Meneja
wa Vodacom kanda ya Kusini, Henry Tzamburakis akikabidhi msaada wa
chakula kwa kituo cha wa watoto yatima cha EAGT Rahaleo Manispaa ya
Mtwara Mikindani. Wanaopokea msaada huo kutoka (kushoto) ni watoto
wanaoishi katika mazingira magumu Yasunta Rawland, Boniface Seleman,
Mkurugenzi wa kituo cha kulelea watoto cha EAGT Mtwara, Caroline Mkwele,
Askofu wa kanisa la EAGT Rahaleo Mtwara pia (mwasisi wa kituo) George
Mrope. Vodacom kanda ya kusini inatarajia kutumia Tsh.Milioni 3 kusaidia
watu wenye matatizo mbalimbali katika jamii ya kanda ya kusini.
Mkurugenzi
wa kituo cha Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) la
Rahaleo Mtwara, Bi. Caroline Mkwele amesema kituo chake hakina majengo
ya kuwalelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu takribani hamsini
na tatu wanaolelewa na kituo hicho, hatua inayowalazimu watoto kuishi na
walezi wao majumbani nakupelekea ugumu katika kuwalea katika maadili.
Mkurugenzi
huyo ameyasema hayo wakati wafanyakazi wa kampuni ya mawasiliano ya
Vodacom Tanzania walipo watembelea kituoni hapo na kukabidhi msaada wa
chakula, fedha na vitu mbalimbali ambavyo vinatoka katika michango ya
wafanyakazi kupitia mpango wa Pamoja na Vodacom unaolenga kutatua
changamoto za ugumu wa maisha zinazoikabili jamii.
“Changamoto
tulizo nazo ni nyingi lakini zaidi ni hili la kukosa kituo rasmi kwa
maana ya majengo ya kuwahifadhi watoto hawa kwa pamoja, kwa sababu
usipowaweka hawa watoto pamoja uwezekano wa kuwa na tabia tofauti ni
mkubwa. Hivyo kutokana na ukosefu wa kituo inatulazimu kukutana na
watoto hawa kila siku ya Jumamosi. Nawashukuru Vodacom kupitia Taasisi
yao ya Vodacom Foundation kwa msaada huu, pia natoa wito kwa wafadhili
wengine watusaidie watoto hawa, wasilifumbie macho tatizo hili.” Alisema
Bi. Mkwele
Akizungumza
wakati wa kukabidhi msaada huo Meneja wa Vodacom Tanzania kanda ya
kusini Henry Tzamburakis amesema watoto yatima wanahitaji kupata elimu
na mahitaji muhimu kama walivyo watu wengine hivyo kampuni yake
itaendelea kutoa msaada ili kuwapunguzia watoto hao ugumu wa maisha.
“Watoto
hawa naweza kusema kwamba ni watoto wetu, wadogo zetu na ndugu zetu
hivyo yatupasa kuwajali kwa kusikiliza mahitaji yao. Mimi binafsi
ningependa kutoa wito tusingojee mpaka kampuni ijikusanye ndio tuje
kutoa msaada, mtu yeyote anaweza kufanya hivi kwani haihitaji mpaka uwe
tajiri sana, ukiwa na chakula, nguo, chochote kile ambacho unaona
kitawafaa watoto hawa usisite kuwaletea.” Alisema Tzamburakis
Kwa
upande wao watoto wanaolelewa na kituo hicho walibainisha kwamba si
kupenda kwao kuwa yatima hali hiyo inaweza kumkuta yeyote yule ndani ya
jamii, wanawasihi watu wenye uwezo wa aina yeyote kuwasaidia.
“Tunashukuru
kwa msaada huu, kwa kweli utatusaidia siku zote za maisha yetu,
nawaomba msife moyo kutusaidia kwani bado tunahitaji sana na pia
tunathamini kwa kile mnachokifanya.” Alisema Boniface Seleman mmoja wa
watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha EAGT Rahaleo Mtwara
Naye
mtoto wa kituoni hapo, Sofia Said alisisitiza kuwa “tunashukuru kwa
msaada huu, nawasihi na wengine kuiga mfano waliouonesha kampuni ya
Vodacom, zaidi ya hayo ningependa kusema asanteni sana.”
“Napenda
kuwaambia wanajamii wenzetu kama unamuona mtoto yatima na wewe una
uwezo hata kidogo, sio lazima iwe pesa hata chakula unamsaidia tu.”
Alimalizia Yasunta Rawland ambaye pia ni mtoto yatima wa kituoni hapo
Kwa
zaidi ya miaka kumi kampuni ya simu za mkononi Vodacom imekuwa mstari
wa mbele kusaidia makundi ya watu wenye mahitaji maalumu ambapo katika
kipindi hiki watoto zaidi ya 53 wanaolelewa na kituo EAGT Mtwara
wamenufaika na msaada huo.
Ongezeko
la watoto yatima limekuwa ni janga la kitaifa kwa muda mrefu nchini
Tanzania huku serikali, taasisi, mashirika, makampuni binafsi na jamii
kwa ujumla zikifanya jitihada mbalimbali za kupambana na kuondokana na
changamoto hiyo inayotukabili.
Taasisi
ya Vodacom Foundation imekuwa mstari wa mbele kushirkiana na serikali,
mashirika, taasisi na wadau mbali mbali wa sekta za maendeleo nchini
katika kuisaidia jamii ambayo kwa kiasi kikubwa ni wateja wake. Taasisi
hiyo imejidhatiti kufanya kazi na kutoa ushirikiano wa aina yeyote
kuhakikisha gurudumu la maendeleo la watanzania linasonga mbele kwa kasi
inayotakiwa.
0 comments:
Post a Comment