Hali si shwari katika Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali
Kuu (Tughe), baada ya Baraza lake Kuu la Taifa kuwasimamisha viongozi
wakuu hadi mkutano mkuu wa chama hicho utakapoitishwa.
Viongozi hao wamesimamishwa kutokana na kukacha
mkutano wa Baraza Kuu la Taifa baada ya kuhojiwa kwa tuhuma za
ubadhirifu na kuvunja katiba.
Mwenyekiti wa Kamati Teule, Archie Mntambo alisema
viongozi hao walikimbia baada ya kuhojiwa juu ya uvunjifu wa katiba kwa
kutoitisha vikao vya baraza hilo na ubadhirifu wa fedha za chama hicho.
Akizungumza kabla ya kuahirisha mkutano huo
mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa, Mntambo aliwataja
waliosimamishwa kuwa ni Mwenyekiti wa Taifa, Dk Diwani Mrutu, Makamu
Mwenyekiti, Maclean Chitete na Katibu Mkuu Ally Kiwenge.
Alisema kikao hicho hakina madaraka ya kuwavua
uongozi na kwamba suala hilo litapelekwa kwenye mkutano mkuu wenye
uamuzi wa mwisho kuhusiana na jambo hilo.
“Tangu wachaguliwe Septemba, 2011, hawajawahi
kuitisha kikao cha Baraza Kuu la Taifa ambalo ndilo linalohusika na
upangaji wa bajeti ya chama,” alisema.
Alisema viongozi hao baada ya kusomewa mashtaka
yao waliitwa mmojammoja mbele ya wajumbe wa baraza hilo na kuhojiwa
lakini kabla ya kupewa majibu ya tuhuma zao waliondoka.
Katiba ya chama hicho inautaka uongozi kuitisha vikao vya baraza kuu mara mbili kwa kila mwaka.
Hata hivyo, Chitete alikana kusimamishwa akisema
mkutano huo ambao ulianza Desemba 19 mwaka huu, ulimalizika kwa
mwenyekiti kuufunga... “Mwenyekiti wa Taifa alifunga kikao na mimi
nikaondoka kwenda hotelini kwangu.”
Kwa upande wake, Dk Mrutu alisema jana kuwa kikao
hicho kilichochagua kamati teule hakikuwa halali kwa sababu alifunga
kikao bila uamuzi huo kufikiwa.
Kuhusu tuhuma za ubadhirifu na uvunjaji wa katiba,
alikataa kulizungumzia suala hilo kwa undani na kusema anasubiri barua
ya kumtuhumu kutoka katika kikao halali cha chama.
0 comments:
Post a Comment