Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba
ameitaka Serikali kutafuta ufumbuzi wa haraka wa matatizo ya kiuchumi,
kwa kuwa hali ilivyo sasa ni mbaya.
Profesa Lipumba ambaye pia ni profesa wa uchumi
alisema hivi karibuni Dar es Salaam kuwa hali ya uchumi imezidi kudorora
na kusababisha maisha ya wananchi wengi kuwa magumu.
“Vijana wa siku hizi wengi hawana simile
kushughulika na mambo yanapokwenda sivyo, ajabu ni kwamba wanaofanya
mambo hayo yawe magumu wamekuwa wepesi wa kutetea kwa hoja zisizo na
msingi kwa masilahi yao binafsi,” alisema.
Akizungumzia maazimio yaliyofikiwa kwenye Kikao
cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kilichofanyika Desemba 21-22
mwaka huu Dar es Salaam, alisema hatua ya kupandishwa kwa gharama za
umeme iliyotangazwa hivi karibuni na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
ni miongoni mwa mambo ambayo yanaendelea kuongeza ugumu wa maisha kwa
wananchi, jambo ambalo lingeweza kuzuilika kwa shirika hilo kudhibiti
wizi wa nishati hiyo.
Kuhusu hali ya kisiasa nchini, Profesa Lipumba
alisema Baraza Kuu limetoa wito kwa vyombo vya Dola kuwa na weledi na
uadilifu na kuacha kutekeleza amri za wanasiasa zisizojali utawala wa
sheria na haki za binadamu ili vipunguze uhasama baina yao na raia.
“Serikali pia isitumie Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) katika kushughulikia masuala ya uvunjifu wa sheria
katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, badala yake kazi hiyo ifanywe na
Jeshi la Polisi kwa mujibu wa taratibu za kisheria. Nao pia waongezewe
uwezo wa kiutendaji,” alisema.
Alisema CUF inaona si vyema kutumia JWTZ kudhibiti
vurugu kwa kuwa wanajeshi hao hawana mafunzo ya kukamata wananchi wenye
tuhuma za uhalifu isipokuwa wamefundishwa jinsi ya kulinda usalama wa
nchi katika mipaka.
0 comments:
Post a Comment