Maswali juu ya utaratibu uliotumika kutoa fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye Akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutokana na mvutano baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na IPTL yameanza kupata majibu.
Wakati mmiliki kwa Kampuni ya VIP Engineering and
Marketing, James Rugemalira ameibuka na kukiri kuwa yeye ni miongoni mwa
waliolipwa fedha hizo huku uongozi wa IPTL ukifafanua utata kuhusu
mkataba wake na Tanesco na jinsi kampuni hiyo ilivyouzwa jumla kwa Pan
African Energy.
Katika ufafanuzi wake, Rugemalira alisema kati ya
fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow, yeye akiwa mwanahisa wa IPTL
alilipwa Dola za Marekani 75 milioni (Sh120 bilioni), alizoziita
‘vijipesa vya ugoro’ sawa na asilimia 30.
Alisema baada ya kuuza hisa zake kwa Kampuni ya
Pan African Power (PAP) aliruhusu pia asilimia 70 ya hisa za mbia
mwenzake, Mechmar kutoka Malaysia ziuzwe pia kwa PAP.
Alisema kwenye akaunti hiyo kulikuwapo na Dola za
Marekani 120 milioni, tofauti na kiwango kilichotajwa na Gavana wa BoT,
Profesa Benno Ndulu aliyesema fedha hizo zilikuwa Dola 122 milioni.
Rugemalira alisema pia kuwa hatua ya kufikiwa kwa
hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Jaji John
Utamwa Januari 17, mwaka 2014 saa 8: 30 usiku, ilitokana na Waziri wa
Nishati kumuomba wamalize kesi zilizokuwa mahakamani.
“Niliiambia Serikali kuwa nyie mmeibiwa na sisi
tumeibiwa. Mimi nikawaambia kuwa ‘the end justify the means’ (jambo la
muhimu ni matokeo, si njia ulikopitia), mwisho tulikubaliana kwamba kwa
masilahi ya Taifa tumalize kesi hii, na mimi ndiyo nikalipwa hivyo
vijipesa vya ugoro,” alisema Rugemalira.
Hatua ya kutoa fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya
Escrow na kugawiwa kwa VIP Engineering na PAP, imefikiwa huku mkopeshaji
wa IPTL, Benki ya Standard Charted ya Hong Kong (SCB-HK), inayodai Dola
za Marekani 145 milioni (Sh234.456 bilioni), ikiwa haijalipwa na wala
haijajulikana italipwa kwa kutumia kanuni gani.
Itakumbukwa kuwa, baada ya benki za Malaysia
zilizokuwa zimeikopesha IPTL kuyumba kiuchumi, deni la benki hizo
lilinunuliwa na SCB-HK.
“Tumeridhia kuwa hizo asilimia 70 zichukuliwe na
PAP na Standard Charted anadai kwamba yeye ndiye mkopeshaji na dhamana
yake ni hiyo mitambo, kitu ambacho siyo kweli. Lakini kama ni kweli
aende mahakamani kuthibitisha,” alisema Rugemalira.
Hukumu iliyotolewa Februari 12, 2014 na Kituo cha
Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji cha Washington DC,
Marekani, ilitaka pande hizo mbili zikae na kukubaliana namna ya
kukokotoa gharama ambazo shirika hilo la umeme linapaswa kuilipa benki
hiyo.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana, Rugemalira
alionekana kujikanganya juu ya kuitambua SCB-HK, kuna wakati alisema
haitambui na hivyo haikuwa na fedha zilizokuwa Escrow na wakati mwingine
alisema bado anaidai benki hiyo na kesi ipo mahakamani.
Rugemalira alisema kwamba alikuwa Mkurugenzi wa
IPTL hadi Januari 24, mwaka huu alipong’atuka, ingawa pia alisema baada
ya kung’atuka alikuwa bado anaiwakilisha IPTL kwenye vitu vingi, ikiwa
ni pamoja na kuuza hisa zake kwa PAP.
Katika mkutano huo wa waandishi wa habari,
Rugemalira alitumia muda mrefu kuipigia debe PAP akisema ni kampuni bora
inayoweza kuzalisha umeme kwa bei nafuu.
“Swali la kujiuliza sasa, IPTL ni nani, jibu lake ni PAP,” alisema Rugemalira.
Pia kuhusu suala la Mkataba wa IPTL na Tanesco
kuanza 1995 na kutarajiwa kufikia kikomo 2015, Rugemalira alisema siyo
sahihi na kuwa mkataba huo ulianza 2002 na ulitarajiwa kukamilika 2022.
Akizungumzia suala hilo, Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali (CAG), Ludovick Utouh alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala
hilo kwa kuwa bado hana taarifa rasmi.
“Kwa sasa siwezi kusema chochote, hizi taarifa
ndiyo kwanza nazisoma, lakini kama itagundulika kuna vitu vimekiukwa,
kuna vyombo husika vitakavyochukua hatua,” alisema Utouh.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usajili, Ufilisi
na Udhamini (Rita), Philip Saliboko alisema ofisi yake ilikabidhiwa
kazi ya ufilisi wa IPTL na Mahakama mwaka 2008 lakini mahakama hiyohiyo
iliamuru Rita inyang’anywe ufilisi huo, Septemba 5, mwaka jana.
Saliboko alisema baada ya kunyang’anywa mamlaka ya
ufilisi, IPTL ilikabidhiwa kwa Kampuni ya Pan African Energy Ltd (PAT)
iliyoelezwa kuinunua.
“Hata hivyo, ofisi yangu haikupewa ufilisi wa muda
mrefu, ilipewa wa muda mfupi, kwa hiyo majukumu yangu hayakufikia yale
ya kuuza au kufilisi mitambo, bali kuuangalia kama IPTL ipo salama hadi
hatua nyingine zitakapotajwa,” alisema.
Mwanasheria wa IPTL, Joseph Mwakandege alisema PAT ilinunua hisa
kutoka kwa VIP Engineering na Nechmar kwa uwiano wa asilimia 70 kwa 30
na baada ya kununuliwa hisa hizo, Mahakama iliamuru kuwa PAT iwe mbia wa
jumla wa Kampuni ya IPTL.
Mwakandege alipohojiwa kuhusu mkanganyiko wa
mkataba kati ya Serikali na IPTL, alisema makubaliano baina ya pande
hizo yalikuwa ni yale ya Kujenga, Kuendesha na Kumiliki (BOO), hivyo
mali za IPTL zinabaki kuwa zake hadi baada ya mkataba kumalizika 2015.
Alisema mkataba huo haukuwa na kipengele cha kuiachia Serikali mitambo yake ya kuzalisha umeme.
Kuhusu Akaunti ya Escrow, mwanasheria huyo alisema
haikuwa akaunti ya Serikali, bali fedha zilizokuwamo zilikuwa mali ya
IPTL baada ya kuwapo kwa mgogoro baina ya wadau – IPTL na Tanesco.
“Kwanza ifahamike kuwa Escrow ilianzishwa kwa
ajili ya wadau. Baada ya VIP Engineering na Nechmar kuuza hisa, akaunti
ilikabidhiwa kwa PAT,” alisema.
Alisema baada ya mgogoro huo kutokea, kila mdau aligawiwa kiasi chake cha hisa na kuondoka, hivyo fedha zilizobaki ni za IPTL.
Alikanusha kuwa Akaunti ya Escrow ilikuwa na Dola za Marekani 270 milioni, bali Dola 105 milioni na wala si zaidi ya hapo.
“Nyinyi mnafikiri Escrow ni ya Serikali. Mnafikiri Serikali ni wajinga na mafisadi kiasi hicho?” alisema.
0 comments:
Post a Comment