Monday, January 6, 2014

SERIKALI YAWEKA WAZI SABABU YA KIFO CHA DR. MGIMWA

http://azizicompdoc.blogspot.com/
Mama Maria Nyerere akitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa, wakati wa shughuli za kuaga mwili huo zilizofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam jana. Mwili huo umesafirishwa kwenda mkoani Iringa kwa maziko. Picha na Venance Nestory 

Wakati mwili wa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa ukitarajiwa kuzikwa leo, Serikali imesema kilichosababisha  kifo chake ni ugonjwa wa figo.
Dk Mgimwa alifariki Januari Mosi, mwaka huu katika Hospitali ya Kloof Medi Clinic, Pretoria nchini Afrika Kusini alikokuwa amelazwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile uliutaja ugonjwa huo mbele ya waombolezaji waliofika kuuaga mwili wake kwenye Viwanja vya Karimjee.
Likwelile alisema: “Marehemu Mgimwa alikwenda Hospitali ya Kloof Medi Clinic, Afrika Kusini Novemba 3, mwaka 2013 kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake...baada ya uchunguzi, madaktari walimshauri alazwe kwa uangalizi zaidi na matibabu na kwamba aliendelea na matibabu ya figo hadi kifo chake.”
Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema wamepoteza mtu muhimu waliyekuwa wakimtegemea hasa katika mabadiliko ya muda wa bajeti yaliyoanza mwaka 2013.
“Kama tungekuwa na uwezo wa kumrudisha duniani na kumpeleka mtu mwingine tungefanya hivyo kwa sababu ya umuhimu wake, lakini hatuna uwezo huo, tulimpenda, tulimuhitaji lakini Mungu amempenda zaidi,” alisema Makinda.
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema Dk Mgimwa alikuwa kiongozi asiye na mzaha kazini lakini hakuwa na makuu wala hakujikweza.
Alisema Mgimwa alizingatia sheria, taratibu na kanuni katika kushughulikia kero za Watanzania katika kujenga msingi imara ya Bajeti ya Serikali.
“Katika kipindi cha takribani miaka miwili ambacho tumekuwa chini ya uongozi wa Dk Mgimwa, tumejifunza mambo mengi ya kifedha, kibajeti na kiuongozi ambayo tutaendelea kuyatumia,” alisema.
Naye Waziri wa Fedha wa Uganda, Jackson Kajala alisema Sekta ya Uchumi na Fedha imepata pigo kubwa kutokana na kifo hicho kutokana na mchango wake katika masuala ya forodha na sarafu moja kwa nchi wanachama wa jumuiya.
“Tutamkosa, nilipata kukutana naye katika mikutano mingi ya Jumuiya na nipo hapa kuwawakilisha Mawaziri wa Fedha wa Afrika Mashariki na wote kwa ujumla wetu tumesikitishwa sana na kifo cha Waziri Mgimwa,” alisema Kajela.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alberic Kacou alisema kuwa marehemu alitumia muda wake mwingi na sehemu kubwa ya maisha yake katika fani yake ya uchumi na fedha.
Alisema kuanzia NBC alikokuwa ameajiriwa wakati fulani utumishi wake chuo cha benki hadi katika nafasi yake ya uwaziri alikuwa kiungo muhimu baina ya wahisani, serikali na wafanyabiashara wadogo.
“Alikuwa na mchango mkubwa sana katika masuala ya uchumi kwani hata hoja za wahisani zilipata majibu ya msingi kuhusiana na bajeti ya nchi, ninaamini kuwa waliobaki wataendeleza kile ambacho marehemu alikuwa anaifanya,” alisema Kacou.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, alisema tofauti na mawaziri wengine, Mgimwa alifanya kazi kwa zaidi ya saa 16 kwa siku wakati wanapitia Sheria ya Fedha ambako walikaa katika kikao hadi saa saba usiku.
Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya waombolezaji waliofika kwenye viwanja vya Karimjee kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Dk Mgimwa, pamoja na viongozi wengine wakiwemo Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Spika wa Bunge, Anne Makinda, mawaziri, Mama Maria Nyerere na viongozi wengine wa vyama vya siasa.
Kikwete ambaye alikuwa wa mwisho kutoa heshima zake baada ya kuchelewa kufika kwenye viwanja hivyo akitokea Zanzibar, mara baada ya kufika alitia saini kitabu cha maombolezo na kutoa heshima za mwili kwa marehemu Mgimwa.
Kwa mujibu wa ratiba, leo Rais Kikwete pia anatarajiwa kuongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Iringa kwenye mazishi ya waziri huyo yanayotarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Magunga.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema Dk Mgimwa alikuwa mwelewa, mnyenyekevu na mstarabu.
“Kwa muda niliomfahamu Dk Mgimwa akiwa kwenye siasa, sikuwahi kumwona akikwaruzana wala kugombana, muda wote alikuwa mstaarabu na msikivu kwa kila mtu,” alisema.
Mbowe alisema viongozi wa kisiasa wanatakiwa kuiga mfano wake kwa kuacha chuki na malumbano yasiyokuwa na tija.
“Nilikutana naye tena baadaye usiku huo na nilipomuuliza, alinieleza kuwa alikuwa anamtaarifu Waziri Mkuu Mizengo Pinda walipofikia katika kikao hicho,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema Mgimwa atakumbukwa kwa mengi kwani licha ya uchapakazi, alikuwa anasikiliza, anatafakari kisha anajibu.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana jioni aliupokea mwili wa Dk Mgimwa baada ya kuwasili mkoani Iringa uliowasili saa 11:15 jioni tayari kupelekwa katika kijiji cha Magunga, Kata ya Maboga, Wilaya ya Iringa Vijijini tayari kwa mazishi leo.
Mara baada ya kuwasili, mwili wa Dk Mgimwa uliosindikizwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, Naibu Spika, Job Ndugai, wabunge na viongozi wa dini ulipelekwa kwenye Ukumbi wa Siasa ni Kilimo ambako Waziri Mkuu aliongoza maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Iringa na vitongoji vyake kuuaga.
Huzuni, vilio na simanzi vilitanda ndani na nje ya ukumbi huo, huku baadhi ya wapiga kura wake wakiwemo madiwani wakiangua vilio na wengine wakiwa katika makundi wakitafakari.
Baadaye, Waziri Mkuu aliyetokea kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mpanda, Katavi alikokwenda kwa mapumziko ya mwisho ya mwaka, alikwenda kijijini Magunga kukagua ujenzi wa kaburi atakalozikwa Dk Mgimwa, uwekaji wa mahema pamoja na eneo la kufanyia ibada ya mazishi.
Vilevile alikagua mahali ambapo mwili wa marehemu utalazwa ukisubiri taratibu za mazishi hapo leo.
Akiwa Kijiji cha Magunga kilichopo kilometa 66 kutoka Iringa mjini, Waziri Mkuu alifika nyumbani kwa Mama Mzazi wa Dk Mgimwa, Consolata Semgovano na kumpa pole pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.
Hali ya Mji wa Iringa pia ilionekana kubadilika huku kukiwa na misafara ya magari yaliyokuwa inakwenda kwenye kijiji hicho ambacho mazishi hayo yatafanyika leo.
*Imeandikwa na Raymond Kaminyonge, Joseph Zablon, Dar na Geofrey Nyang’oro, Iringa.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About