Friday, January 17, 2014

MRADI WA MABASI YAENDAYO KASI KUSIMAMIWA NA KAMPUNI YA KIHOLANZI


unnamed (10)
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa),Bwana Jumane Sagini akiongea na waandishi wa habari muda mfupi mara baada ya kusainiwa mkataba wa kusimamia mradi wa mabasi yaendayo haraka kati ya Wakala wa Mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (DART) na Kampuni ya Uholanzi ya REBEL Group jijini Dar es Salaam jana. Wengine kulia ni Kaimu Afisa Mkuu wa DART, Bi. Asteria Mlambo na Mshauri wa Masuala ya Fedha wa REBEL Group, Bw.Jeroen Kok (kushoto).
unnamed (11)
Kaimu Afisa Mkuu wa DART, Bi. Asteria Mlambo(kulia) akibadilishana nyaraka za makubaliano na Mshauri wa Masuala ya Fedha wa REBEL Group, Bw.Jeroen Kok (kushoto) muda mfupi baada ya kusaini mkataba jijini Dar Es Salaam jana anayeshuhudia katikati ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa),Bwana Jumanne Sagini.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 
Mradi wa mabasi yaendayo kasi umepiga hatua nyingine kubwa baada ya kupatikana kwa kampuni ya washauri kutoka Uholanziya Rebel Group, itakayofanya kazi ya ushauri wakati wa kuanza mradi huo jijini Dar.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kampuni hiyo ya REBEL Group ya Uholanzi kushinda zabuni na kusaini mkataba wa kufanya kazi hiyo kati yake na Wakala wa Mabasi yaendayo kasi (DART).
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).Bw. Jumanne Sagini aliyeshuhudia utiaji saini huo aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya kusainiwa kwa mkataba huo kuwa mradi huo sasa unaelekea hatua za mwisho kabisa kuanza kufanya kazi za usafiri wa jiji la Dar es Salaam.

Kampuni hiyo iliyosaini mkataba na DART ilishinda zabuni miongoni mwa Kampuni sita zilizoingia katika hatua ya mwisho ya ushindani huo.
Kwa upande wa kampuni hiyo mkataba huo ulisainiwa na mshauri wa maswala ya fedha,Bw. Guillaume Remy, wakati DART iliwakilishwa na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji, Bi. Asteria Mlambo.
“Hatua hii ni muhimu kwa mradi huu nyeti kwa nchi yetu,”amesema Katibu Mkuu huyo.
Amesema kutokana na kufikiwa kwa hatua hiyo, kampuni hiyo sasa itasaidia kutoa ushauri wa jinsi ya kupatikana watoa huduma kama vile wakusanyaji nauli, na watoa huduma wengine watakaowezesha mfumo huo kufanya kazi kwa ufanisi.

Wadau wengine watakaoshiriki katika mchakato huo ni pamoja na DART wenyewe, watoa huduma za daladala na wananchi wote katika kufanikisha jambo hilo.
“Tumewaambia wenzetu wa kampuni hii kuwa kazi hii ni nzito lakini lazima tushinde kwa ajili ya kutoa usafiri mzuri kwa wananchi,” amesema na kuongezakuwa swala hilo litasaidia kukabiliana na changamoto ya foleni iliyopo jijini Dar es Salaam.
Aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inafanya kazi hiyo vizuri na kuwa serikali ipo tayari kutoa msaada pale zitakapojitokeza kero ambazo ni kikwazo kwa utekelezaji.
Amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP) ambapo sekta binafsi itawekeza dola za Kimarekani milioni 180 na sekta ya umma dola za Kimarekani milioni 250.
Afisa Mwandamizi kutoka kampuni hiyo ya Rebel Group, Bw. Jeroen Kok alisema kampuni yao ipo tayari kufanya kazi iliyoomba ili kusaidia Tanzania kupata huduma ya kisasa ya usafiri na kupunguza foleni ambayo ni kero kubwa.

“Kampuni yetu ina uzoefu wa kazi hizi ambapo tumewahi kufanya kazi Bara la Ulaya, Asia, Ameria, Afrika ya Kusini na sasa tupo Tanzania ambayo itakakuwa mfano mzuri katika eneo hili la Afrika juu ya utendaji wetu na mfumo huu wa usafiri,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala mkoa wa Dar es Salaam (DARCOBOA), Bw. Sabri Mabruki amesema mradi huo ni mkubwa na utasaidia katika kufikia malengo ya serikali katika sekta ya usafirishaji jijini Dar es Salaam.
“Sisi wamiliki wa daladala tupo begakwabega tangu mradi huu ulipoanzishwa na tumekuwa tukishiriki na tutaendelea kushiriki ili malengo yake yaweze kufikiwa,”amesema Bw. Mabruki.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About