Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
wiki hii atahudhuria mikutano miwili mikubwa ya kimataifa ukiwamo wa
kujadili amani na usalama Barani Afrika kwa mwaliko wa Rais Francois
Hollande wa Ufaransa.
Rais
Kikwete ambaye aliondoka nchini usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Desemba
4, 2013, atakuwa mmoja wa viongozi wa Afrika ambao watahudhuria Mkutano
Kati ya Marais wa Afrika na Ufaransa, ambao utafanyika kwa siku mbili
katika Kasri ya Elysee mjini Paris kuanzia keshokutwa Ijumaa, Desemba 6,
2013.
Mkutano
huo uliopewa jina la Elysee Summit utakuwa ni mkutano wa 26 wa Mikutano
ya Wakuu wa Nchi za Afrika na Ufaransa ambao walikutana kwa mara ya
kwanza mwaka 1973 kwa madhumuni ya kuzikutanisha Ufaransa na makoloni
yake ya zamani katika Afrika.
Kwa
mikutano miwili ya kwanza, washiriki walikuwa ni marais wa nchi za
Afrika zilizokuwa makoloni ya Ufaransa lakini mwaka 1976 zilialikwa nchi
zinazozungumza lugha ya Kireno katika Afrika kama watazamaji tu.
Mwaka
1981 jina na madhumuni ya mkutano huo yalibadilika na ukaanza kuitwa
The Conference of Heads of States and Government of Africa and France na
mwaka 1996 mkutano huo ulifunguliwa kwa nchi zote za Afrika bila kujali
zinazungumza lugha gani. Awali mkutano huo ulikuwa unafanyika kila
baada ya miaka miwili, sasa ni kila baada ya miaka mitatu.
Kama
ilivyokuwa mkutano uliopita uliofanyika mwaka 2010 mjini Nice,
Ufaransa, mada kuu ya Mkutano huo ni kujadili amani na usalama katika
Bara la Afrika vikiwemo vita ndani ya nchi mbalimbali, uharamia kwenye
bahari, biashara ya dawa za kulevya, ugaidi na ujambazi wa vikundi na
jinsi mambo hayo yanavyoathiri Afrika na Ufaransa.
Aidha, Mkutano huo utajadili mada nyingine mbili ambazo ni Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Rais
Kikwete na mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Hollande watakuwa
Wenyeviti-Wenza wa kikao kitakachojadili madhara ya Mabadiliko ya Tabia
Nchi. Rais Kikwete atakuwa Mwenyekiti-Mwenza wa kikao hicho katika
nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Umoja wa
Afrika (AU) Juu ya Mabadiliko ya Tabia Nchi (CAHOSCC).
Rais
Kikwete anatarajiwa kuwaeleza viongozi wenzake matokeo ya Mkutano wa
COP19/CMP9 uliofanyika karibuni mjini Warsaw, Poland kujadili suala zima
la Madhara ya Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Mkutano
mwingine mkubwa ambao Rais Kikwete atahudhuria ni ule wa marais wa
Afrika utakaojadili jinsi ya Jumuiya ya Kimataifa inavyoweza
kushirikiana kukomesha ujangili na biashara haramu ya pembe za tembo na
faru.
Katika
Mkutano huo utakaofanyika Hoteli ya de la Marine, Rais Kikwete
aanatarajiwa kuwaeleza viongozi wenzake kuhusu hatua ambazo
zinachukuliwa na Serikali yake kukabiliana na ujangili nchini chini ya
Operesheni Tokomeza.
0 comments:
Post a Comment