Wednesday, December 25, 2013

WATAALAMU WA UCHUMI WAIPINGA TANESCO KUPANDISHA BEI YA UMEME

http://www.azizicompdoc.blogspot.com/
Baadhi ya wachumi na wadau mbalimbali wa nishati ya umeme wameikosoa hatua ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) baada ya kuongeza gharama za umeme kwa maelezo kuwa hatua hiyo itamkandamiza mwananchi wa kawaida.
Kauli hizo zimekuja siku moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za umeme huku kukiwa na ongezeko kubwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana, baadhi yao walisema hatua iliyochukuliwa siyo mwarobaini wa matatizo ya umeme, badala yake unahitajika mfumo mpya wa kiutendaji ili kuinusuru Tanesco.
Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Felix Mosha alisema kitendo cha kuongeza gharama ya umeme kitapunguza ushindani wa kibiashara.
“Wananchi walitarajia ongezeko la viwango vya gharama ambavyo vingeweza kuongeza ushindani wa bidhaa zetu dhidi ya zile zinazotoka nje. Tangazo hilo la Ewura linatakiwa kutazamwa upya,” alisema Mosha.
Pia alisema kuwa gharama za uzalishaji nchini zimekuwa kubwa kutokana na matumizi ya jenereta ambazo ni mara nne zaidi ya mitambo ya kawaida.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEO’s Roundtable), Ali Mufuruki alitofautiana msimamo huo wa wenye viwanda akisema hatua hiyo ni sahihi endapo itakuwa suluhisho la kupunguza changamoto za kupatikana kwa umeme.
Mufuruki alisema Tanesco imekuwa na tatizo kubwa la kununua umeme kwa bei ya juu ukilinganisha na ankara inazotuma kwa wateja wake.
“Tusiangalie zaidi kumuathiri mwananchi na kupunguza ushindani wa kibiashara tu kwani mtu anaweza kujipanga. Ni heri bei ipande kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha kuliko kuwa na umeme wa kubabaisha,” alisema Mufuruki.
Wanaharakati
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema mwananchi amebebeshwa mzigo huku baadhi ya watumishi wa Tanesco wakituhumiwa kufanya ubadhirifu.
“Leo hii mamalishe na wajasiriamali wadogo watafanyaje kazi zao? Kwa nini wadaiwa sugu wa kodi wasingebebeshwa mzigo huo... Mimi ningekuwa na uwezo ningetembea peke yangu kuandamana kwa sababu wananchi wanaona lakini wanaendelea kuvumilia maumivu yasiyostahili,” alisema Dk Bisimba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya alisema kwa ongezeko hilo la bei, Serikali haina mpango madhubuti wa kupunguza umaskini wa Mtanzania.
“Kuna kila sababu ya Serikali kukaa chini na kutafakari upya juu ya gharama hizo za umeme ili kumsaidia mwananchi kwa sababu hakuna uhusiano wa kupanda kwa gharama hizo na maisha anayoishi kwa sasa na badala yake itaendelea kumuumiza,” alisema Usu.
TUCTA yatoa tamko
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya alisema shirikisho hilo limetoa maazimio kadhaa ikiwamo kuitaka Serikali kuongeza mishahara kwa wafanyabiashara ili kutengeneza uhusiano wa ongezeko hilo na kipato cha mshahara uliopo.
“Kama imeona ni vyema kuongeza bei hizo, basi iongeze hata mishahara kwani ongezeko la Tanesco ni asilimia 40 kwa mtu wa chini wakati mshahara wake ulipanda kwa asilimia 25 tu. Kwa mazingira hayo ni lazima ataumia tu,” alisema Mgaya.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kiuchumi alisema Tanesco itahitaji kuwa na menejimenti yenye uwezo wa kulisimamia shirika hilo ikiwa ni pamoja na kudhibiti upotevu mkubwa wa fedha.
“Hakuna menejimenti ya kusimamia shirika, tunataka uongozi wa watu wenye uwezo wa kulinusuru shirika ambao wataokoa upotevu wa fedha,” alisema Profesa Lipumba.
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Constantine Akitanda alisema kupanda kwa gharama za umeme kunaathiri sekta nyingine zinazotegemea huduma kutoka Tanesco, hivyo wananchi wategemee mabadiliko ya bei za bidhaa.
“Ni bora wangeboresha miundombinu ya Tanesco na kuondoa mikataba mibovu ambayo inawafanya watumie sehemu kubwa ya mapato yao kulipa madeni,” alisema Akitanda.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About