Takriban wanajeshi 200 wa
Nigeria wanatarajiwa kuwasili nchini Mali kusaidia katika harakati dhidi
ya wapiganaji wa kiisilamu Kaskazini mwa nchi.
Ni kikosi cha kwanza cha jeshi kutoka Magharibi
mwa Afrika kujiunga na wanajeshi wa Ufaransa walioanza kupambana na
wapiganaji wa kiisilamu tangu Ijumaa iliyopita.Jumla ya wanajeshi 3,300 wa kikanda watapelekwa nchini Mali chini ya azimio la Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa. Chad imesema itapeleka wanajeshi 2,000.
Wakati huohuo, wanajeshi wa Mali na Ufaransa, wameanza operesheni yao ya ardhini dhidi ya wapiganaji hao wa kiisilamu.
Duru zinasema kuwa makabiliano yalizuka kati ya waasi na wanajeshi mjini Diabaly, umbali wa kilomita 350 kaskazini mwa mji mkuu Bamako siku ya Jumatano.
Wapiganaji wa kiisilamu waliingia mji wa Diabaly siku ya Jumatatu na kutwaa mji huo kutoka kwa waasi. Ndege za kivita za Ufaransa tayari zimeshambulia ngome moja ya waasi hao.
Takriban wanajeshi 190 wa Nigeria wanatarajiwa kwenda kwa ndege nchini Mali kutoka Kaduna baadaye leo.
Chad pia imethibitisha kutuma wanajeshi 2,000 watakaojiunga na harakati dhidi ya wanajeshi nchini Mali.
Benin, Ghana, Niger, Senegal, Burkina Faso na Togo pia zimeahidi kutuma vikosi.
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande alisema kuwa lengo na nia ya Ufaransa ni kuhakikisha uthabiti wa Mali.
Nchi hiyo imepeleka wanajeshi, 800 kupambana na waasi ardhini na duru za ulinzi zinasema kuwa idadi ya wanajeshi hao inatarajiwa kuongezeka hadi 2,500.
Hata hivyo, Ufaransa imekuwa ikishinikiza kutumwa kwa kikosi cha kanda ya Afrika Magharibi.
Kuwasili ka wanajeshi wa kwanza wa Nigeria itakuwa afueni kwa wale wa Ufaransa ambao hawajapata msaada wa kutosha kutoka kwa jeshi la Mali ambalo halina nguvu sana.
0 comments:
Post a Comment