Waziri wa Fedha, Mheshimiwa William Mgimwa.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amemtembelea Waziri wa Fedha, Mheshimiwa William Mgimwa katika Hospitali
ya Kloof mjini Pretoria, Afrika Kusini, ambako Waziri huyo amelazwa
akitibiwa.
Rais
Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Afrika
Kusini alimtembelea Waziri Mgimwa jioni ya jana, Jumanne, Desemba 10,
2013, baada ya kumaliza shughuli za jana za Kumbukumbu ya Kifo cha
aliyekuwa kiongozi mashuhuri wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela.
Katika mazungumzo yaliyochukua kiasi cha robo saa, Waziri Mgimwa alimwambia Rais Kikwete: “Hali
yangu inaendelea vizuri Mheshimiwa Rais na nakushukuru sana kwa kupata
muda wa kuja kuniona. Inatia moyo na nguvu sana Mheshimiwa Rais.”
Naye Rais
Kikwete amemtakia heri Waziri Mgimwa ambaye amekuwa kwenye hospitali
hiyo kwa muda sasa na baadaye alipata nafasi ya kusalimia na
wana-familia wa Mheshimiwa Mgimwa ikiwa ni pamoja na mke wake na binti
yake mkubwa.
Wakati huo
huo, Rais Kikwete jana, Jumatano, Desemba 11, 2013, amemtembelea Ofisa
Mwandamizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jenerali Vicent Kariongo
Mritaba ambaye amelazwa kwenye Hospitali ya Mifupa ya Lynnmed Clinic
iliyoko eneo la Lynnwood mjini Pretoria.
Rais
Kikwete amemtembelea Jenerali Mritaba akiwa njiani kwenda Uwanja wa
Ndege wa Kituo cha Jeshi la Anga la Waterkloof ili aweze kupanda ndege
kurejea nyumbani.
Kabla ya
kuondoka nchini, Rais Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi 91 wa wakuu
wa Serikali na nchi waliotoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mzee Mandela
na kutia saini Kitabu cha Kumbukumbu cha Kifo cha kiongozi huyo ambaye
hujulikana kwa jina maarufu la Madiba.
Viongozi
hao walikuwa wa kwanza kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili huo ambao
utalazwa kwenye Ofisi ya Urais wa Afrika Kusini zilizoko katika majengo
ya Union Buildings, Pretoria.
0 comments:
Post a Comment