
AU inajadili swala hili baada ya ICC kupuuza ombi la kutaka kuhamisha kesi za Kenyatta na Ruto
Marais wa Afrika wanakutana
wikendi hii mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kujadili uhusiano wa bara
la Afrika na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC.
Mkutano huu maalum umeitishwa baada ya ICC
kukataa ombi la wanachama 54 wa Muungano wa Afrika kurejesha kesi za
Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto nyumbani.
Viongozi hao wanatarajiwa kujadili hoja ya kujiondoa kutoka kwa mahakama hiyo.
Baada ya miezi kadhaa ya kutofautiana kati ya
ICC na AU, viongozi wa Afrika wanakutana katika makao makuu ya AU katika
kile kinachosemekana ni kutafakari upya uhusiano wa bara hilo na
mahakama ya ICC.
Kwa mujibu wa AU, mahakama hiyo ya ICC imekosa
kushughulikia ombi lililowasilishwa na AU mwezi Mei kuhusu kesi za
Kenya. AU inasema kuwa ICC ina njama za kibaguzi dhidi ya viongozi wa
kiafrika.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake
William Ruto wanakabiliwa na kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu
katika mahakama hiyo.
Kesi yao inahusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu Kenya mwaka 2007/2008 ambapo zaidi ya watu 1100 waliuawa.
Hata hivyo viongozi hao wamekanusha madai hayo.
Bunge la Kenya ambalo lina idadi kubwa ya
wabunge wa mrengo wa Jubilee unaotawala nchi, tayari lieanzisha hoja ya
kuondoa Kenya kutoka katika mahakama ya ICC.
Lakini serikali ya Kenya imesema haijashinikiza
nchi za Afrika kujadili hoja ya kujiondoa ICC licha ya kuungwa mkono na
majirani zake kama Uganda na Rwanda.
Naibu mwenyekiti wa AU Erastus Mwencha, ameambia www.azizicompdoc.blogspot.com kuwa swala hilo sasa ni zaidi ya kutaka tu kujiondoa ICC.
Wadadisi hata hivyo wanasema kuwa huenda AU
isikubali kwa ujumla kujiondoa ICC. Baadhi ya nchi kama Ghana na
Botswana tayari zimepinga hatua ya kujiondoa ICC.