Tuesday, December 11, 2012

ZFA KUWAWEKA KITI MOTO CANNAVARO NA MORRIS;

CHAMA cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kimeamua kuwaweka kiti moto nahodha wa timu ya Zanzibar Heroes, Nadir Haroub Cannavaro na msaidizi wake, Aggrey Morris.
Uamuzi huo wa ZFA umefikiwa leo katika kikao cha dharula cha kamati ya utendaji ya chama hicho kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili kitendo cha manahodha hao kupokonya dola 10,000 za ushindi wa tatu wa michuano ya Kombe la Chalenji na kuzigawa kwa wachezaji.
Cannavaro na Morris wanadaiwa kupora fedha hizo kwa Katibu Mtendaji wa ZFA, Kassim Ali wakati timu hiyo ilipokuwa ikirejea kutoka Kampala, Uganda, ambako ilishiriki michuano ya Kombe la Chalenji na kutwaa nafasi ya tatu.
Mjumbe wa kamati ya utendaji ya ZFA, Mussa Soraga amesema leo kuwa, wachezaji hao wameitwa kesho kwa ajili ya kuhojiwa na kamati ya utendaji  kuhusu kuongoza kitendo hicho.
Tayari ZFA imeshatangaza kuwafungia kwa muda usiojulikana wachezaji wote wa Zanzibar Heroes, wakiwemo walioteuliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kinachojiandaa kumenyana na Ethiopia na Zambia katika mechi za kirafiki za kimataifa.
Kwa mujibu wa Soraga, fedha hizo ni zile zilizotolewa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kutokana na Zanzibar kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Chalenji.
Soraga alisema baada ya Cannavaro kumnyang'anya Kassim fedha hizo, aliamua kuzigawa kwa wachezaji kwa madai kuwa ni mali yao na si ya ZFA.
Mjumbe huyo wa ZFA alisema kutokana na kitendo cha wachezaji kukubali kugawana fedha hizo, chama hicho kimewaona wote kuwa wana hatia ya kushiriki kula njama ya kupora fedha hizo na kugawana.
"Kitendo kilichofanywa na wachezaji wetu ni cha aibu na kimeifedhehesha mno serikali ndio sababu ZFA iliamua kukutana kwa dharula leo na kuamua kuchukua uamuzi huu mzito,"amesema Soraga alipozungumza na liwazozito muda mfupi uliopita.
Kutokana na uamuzi huo, Soraga alisema chama chake kimeamua kuandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulifahamisha kwamba, wachezaji hao, waliopo kwenye timu ya taifa, Taifa Stars na klabu za Yanga, Azam na Simba hawaruhusiwi kuzichezea kwenye michuano yoyote.
Wachezaji waliopo Tanzania Bara waliokumbwa na adhabu hiyo ni Cannavaro wa Yanga, Mwadin Ally, Aggrey Morris, Mcha Khamis na Samir Nuhu wa Azam, Selemani Selembe wa Coastal Union,Masoud Nassoro Cholo wa Simba, Amir Hamad wa JKT Oljoro na Twaha wa Mtibwa Sugar.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa ZFA, Amani Makungu ameamua kulizawadiwa benchi la ufundi la Zanzibar Heroes, dola 10,000 kutokana na timu hiyo kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Chalenji.
Soraga amesema leo kuwa, Makungu alikuwa ameahidi kuwaongezea wachezaji wa Zanzibar Heroes kitita hicho cha fedha kutokana na kushika nafasi hiyo, lakini kutokana na kitendo chao cha kupora fedha kutoka kwa kiongozi wa ZFA, ameamua kufuta ahadi hiyo.
Makungu amekabidhi fedha hizo kwa aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Seif Bausi na msaidizi wake, Kassim Muhidin.
Kikosi cha Zanzibar Heroes kilichokwenda Uganda kushiriki michuano ya Chalenji ni makipa; Mwadini Ali (Azam), Suleiman Hamad (Black Sella), Abdalla Juma (Kipanga).
Mabeki ni Nassor Masoud 'Chollo' (Simba), Samir Haji Nuhu (Azam), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub Ali 'Canavaro' (Yanga), Aziz Said Ali (Kmkm), Mohammed Juma Azan (JKU) na Ali Mohammed Seif (Mtende Rangers).
Viungo ni Hamad Mshamata (Chuoni), Ali Bakar (Mtende Rangers), Is-haka Mohammed (JKU), Twaha Mohammed(Mtibwa Sugar), Suleiman Kassim 'Selembe' (Coastal Union), Saad Ali Makame (Zanzibar All Stars), Makame Gozi (Zimamoto), Issa Othman Ali (Miembeni), Aleyuu Saleh (Black Sella), Khamis Mcha Khamis 'Viali' (Azam).
Washambuliaji ni Amir Hamad (JKT Oljoro), Jaku Juma Jaku (Mafunzo), Abdallah Othman (Jamhuri), Nassor Juma (JKU) na Faki Mwalim (Chipukizi).
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About