Wednesday, February 27, 2013

MADUDU YALIYOMFANYA PAPA AJIUZULU HAYA HAPA

*Makachero waibua kashfa nzito
*Papa akabidhiwa ripoti ya usaliti, ufisadi
*Keith Kardinali O'Brien aachia ngazi

SIKU moja kabla ya kung’atuka kwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Benedicto XVI, kwenye wadhifa wake, imeripotiwa kuwa uamuzi wa kuachia ngazi aliufikia baada ya kubaini vitendo vya usaliti, ufisadi na ushoga ndani ya kanisa ambavyo kutokana na umri wake mkubwa hakuwa na uwezo na nguvu za kukabiliana navyo.
Gazeti la Italia, La Repubblica, limekariri taarifa za kiintelijensia za ndani ya kanisa hilo, zilizokuwa zikieleza kuwa makachero wa Vatican, walimfikishia Papa Benedicto ripoti yao ya uchunguzi ya mwenendo wa mlolongo wa matukio ya usaliti, ulaji rushwa na kashfa ya chini kwa chini ya uwepo wa vitendo vya ushoga katika Vatican.

Katika taarifa yake hiyo, gazeti hilo liliripoti kuwa, Papa Benedicto baada ya kuichambua ripoti hiyo na kubaini uwezekano wa kuibuka mgogoro wa kikanisa iwapo hatua za kushughulikia kashfa hizo hazitachukuliwa huku yeye mwenyewe akijitathimini afya yake na kubaini hataweza kuhimili vishindo vya kukabiliana na kashfa hizo, Februari 11 mwaka huu, alitangaza kujiuzulu.

Katika tangazo lake hilo, Papa Benedicto alieleza kuwa anakusudia kujiuzulu rasmi nafasi yake itakapofika Februari 28 kwa sababu hawezi tena kutekeleza majukumu yake kutokana na umri wake.

Wakati hatua ya kujiuzulu kwa Papa ikisubiriwa kwa shauku kubwa na mamilioni ya watu duniani sambamba na uchaguzi wa Papa mpya, ripoti ya kikachero kutoka ndani ya Vatican iliyoripotiwa na gazeti La Repubblica, ilieleza kuwa makardinali watatu, akiwemo mkuu wa zamani wa masuala ya ulinzi wa Vatican, walitakiwa ufanyike uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, ushoga na ufisadi ulioibuliwa na uchapishwaji wa nyaraka za siri za papa katika kashfa iliyopewa jina la ‘Vatileaks.’

Ripoti hiyo inaeleza zaidi kuwa makardinali hao watatu waliwasilisha ripoti ya uchunguzi wao kwa papa Desemba 17 mwaka jana, katika vitabu vikubwa viwili vyenye majalada ya rangi nyekundu vyenye takriban kurasa 300 vilivyokuwa na ramani halisi ya uovu na ufisadi ndani ya kile walichokiita ‘Holy See.’

Kwamba Papa baada ya kupokea ripoti hizo na kuzipitia, akiwa hata hajazitoa mezani kwake alipochukua uamuzi aliokuwa ameuficha kwa muda mrefu pale alipopokea ripoti nyingine iliyokuwa ikielezea kashfa za aina hiyo ya makachero wa Vatican.

Kashfa ya Vatileaks ilitokea Januari mwaka jana, baada ya mlolongo wa nyaraka za ndani za kinachoitwa Holy see, zilipovuja kwenye vyombo vya habari vya Italia na kusababisha sintofahamu kwa taifa zima.

Hata hivyo, wakati tukio hilo likizidi kufukuta ndani ya Vatican, Mwanahabari wa Kiitaliano, Gianluigi Nuzzi, aliongeza mafuta kwenye moto baada ya kutoa kitabu chake kiitwacho ‘His Holiness.’

Kitabu hicho kinaangazia vita vya madaraka ndani ya Vatican kwa kutoa nyaraka na barua za siri kutoka kwa baadhi ya viongozi waandamizi wa kanisa kwenda kwa Papa na kwa katibu wake muhtasi.

Mei mwaka jana, mamlaka za Vatican zilimkamata Paolo Gabriele, msaidizi wa papa kwa tuhuma za kuhusika na uvujishaji wa nyaraka hizo za siri na kumuhukumu kifungo cha miezi 18 jela, hata hivyo baadaye alisamehewa.

Wakati huo huo, Kardinali Keith O'Brien wa Uingereza, amejiuzulu wadhifa wake kutokana na tuhuma za kwenda kinyume na matakwa ya kikasisi mapema miaka ya 1980.

Kardinali Keith O'Brien ambaye alikuwa astaafu uongozi wa kanisa hilo mwezi ujao, akiwa na umri wa miaka 75, ameachia madaraka kama Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo nchini Scotland.

Kutokana na uamuzi huo, hatarajii kusafiri kwenda Vatican kushiriki kumchagua Papa ajaye baada ya Papa Benedict XVI kutangaza kuwa ifikapo kesho ataachia madaraka ya kuliongoza kanisa hilo.

Imeripotiwa kuwa, Askofu huyo mkuu wa zamani wa Kanisa la Andrews na Edinburg, ameshutumiwa na mapadre watatu ambao waliwasilisha malalamiko yao wiki mbili zilizopita kwa mwakilishi wa Papa nchini Uingereza, kuwa aliwavunjia heshima makasisi hao miongo mitatu iliyopita.

Wafuatiliaji wa mambo wanaeleza kuwa, kujiuzulu kwa kardinali huyo kunaongeza shinikizo kwa makardinali wengine wanaokabiliwa na tuhuma juu ya namna walivyoshughulikia kashfa za ngono zilizowakabili watumishi wa kanisa hilo kuachia ngazi.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About