LiberatusSabas
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas.
Watu wanne ambao bado hawajafahamika wanaume wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 35 wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa baada ya kupigwa risasi na askari Polisi. Tukio hilo lilitokea jana tarehe 21.02.2014 muda wa saa 1:00 jioni katika bar moja iitwayo Pama iliyopo maeneo ya Makao Mapya jijini hapa.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema kwamba, tukio hilo lilitokea mara baada ya jeshi la polisi Mkoani hapa kupata taarifa toka kwa raia wema kwamba watu hao walikuwa wanapanga kwenda kufanya tukio la uhalifu katika kituo kimojawapo cha kuuzia mafuta kilichopo jijini hapa ambapo ufuatiliaji wa taarifa hiyo ulianza.

Ilipofika muda huo askari hao walikwenda katika bar hiyo na mara baada ya majambazi hao kuwaona askari hao walihisi wanafuatiliwa ndipo mmojawao ghafla alitoa bastola  na kufyatua risasi tatu ambapo moja ilimparaza askari mmoja aitwaye F. 1416 D/Ssgt Richard katika mkono wake wa kushoto
 “Kufuatia hali hiyo askari nao waliamua kujibu mapigo kwa kupiga risasi ambapo wanne kati ya watano walijeruhiwa na mmojawao alifanikiwa kukimbia akiwa na silaha inayosadikiwa kuwa ni SMG”. Alisema Kamanda Sabas.
Kamanda Sabas alisema kwamba, majambazi hao walifariki dunia wakiwa njiani kuelekea hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu na miili yao imehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya utambuzi toka kwa ndugu na jamaa wa karibu.

Aidha Kamanda Sabas alisema, katika eneo la tukio askari hao walipata bastola moja aina ya Star yenye namba 42640 FNH PISTOLE MODEL KAL 7.65 ikiwa na risasi tatu katika magazine, maganda matatu ya risasi pamoja na begi moja dogo la mgongoni lenye rangi nyekundu likiwa na risasi nne hivyo kufanya jumla ya risasi saba kupatikana.
Bado Jeshi la Polisi Mkoani hapa linaendelea na upelelezi kuhusiana na tukio hilo ikiwa ni pamoja na kumtafuta mtuhumiwa mmoja aliyekimbia.
Kufuatia tukio hilo Kamanda Sabas aliendelea kuwashukuru wananchi wa Arusha kwa ushirikiano wao mkubwa wanaoutoa kwa jeshi la Polisi Mkoani hapa na kuwasihi waendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu hali itakayosaidia kukomesha matukio ya uhalifu mkoani hapa.
 Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha