Wabunge wa Senegal,
wameidhinisha sheria ambayo itaruhusu kuundwa kwa mahakama maalum ya
Muungano wa Afrika kumfungulia mashtaka aliyekuwa kiongozi wa Chad
Hissene Habre.
Habre mwenye umri wa miaka sabini amekuwa
akitumikia kifungo cha nyumbani tangu mwaka wa 2005, nchini Senegal,
ambako alitorokea baada ya kuondolewa madarakani mwaka wa 1990.Kiongozi huyo wa zamani amekanusha madai ya kuhusika na mauaji na dhuluma dhidi ya maelfu ya wapinzani wake.
Mwandishi wa BBC nchini Senegal anasema uamuzi huo, ni habari njema kwa mashirika ya kutetea haki za kibinadam ambayo, yamekuwa yakishinikiza serikali ya nchi hiyo kumfungulia mashtaka kiongozi huyo wa zamani wa Chad kwa miaka kadhaa.
Malumbano makali yamekuwa yakiendelea njini Senegal kuhusu hatma ya Bwana Habre, huku serikali ya rais wa zamani wa nchi hiyo Abdoulaye Wade ikibadili msimamo wake mara kadhaa ikiwa itamfungulia mashtaka au la.
Mashirika ya kutetea haki yaafiki uamuzi wa kumshtaki Habre
''Katika kipindi cha miaka minane, serikali ya Rais Macky Sall, imeafikia mambo mengi hasa kuhimiza waathiriwa walioteswa wakati wa utawala wa miongo miwili wa rais Habre kulipwa fidia kutokana na uvumilivu wao'' Alisema Reed Brody afisa mmoja wa shirika la kutetea haki za kibinadam lililo na makao yake nchini Marekani la Human Rights Watch.Bunge la Senegal lilipitisha sheria hiyo kufuatia makubaliano ya mwezi Agosti mwaka huu kati ya Muungano wa Afrika AU na serikali ya nchi hiyo, ya kutenga fedha zitakazotumiwa na mahakama hiyo maalum.
Msemaji wa wizara ya haki nchini Senegal ameiambia BBC kuwa AU sasa itaanza shughuli ya kuwateuwa majaji kuambatana na orodha iliyopendekezwa na waziri wa wizara ya haki.
Rais wa mahakama hiyo anatarajiwa kuteuliwa kutoka taifa lolote la Afrika na inatarajiwa kuwa uchunguzi kuhusu keshi hiyo itadumu kwa muda wa miezi kumi na mitano, ambapo uamuzi utachukuliwa ikiwa Bwana Habre atafunguliwa mashtaka au la.
0 comments:
Post a Comment