Baadhi ya wachumi na wadau mbalimbali wa nishati ya umeme
wameikosoa hatua ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) baada
ya kuongeza gharama za umeme kwa maelezo kuwa hatua hiyo itamkandamiza
mwananchi wa kawaida.
Kauli hizo zimekuja siku moja baada ya Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za
umeme huku kukiwa na ongezeko kubwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam
jana, baadhi yao walisema hatua iliyochukuliwa siyo mwarobaini wa
matatizo ya umeme, badala yake unahitajika mfumo mpya wa kiutendaji ili
kuinusuru Tanesco.
Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Wenye Viwanda Tanzania
(CTI), Felix Mosha alisema kitendo cha kuongeza gharama ya umeme
kitapunguza ushindani wa kibiashara.
“Wananchi walitarajia ongezeko la viwango vya
gharama ambavyo vingeweza kuongeza ushindani wa bidhaa zetu dhidi ya
zile zinazotoka nje. Tangazo hilo la Ewura linatakiwa kutazamwa upya,”
alisema Mosha.
Pia alisema kuwa gharama za uzalishaji nchini
zimekuwa kubwa kutokana na matumizi ya jenereta ambazo ni mara nne zaidi
ya mitambo ya kawaida.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa
Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEO’s Roundtable), Ali
Mufuruki alitofautiana msimamo huo wa wenye viwanda akisema hatua hiyo
ni sahihi endapo itakuwa suluhisho la kupunguza changamoto za kupatikana
kwa umeme.
Mufuruki alisema Tanesco imekuwa na tatizo kubwa
la kununua umeme kwa bei ya juu ukilinganisha na ankara inazotuma kwa
wateja wake.
“Tusiangalie zaidi kumuathiri mwananchi na
kupunguza ushindani wa kibiashara tu kwani mtu anaweza kujipanga. Ni
heri bei ipande kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha
kuliko kuwa na umeme wa kubabaisha,” alisema Mufuruki.
Wanaharakati
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema mwananchi amebebeshwa mzigo huku
baadhi ya watumishi wa Tanesco wakituhumiwa kufanya ubadhirifu.
“Leo hii mamalishe na wajasiriamali wadogo
watafanyaje kazi zao? Kwa nini wadaiwa sugu wa kodi wasingebebeshwa
mzigo huo... Mimi ningekuwa na uwezo ningetembea peke yangu kuandamana
kwa sababu wananchi wanaona lakini wanaendelea kuvumilia maumivu
yasiyostahili,” alisema Dk Bisimba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu
Mallya alisema kwa ongezeko hilo la bei, Serikali haina mpango madhubuti
wa kupunguza umaskini wa Mtanzania.
“Kuna kila sababu ya Serikali kukaa chini na
kutafakari upya juu ya gharama hizo za umeme ili kumsaidia mwananchi kwa
sababu hakuna uhusiano wa kupanda kwa gharama hizo na maisha anayoishi
kwa sasa na badala yake itaendelea kumuumiza,” alisema Usu.
TUCTA yatoa tamko
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya alisema shirikisho hilo limetoa
maazimio kadhaa ikiwamo kuitaka Serikali kuongeza mishahara kwa
wafanyabiashara ili kutengeneza uhusiano wa ongezeko hilo na kipato cha
mshahara uliopo.
“Kama imeona ni vyema kuongeza bei hizo, basi
iongeze hata mishahara kwani ongezeko la Tanesco ni asilimia 40 kwa mtu
wa chini wakati mshahara wake ulipanda kwa asilimia 25 tu. Kwa mazingira
hayo ni lazima ataumia tu,” alisema Mgaya.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Lipumba ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kiuchumi alisema
Tanesco itahitaji kuwa na menejimenti yenye uwezo wa kulisimamia shirika
hilo ikiwa ni pamoja na kudhibiti upotevu mkubwa wa fedha.
“Hakuna menejimenti ya kusimamia shirika, tunataka
uongozi wa watu wenye uwezo wa kulinusuru shirika ambao wataokoa
upotevu wa fedha,” alisema Profesa Lipumba.
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Constantine
Akitanda alisema kupanda kwa gharama za umeme kunaathiri sekta nyingine
zinazotegemea huduma kutoka Tanesco, hivyo wananchi wategemee
mabadiliko ya bei za bidhaa.
“Ni bora wangeboresha miundombinu ya Tanesco na
kuondoa mikataba mibovu ambayo inawafanya watumie sehemu kubwa ya mapato
yao kulipa madeni,” alisema Akitanda.
0 comments:
Post a Comment