Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema amesikitishwa na madai kuwa hakuhusika na ushindi dhidi ya Yanga.
Madai hayo yalitolewa na Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya klabu hiyo, Sued Nkwabi kwamba hakuhusika kufanikisha
ushindi dhidi ya wapinzani wao, Yanga katika mchezo wa Nani Mtani Jembe
ambapo Simba ilishinda 3-1.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rage alisema
anashangaa madai ya namna hiyo yanaelekezwa kwake Simba inapofanya
vibaya licha ya kwamba yeye si kocha, lakini inapofanya vizuri huambiwa
hahusiki.
“Nimewasikia hao wanaosema kwamba mimi sikuhusika na ushindi ilioupata Simba katika pambano dhidi ya Yanga. Huku ni kupotosha.
“Unawezaje kusema mimi sijahusika wakati hata
mchezaji aliyefunga bao la tatu Awadh Juma nilimsajili mimi nyumbani
kwangu? Na siyo bao la tatu tu, hata pasi ya bao la kwanza alilofunga Hamis Tambwe alitoa yeye,” alisema Rage na kuongeza:
“Kila mtu ana uhuru wa kuongea lakini tuwe wa
kweli basi, ukisema Kamati ya Utendaji ya Simba ndiyo imefanikisha
ushindi maana yake na mimi ni sehemu hiyo kamati inaonekana watu wengine
hawaijui hata katiba ya Simba.”
Siku chache baada ya pambano hilo ambalo Simba
iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, Nkwabi alisema Rage hakuchangia kwa
namna yoyote kufanikisha timu yao kuibuka na ushindi.
Rage yuko kwenye mgogoro na Kamati ya Utendaji ya
klabu ya Simba baada ya wajumbe hao kumsimamisha uongozi wakati akiwa
yeye hayupo kikaoni.
0 comments:
Post a Comment