Kibao cha operesheni kata maji kimeligeukia Shirika la Majisafi
na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) baada ya kukatiwa umeme na Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco), ikidaiwa Sh7 bilioni.
Mmoja wa wafanyakazi katika mtambo wa Ruvu Chini,
Mlandizi ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji, alisema
kuwa umeme ulikatwa juzi katika mtambo huo kuanzia saa tatu asubuhi na
ulirejeshwa saa mbili usiku.
Alisema limekuwa jambo la kawaida umeme kukatwa
katika mtambo huo na kurudishwa baada ya mazungumzo baina ya watendaji
wa juu wa Tanesco na Dawasco na mara ya mwisho ilikuwa miezi miwili
iliyopita.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alikiri
Dawasco kudaiwa kiasi cha Sh6.3 bilioni na kwamba Tanesco ilikata umeme
kwa takriban saa saba juzi.
“Lakini waliurudisha jioni baada ya kuzungumza nao na wakatuelewa,” alisema Profesa Maghembe.
Alisema ameiagiza Dawasco kuandaa programu ya namna ya kulipa deni hilo na kulimaliza.
“Tumezungumza nao (Tanesco) na mazungumzo bado
yanaendelea ila nilichowaagiza Dawasco ni kwamba waweke programu ya
namna ya kulilipa deni hilo. Hayo ndiyo maagizo yangu,” alisema Profesa
Maghembe.
Hali hiyo inaaminika kuwa ndiyo imekuwa ikisababisha kukosekana mara kwa mara kwa maji katika Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumzia athari za kukatiwa umeme, mfanyakazi
huyo wa Dawasco Ruvu Chini alisema: “Kuna wakati mwingine shirika
hutangaza upungufu wa maji kwa madai kuwa kuna marekebisho yanafanyika
na kuna wakati huwa haitangazwi kabisa lakini ukweli ni kwamba umeme
hukatwa mara kwa mara na Tanesco.
“Watu wanaweza wakahisi labda maji hayatoki
kutokana na mgawo usioeleweka wa Dawasco au wakati mwingine kudhani kuwa
pengine ni kutokana na matatizo ya miundombinu, lakini ukweli ni kuwa kuna tatizo baina ya Tanesco na Dawasco.”
Kaimu Meneja wa Tanesco, Adrian Severin alisema
walifikia hatua hiyo kutokana na kuidai Dawasco Sh7 bilioni na kwamba
kwa takriban mwaka mzima uliopita, shirika hilo halikulipa gharama
zozote za huduma.
Severin alisema Dawasco hutumia umeme wa wastani wa Sh600
milioni kwa mwezi... “Walituandikia hundi mara mbili lakini tulipokwenda
benki hatukupata fedha, tukaamua tuwasitishie huduma jana (juzi).”
Alisema baada ya hatua hiyo ndipo Dawasco
walipojitokeza kufanya mazungumzo na kutoa kiasi cha Sh600 milioni na
umeme ukarudishwa. Alisema katika siku za usoni wasipolipa
watawasitishia tena huduma hiyo.
Ofisa Uhusiano wa Dawasco, Everlasting Lyaro
alikiri shirika lake kudaiwa lakini akishutumu hatua ya Tanesco
kulikatia huduma hiyo katika mitambo yake kwa madai kuwa inaweza kuleta
athari kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam.
“Sijafahamu deni hilo lina malimbikizo kwa muda
gani lakini pamoja na hivyo bado sheria haziruhusu kukata umeme kwa
sababu Dawasco tunafanya kazi ya kuhudumia jamii,” alisema Lyaro na
kuongeza:
“Tuna mitambo, ambayo ni Ruvu Juu, Ruvu Chini na
Mtoni ambayo inazalisha takriban lita 270 milioni kwa siku, wakikata
umeme itakuwa ni hatari sana,” alisema.
Imeandikwa na Joseph Zablon, Daniel Mjema, Kelvin Matandiko na Ibrahim Yamola.
0 comments:
Post a Comment