Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Liberatus Sabas akiwaonyesha waandishi wa habari bunduki aina ya SMG
iliyokamatwa wilayani Ngorongoro hivi karibuni huku mkono wake wa kulia
akiwa ameshika kifurushi chenye madawa ya kulevya aina ya Heroin
yaliyokamatwa jana wilayani Arumeru.
(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi
la Polisi Arusha)
Kuelekea
katika kusherehekea Sikukuu ya Krimas, Jeshi la Polisi Mkoani hapa
limeendelea kupambana na wahalifu wa madawa ya kulevya ambapo safari hii
limefanikiwa kuwakamata watu wanne wakiwa na madawa ya kulevya aina ya
Heroin. Tukio hilo limetokea jana tarehe 23.12.2014 muda wa saa 12:30
jioni maeneo ya Elikyurei wilayani Arumeru.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoani hapa
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas amesema
kwamba tukio hilo limefanikiwa baada ya kupata taarifa toka kwa raia
wema ambapo askari wa Jeshi hilo walikwenda katika eneo husika na
kuwakuta watuhumiwa hao wakiwa ndani ya chumba cha mtuhumiwa mmojawapo
huku wakiwa wanaendelea kufunga kete za madawa hayo na tayari walikuwa
wamefunga kete 25.
Kamanda
Sabas aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Seifu Bakari (28) na Hamid
Makame wote ni wakazi wa Elikyurei wilayani Arumeru pamoja na wenzao
ambao ni Evance Gidion (29) Mkazi wa Ngarenaro na Abraham Hamis (23)
Mkazi wa Kaloleni jijini hapa.
Kamanda
Sabas alisema kwamba madawa hayo yenye uzito wa gramu 100 yanakadiriwa
kuwa na thamani ya Tsh 10 Mil. Mpaka hivi Jeshi hilo linaendelea
kuwahoji watuhumiwa hao ili kufahamu undani zaidi na watafikishwa
mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.
Kufuatia
tukio hilo na mengine ya nyuma Kamanda Sabas alizidi kuwashukuru
wananchi wa Mkoa huu kwa jinsi wanavyoonyesha ushirikiano kwa jeshi hilo
juu ya kufichua vitendo vya uhalifu na wahalifu na kuahidi kuendeleza
falsafa ya Polisi Jamii ambayo inaleta mafanikio makubwa katika suala
zima la kuimarisha amani na utulivu Mkoani hapa.
0 comments:
Post a Comment