanzia saa tatu asubuhi na ulirejeshwa saa mbili usiku.
Alisema limekuwa jambo la kawaida umeme kukatwa katika mtambo huo na kurudishwa baada ya mazungumzo baina ya watendaji wa juu wa Tanesco na Dawasco na mara ya mwisho ilikuwa miezi miwili iliyopita.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alikiri Dawasco kudaiwa kiasi cha Sh6.3 bilioni na kwamba Tanesco ilikata umeme kwa takriban saa saba juzi.
“Lakini waliurudisha jioni baada ya kuzungumza nao na wakatuelewa,” alisema Profesa Maghembe.
Alisema ameiagiza Dawasco kuandaa programu ya namna ya kulipa deni hilo na kulimaliza.
“Tumezungumza nao (Tanesco) na mazungumzo bado yanaendelea ila nilichowaagiza Dawasco ni kwamba waweke programu ya namna ya kulilipa deni hilo. Hayo ndiyo maagizo yangu,” alisema Profesa Maghembe.
Hali hiyo inaaminika kuwa ndiyo imekuwa ikisababisha kukosekana mara kwa mara kwa maji katika Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumzia athari za kukatiwa umeme, mfanyakazi huyo wa Dawasco Ruvu Chini alisema: “Kuna wakati mwingine shirika hutangaza upungufu wa maji kwa madai kuwa kuna marekebisho yanafanyika na kuna wakati huwa haitangazwi kabisa lakini ukweli ni kwamba umeme hukatwa mara kwa mara na Tanesco.
“Watu wanaweza wakahisi labda maji hayatoki kutokana na mgawo usioeleweka wa Dawasco au wakati mwingine kudhani kuwa pengine ni kutokana na matatizo ya miundombinu, lakini ukweli ni kuwa kuna tatizo baina ya Tanesco na Dawasco.”

Kaimu Meneja wa Tanesco, Adrian Severin alisema walifikia hatua hiyo kutokana na kuidai Dawasco Sh7 bilioni na kwamba kwa takriban mwaka mzima uliopita, shirika hilo halikulipa gharama zozote za huduma.
Severin alisema Dawasco hutumia umeme wa wastani wa Sh600 milioni kwa mwezi... “Walituandikia hundi mara mbili lakini tulipokwenda benki hatukupata fedha, tukaamua tuwasitishie huduma jana (juzi).”
Alisema baada ya hatua hiyo ndipo Dawasco walipojitokeza kufanya mazungumzo na kutoa kiasi cha Sh600 milioni na umeme ukarudishwa. Alisema katika siku za usoni wasipolipa watawasitishia tena huduma hiyo.

Ofisa Uhusiano wa Dawasco, Everlasting Lyaro alikiri shirika lake kudaiwa lakini akishutumu hatua ya Tanesco kulikatia huduma hiyo katika mitambo yake kwa madai kuwa inaweza kuleta athari kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam.
“Sijafahamu deni hilo lina malimbikizo kwa muda gani lakini pamoja na hivyo bado sheria haziruhusu kukata umeme kwa sababu Dawasco tunafanya kazi ya kuhudumia jamii,” alisema Lyaro na kuongeza:
“Tuna mitambo, ambayo ni Ruvu Juu, Ruvu Chini na Mtoni ambayo inazalisha takriban lita 270 milioni kwa siku, wakikata umeme itakuwa ni hatari sana,” alisema.
Imeandikwa na Joseph Zablon, Daniel Mjema, Kelvin Matandiko na Ibrahim Yamola.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About