Mkuu wa Majeshi Nchini, Davis Mwamunyange na
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema nao wametakiwa kujiuzulu
kutokana na uozo uliobainika katika ripoti ya Operesheni Tokomeza
Ujangili, iliyosababisha Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri
wake wanne.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar
es Salaam katibu wa madiwani wa jiji hilo, Julian Bujugo alisema wakuu
hao wanapaswa kujiuzulu kwa kuwa wao ndio wanaotoa amri kwa askari wao
na siyo mawaziri.
“Nao wanatakiwa kuchukua uamuzi wa kujiuzulu kama
hatua ya kuonyesha uwajibikaji wao, askari wao wamefanya maovu makubwa,”
alisema. Alisema kama wakuu hao wa watakaidi agizo la madiwani
watalipeleka suala hilo kwa Rais Kikwete.
“Watendaji wa Serikali ndio chanzo cha uonevu,
hata mawaziri ‘mizigo’, nao wanatakiwa kujiuzulu. Alimtolea mfano Waziri
wa Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Bujugo alisema ameshindwa
kuwasimamia wakulima na kusababisha mvutano na vurugu katika Sekta ya
Kilimo.
Chiza alitajwa kama waziri ‘mzigo’ na Kamati Kuu ya CCM iliyokutana wiki mbili zilizopita chini ya uenyekiti wa rais Kikwete.
Bujugo ambaye ni diwani wa Kata ya Magomeni
alisema mbali na wakuu hao wa ulinzi na usalama, pia wakuu wote wa
wilaya waliohusika kusimamia operesheni hiyo nao wanapaswa kuwajibika
kwa kuwa walijua na waliona wazi vitendo vichafu walivyofanyiwa wananchi
lakini walikaa kimya.
Ripoti ya tume ya kuchunguza Operesheni Tokomeza
Ujangili ilisomwa bungeni mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita na
mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembelii na kuwango’a mawaziri hao.
Waliong’olewa ni Waziri wa Maliasili na Utalii,
Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi,
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David na Waziri wa Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
akiwa njia panda kutokana na wabunge kuendesha mpango wa chini chini wa
kupiga kura ya kutokuwa na Imani naye kwa maelezo kuwa ameshindwa
kuwasimamia mawaziri wake.
0 comments:
Post a Comment