Friday, January 17, 2014

TANESCO HALI YAZIDI KUA TETEMwishoni mwa wiki iliyopita, wezi walivamia na kuiba nyaya katika kituo cha kusambazia umeme cha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Ubungo, Dar es Salaam hivyo kuathiri huduma ya umeme katika sehemu kubwa ya jiji hilo kwa takriban siku tatu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, wizi huo umelisababishia shirika lake hasara ya Sh200 milioni.
Wakati hali ikiwa haijatengamaa, wezi tena wameripotiwa kuiba vyuma vinavyobeba nyaya za umeme huko Kahama na kusababisha sehemu kubwa ya wilaya hiyo hususan machimbo ya dhahabu ya Bulyanhulu kukosa huduma ya nishati. Tanesco imesema wizi huo umelitia hasara shirika hilo ya Sh1.2 bilioni.
Wizi katika miundombinu ya Tanesco siyo jambo geni, tumekuwa tukisikia taarifa mbalimbali za tatizo hilo lakini kimsingi hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa hazilingani na ukubwa wake.
Mathalan, akizungumzia wizi huu wa Ubungo, Mramba alisema walinzi waliokuwa zamu katika kituo hicho wamekamatwa huku akisema sehemu hiyo inakuwa ngumu kudhibiti wizi kutokana na mwingiliano wa watu. Tunasema hapana. Hasara ya Sh200 milioni haiwezi kuishia kwa walinzi kukamatwa, tunadhani hatua kubwa zaidi zinastahili kuchukuliwa ili siyo tu tabia hiyo isijirudie tena katika maeneo hayo, bali iwe funzo kwa wengine.
Tunaamini kabisa wapo watu waliopewa dhamana ya kusimamia maeneo husika ulipotokea wizi huo, tungependa kusikia hatua zilizochukuliwa dhidi yao.
Tanesco imekuwa ikilalamikia kutokuwa na fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya wateja wake ilionao sasa huku kukiwa na foleni ndefu ya wengine wanaohitaji huduma hiyo nyeti ya nishati.
Hasara kama hii ikichangiwa na kuvuta miguu katika kukusanya madeni, vimeilazimu kubeba magunia ya lawama. Kama ilivyoeleza jana, Tanesco inazidai taasisi za Serikali kiasi cha Sh129 bilioni, kati ya hizo Sh70 bilioni zikiwa deni la Zanzibar.
Aidha, linawadai wateja binafsi pamoja na kampuni mbalimbali kiasi cha Sh104 bilioni. Inasikitisha kwamba Tanesco imekuwa ikitoa takwimu hizi za madeni hadharani lakini ufuatiliaji wake umekuwa hafifu na dhaifu.
Katika hali ya kawaida, Serikali au taasisi zake hazikupaswa kuwa katika mkumbo huu. Tunasema hivyo kwa sababu kila mwaka fedha kwa ajili ya malipo ya huduma hiyo hutengwa na kupitishwa na Bunge katika Bajeti, vinginevyo tuelezwe kwamba fedha hizo zimetumika kwa ajili ya shughuli gani nyingine.
Pia Tanesco imeonyesha udhaifu mkubwa katika ufuatiliaji wa madeni kwa watu binafsi na kampuni. Tungependa kusikia hatua stahiki zikichukuliwa na shirika hilo dhidi ya wadaiwa sugu.
Sambamba na kuchukua hatua, tunadhani kwamba ipo haja kwa Tanesco kuimarisha kitengo chake cha elimu kama ilivyo katika baadhi ya taasisi za Serikali na mashirika mengine, ili kuwafanya wateja wake kutoa ushirikiano na kuliwezesha kutimiza wajibu wake kwa jamii.

Kwa mfano, sababu zilizotolewa za wizi wa Kahama kwamba wezi hutumia vyuma hivyo vyenye thamani kubwa kwa ajili ya kutengenezea majembe, matoroli na kuviuza kama chuma chakavu, zingeweza kudhibitiwa pia kwa kutoa elimu kwa wananchi.
Pamoja na mikakati ya maboresho inayoendelea hivi sasa ndani ya shirika, tunautaka uongozi mpya wa Tanesco kuvalia njuga matatizo hayo ambayo yanaonekana kuwa sugu vinginevyo itakuwa ndoto kwake kupiga hatua za maendeleo. Kwa lugha za kisiasa, tunadhani umefika wakati kwa Tanesco kujivua gamba ili kuleta matumaini ya kuiangaza Tanzania kiuchumi.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About