Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Ardhi (HakiArdhi), imekosoa hatua ya Naibu Spika, Job Ndugai kuingilia mgogoro wa wakulima na wafugaji wilayani Kiteto na kusema kuwa ni mwendelezo wa uchochezi wa wanasiasa katika migogoro hiyo.
Akiwa kwenye mazishi ya Mchungaji Emanuel Manyaji
(38) na mwanaye Shukuru Manyaji (13) ambao waliuawa na wafugaji kwa
kuchinjwa wakiwa kanisani katika eneo la Hifadhi ya Embroy Murtangos
wilayani Kiteto, Ndugai alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Martha Umbura
kujiuzulu kutokana na madai kuwa hana sifa za kuendelea na wadhifa huo.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari
jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa HakiArdhi, Yefred Myenzi alisema,
kauli hiyo ni mwendelezo wa malumbano ya wanasiasa yanayochochea
migogoro kwa wananchi.
“Nimemsikia naibu spika akisema kuwa viongozi wa
wilaya ndiyo wanahusika, je anao ushahidi? Kwa nini kauli kama hizi
zitoke nje ya Wilaya ya Kiteto? Inaonyesha kuna wanasiasa wanaohamasisha
wananchi wavamie ardhi iliyozuiwa kutumika.”
Kauli ya Ndugai imekuja wakati kukiwa na madai kuwa anamiliki mashamba katika eneo hilo la mgogoro.
Hata hivyo, akizungumza kwa simu,Ndugai alikanusha
kuwa na shamba wilayani humo na kuendelea kusisitiza kuwa, lazima mkuu
wa wilaya awajibike kwa kuwa wananchi wa jimbo la Kongwa wana haki ya
kuishi mahali popote nchini.
“Kwani kuwa na shamba ni kosa?... kwa kifupi mimi
sina shamba Kiteto wala Kongwa kwa sababu mimi silimi. Haya ni mauaji
mabaya mno. Mimi kama naibu spika siyo msemaji sana, hata bungeni
sichangii hoja, ila kwa hili sitaacha kusema,” alisema Ndugai na
kuongeza:
“Mkuu wa Wilaya ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Wilaya, mwananchi aamke salama na afanye kazi, sasa
ikitokea mauaji, mauaji mauaji, unafikiri nini kifanyike? …
“Si Kiteto tu, wananchi wa Kongwa wako Mtwara, Dodoma,Kilimanjaro na popote pale Tanzania wanatafuta maisha,” alisisitiza.
Akifafanua chanzo cha mgogoro wa wakulima na
wafugaji wilayani Kiteto, Myenzi alisema ni hatua ya halmashauri hiyo
kutaka kuwahamisha wakulima katika eneo ambalo wamekuwa wakilitumia kwa
kilimo huku ikidaiwa kuwa eneo hilo ni hifadhi ijulikanayo kama Emboroy
Murtangos.
“Mgogoro huu ulifikishwa katika vyombo vya sheria
ambapo wakulima walishinda… mwaka 2007 katika Mahakama Kuu Kitengo cha
Ardhi. Hata hivyo halmashauri ya wilaya ilikata rufaa Mahakama ya Rufani
na kushinda katika kesi namba 58 ya mwaka 2010. Hata hivyo wakulima
wameomba mapitio ya kesi hiyo,” alisema Myenzi.
Licha ya mgogoro huo, Myenzi alitaja migogoro ya
wakulima na wafugaji wilayani Mvomero na mgogoro wa mwekezaji na
wananchi Mkoa wa Morogoro na mwingine wa mwekezaji na wananchi wilayani
Mbarali Mkoa wa Mbeya.
“Migogoro hiyo inasababishwa na Serikali kushindwa kuchukua
hatua au kuwajibika pale kunapokuwa na fukuto la migogoro licha ya kuwa
na taarifa kwa muda mrefu,”alisema Myenzi.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni Serikali kushindwa
kutoa huduma katika ardhi kama kupima na kumilikisha maeneo hali
inayosababisha wananchi kujichukulia hatua mikononi kwa kuvamia maeneo
na ukiukwaji wa sheria unaofanywa na wananchi kwa kushirikiana na
watendaji wa Serikali.
Kwa upande wake, Chama cha Wananchi(Cuf),
kimeelezea kulaani mauaji hayo yanayoendelea kwenye mji wa Kiteto na
kusema kuna kila sababu ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Martha Umbulla
kujivua wadhifa huo.
“Cuf tunaitaka Serikali isichukulie maisha ya
binadamu kama kitu cha kuchezea…mgogoro huu wa wakulima na wafugaji
umedumu kwa miaka minne sasa bila kuchukuliwa hatua zozote.
“Utararibu wa Serikali wa matumizi ya ardhi bila
ushiriki wa wazi kwa wananchi umekuwa chanzo cha migogoro mingi ya ardhi
nchini Tanzania.”
Cuf ilisema katika taarifa yake kuwa mara kadhaa
Serikali ya CCM imekuwa ikiziangalia chokochoko hizo na kuziacha bila
ufumbuzi wa kudumu, sheria zinavunjwa bila hatua kuchukuliwa na matokeo
yake ni mauaji yanayoendelea Kiteto.
Taarifa hiyo imeongeza mkuu huyo wa wilaya
ameshindwa kubaini dalili na kutatua mgogo huo kwa muda mrefu hadi leo
hii watu wanachinjana na kuchomana moto.Ni vyema akajiuzulu.
0 comments:
Post a Comment