Abiria 37 waliokuwa wamesafaria ndege ya Shirika la Precision Air, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana walinusurika kifo, baada ya magurudumu manne ya ndege hiyo kupasuka ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Arusha.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea saa 6:15
mchana, wakati ndege hiyo, ikitua kutoka jijini Dar es Saalam, ikiwa na
abiria hao 37, marubani wawili na wahudumu wawili.
Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza hakuna majeruhi aliyeripotiwa.
“Hadi sasa hali ni shwari, ndege iliweza kusimama
licha ya kupasuka magurudumu. Kiutaratibu uchunguzi umeanza kufanywa na
wataalamu husika,”alisema Kamanda Sabas.
Ofisa Mwendeshaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
nchini (TCAA), wa Uwanja wa Ndege Arusha, Roland Mwalyambi, alisema kuwa
katika tukio hilo, hakuna abiria aliyejeruhiwa licha ya kupata mshtuko
mkubwa.
“Uchunguzi wa ajali hii umeanza, lakini hakuna majeruhi, abiria wote walifanikiwa kushuka salama,”alisema Mwalyambi.
Alisema ndege hiyo, kama ingetua salama
ilitarajiwa kusafiri kurejea Dar es Salaam kupitia Zanzibar, lakini
abiria waliotarajia kusafiria ndege hiyo, walipelekwa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro ili kuendelea na safari.
Katika ndege hiyo, pia kulikuwa na maofisa
mbalimbali wa Serikali na Jeshi la Wananchi, ambao leo wanatarajia
kuhudhuria sherehe ya kutolewa kamisheni kwa maofisa wa jeshi katika
Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli(TMA), ambapo Rais Jakaya Kikwete
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Tukio hilo la ndege kupata ajali katika uwanja huo
ni la pili kutokea mwaka huu, kwani mapema mwaka huu, mfanyabiashara
maarufu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha, Babu Sambeki alipata ajali pia
katika uwanja huo, wakati akijiandaa kutua na ndege yake.
Mfanyabiashara huyo, alifariki papo hapo baada ya
moja ya mabawa ya ndege kunasa katika matawi ya mti jirani na uwanja
huo. Hata hivyo, taarifa ya ajali hiyo hadi sasa haijawekwa hadharani.
Kukosekana kwa taa katika uwanja huo, ambao
umekuwa ukitumiwa na ndege nyingi ndogo hasa za watalii, imekuwa ni kero
kubwa na mara kadhaa safari zimeahirishwa kutokana na tatizo hilo.
0 comments:
Post a Comment