Tuesday, December 18, 2012

Duka la Kariakoo Bazaar Lavamiwa na Majambazi na Kuporwa Mil. 40

 Tukio hilo lilitokea kwenye mishale ya saa 3:45, majambazi walimvamia mhasibu wa duka hilo aitwae Kishori Sheti na kumpora mamilioni hayo ya fedha na kutoweka nayo.
Uvamizi wa duka hilo lililopo kwenye makutano ya Mtaa wa Swahili na Narung’ombe Kariakoo ulisababisha vurugu kubwa hadi wapita njia wengine kutaka kupoteza maisha yao.
Akielezea tukio hilo ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile amesema kuwa majambazi yapatayo manne yalimvamia mhasibu huyo na kumpora begi lililokuwa na fedha hizo.
Amesema mhasibu huyo alikuwa anatokea kwenye duka lao jingine lililopo mtaa wa Livingistone na Maina akiwa amebeba begi lililokuwa na fedha hizo akiwa na dhumuni la kuzileta dukani hapo.
Amesema mara baada ya mhasibu huyo kushuka ndani ya gari lililomleta alivamiwa na watu watatu huku wawili kati yao wakijaribu kuvuta begi alilokuwa amebeba huku mwingine akimtishia kwa bastola.
Kamanda Shilogile alisema kuwa mlinzi wa mhasibu huyo aliyefahamika kwa jina la Joseph Hassan aliyekuwa amebaki ndani ya gari baada ya kuona mhasibu huyo amevamiwa alitoka haraka kwenye gari hiyo na kuanza kupiga risasi hewani.
Majambazi hayo kusikia mlio wa risasi walijibu mashambulizi na kupiga risasi zingine mbili hewani kwa lengo la kumtisha mlinzi huyo.
Mlinzi huyo baada ya kuona risasi hizo zikimiminika alionekana kulegalega na majambazi hao kufanikiwa kupora begi lile na kufanikiwa kuingia kwenye gari walilokuwa wakilitumia aina ya Toyota Corolla lenye namba T 429 AAT na kufanikiwa kutoweka na begi hilo lililokuwa na fedha.
Kamanda Shilogile aliendelea kusema kuwa mlinzi huyo kuona majambazi yamefanikiwa kutoweka na begi alianza kurusha risasi kuelekea kwenye gari walilokuwa wakilitumia majambazi hayo bila kujali usalama wa raia wengine.
Akiendelea kusimulia mkasa huo Shilogile amesema kuwa, mlinzi huyo alifanikiwa kupasua kioo cha nyuma cha gari hilo lakini hakuweza kufanikiwa kupata fedha hizo.
Amesema kutokana na sakata hilo Jeshi la polisi limefanikiwa kuwakamata watu watano, watatu kati yao kutoka kwenye duka hilo ambao inasemekana wanaweza wakahusika kwa namna moja ama nyingine.
Wakati huo huo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova, amewalaumu wamiliki wa maduka makubwa katika jiji la Dar es Salaam kwa kutotoa taarifa kwenye vituo vya polisi kupatiwa msaada wakati wa kwenda kusafirisha ama kuchukua fedha zao.
“Wafanyabiashara na wananchi wengine wanajiamini sana kusafirisha fedha bila kutumia jeshi la polisi, wakati tulishatangaza na kutoa wito kwa wananchi wote watumie jeshi wakati wa kusafirisha fedha zao na hakutakuwa na gharama yoyote lakini kutokana na kutoamini Jeshi hili ndio matukio ya ujambazi yanatokea kama haya” alisema Kova
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About