Tarehe 3 novemba mwaka huu, siku ya Juma pili saa 8:05 mchana mpaka Jua kuchwa, tutakuwa miongoni mwa wachache watakao bahatika kushudia tukio la angani ambalo limewastaajabisha watu tangu zama za kale. Katika nchi chache za Afrika ya kati, katika eneo mwembamba linaloanzia Bahari ya Pasifiki, kukatisha Gaboni, Zaire, kaskazini ya Uganda, kaskazini ya Kenya karibu na Ziwa la Turkana, Ethiopia na kuishia Somalia, watu wa maeneo hayo watabahatika zaidi kushuhudia Jua likifunikwa kabisa, na kwao mchana utageuka usiku. Kwa upande wetu, nchini Tanzania, tutaona takribani asilimia 70 % ya Jua kufunikwa na kuonyesha Jua likiwa na umbo la hilali kama vile Mwezi mwandamo, linapoangaliwa kwa miwani maaalum ya kuangalizia Jua.
Kupatwa kwa Jua kwa
tarehe 3 novemba ni aina maalumu ya kupatwa huko, kunakojulikana kama kupatwa
mchanganyiko (Hybrid Eclipse) kwa sababu huanza kama kupatwa kwa pete (Annular
Eclipse), ambapo ukingo wa Jua unakuwa haujafunikwa na hivyo kuonekana kama
pete. Baada ya muda pete hiyo nayo inafunikwa na kubadilika kuwa kupatwa
kamili. Kupatwa kwingine kwa mchanganyiko kuma ule wa Novembar 3 kutatokea
tarehe 20 Aprili 2023, katika maeneo ya Asia ya kusini mashariki.
Sisi nchini Tanzania, na takriban bara lote la Afrika
(Angalia mchoro wa Afrika), watu wataona kupatwa kwa Jua kwa sehemu asilimia
mbali mbali kutegemeana na umbali kutoka mkanda wa kupatwa kamilifu. Hili tukio
kubwa kwa vile watu wa bara lote la Afrika watashuhudia tukio hlili kwa pamoja,
muda ule ule. Kwa hiyo wananchi barani kote Africa
wanahamasishwa wangalie tukio hili la maumbili ya kustajabisha na ni maajabu
kwa watoto na vijana kuwachocheza wapende sayansi.
Je kupatwa kunatokeaje? Wakati wa kupatwa kwa Jua, uso wa Jua tunaouona sisi hufunikwaa
na Mwezi. Wakati huo, Mwezi unakuwa kati ya Dunia na na Jua,
kwa hiyo kivuli cha Mwezi huangukia Duniani.
Kutoka angani ungeona kivuli cha Mwezi kinaangukia Dunini (Angalia mchoro
wa jiometri unaononesha mistari ya
mionzi inayosababisha kivuli.)
Wakati wa kupatwa kwa
Mwezi (ambalo lilitokea wiki mbili zilizopita, tarehe 19 Oktoba), pia kuna
kufunikwa kwa Jua. Lakini wakati huo Dunia inakua kati ya Jua na Mwazi.
Hivyo kivuli cha Dunia kinaangukia Mwezini na kusababisha kiza katika
sura ya Mwezi.
Mwezi huzunguka Dunia kila mwezi. Kwa hiyo Mwezi waweza kujipanga mstari mmoja na
Dunia na Jua kwa namna ambayo Mwezi uko kati ya Jua na Dunia, na kusababishwa
kupatwa kwa Jua. Nyakati nyingine Mwezi unaweza kujipanga mstari kwa namna
ambayo Dunia ipo kati ya Jua na Mwezi na kusababisha kupatwa kwa Mwezi.
Kwa vile Mwezi unazunguka Dunia kila mwezi, tungetarajia kutokee
kupatwa kwa Mwezi mara moja kwa mwezi, na kupatwa kwa Jua pia mara moja kwa
mwezi, yaani tungeshuhudia matukio ya kupatwa mara mbili kila mwezi. Lakini tunaelewa kuwa katika mwaka mmoja,
hali ya kupatwa hutokea tatu au nne tu kila mwaka. Kuna tatizo gani?
Dunia inazunguka Jua, na Mwezi unaizunguka Dunia. Na mizunguko hiyo ni ya uso bapa ambayo
imeinamia kiasi kidogo. Hivyo, mstari wa
Jua, Mwezi na Dunia hauwi wa kunyooka, kupatwa hakuwezi kutokea. Kupatwa
kunatokea tu wakati Mwezi unapokuwa pale ambapo mizunguko ya Dunia na Mwezi inakatisha.
Hii hutokea mara tatu au nne tu kila mwaka na matokeo ni kwamba tunapata
matukio mawili hadi manne tu ya kupatwa kila mwaka.
Sababu nyingine ya Jua kuweza kupatwa na Mwezi ni kwamba unapangalia
kutoka Duniani, ukubwa wa Jua na Mwezi zinaukubwa uliolingana kabisa. Ukiangalia
Jua kwa kutumia miwani maalumu ya kujikinga, utatambua kuwa Jua linaonekana
ukubwa sawa kabisa na Mwezi mpevu. Ingawa kipenyo cha Mwezi ni ndogo, (km3,500), na kile cha Jua ni kikubwa kwa
mara mia nne (km. milioni 1.4), vinaonekana ukubwa sawa, kwetu kwa sababu Jua
liko umbali wa mara 400 kutoka kwetu. Kwa hiyo ukubwa wao dhahiri ni sawa kabisa. Jambo hili la ulingano kamili wa Jua na Mwezi
kutoka hapa Duniani kwetu, ni wa
kustaajabisha sana na kinavutia wananchi wote.
Ni rahisi kuonyesha kwa vitendo, kwamba kitu kidogo sana
kinaweza kufunika kuona kwako kitu kikubwa sana. Kata mduara mdogo kwenye
kadibodi na shika mbali kidogo na macho yako. Utaona kwamba mduara mdgogo unaweza
kuficha hata jengo zima au mti wote, jinsi ilivyooneshwa kwenye mchoro.
Pia inavutia kuelewa kwa nini kupatwa kwa Jua hutokea wakati
wa Mwezi mwandamo tu. Wakati huo, Jua linakuwa nyuma ya Mwezi, ambao upande
wake wa giza unatuelekea sisi. Wakati wa kupatwa kwa Jua, upande mweusi wa
Mwezi (upande wenye giza) unakuja mbele ya
Jua na kulificha Jua tusilione. Kwa upande mwingine, kupatwa kwa Mwezi, hutokea
wakati wa Mwezi mpevu kama ilivyotokea wakati wa kupatwa kwa Mwezi kwa giza
jepesi (Penumbral Lunar Eclipse), usiku wa tarehe 19 oktoba 2013. Wakati wa Mwezi
mpevu, uso wa Mwezi unaangazwa na Jua kwa ukamilifu na pia linalotuangaza, Duniani
upande wa mchana. Fikiria Dunia (yaani sisi) kuwa kati ya Jua na Mwezi. Utaona kuwa kivuli cha Dunia kinaweza
kuangukia kwenye Mwezi na kusababisha kupatwa kwa Mwezi. Aina mbili hizo za
kupatwa, mara nyingi, hufuatana moja baada ya nyingine, jinsi ilivyotokea safari
hii. Mwezi ulipatwa tarehe Oktoba 19 na
Jua litapatwa wiki mbili baadaye, yaani
tarehe 3, Novemba.
Tumetaja aina mbalimbali za kupatwa kwa Jua: kupatwa kabisa,
kupatwa sehemu, kupatwa kwa petu na kupatwa mchanganyiko wa Jua. Kupatwa huku,
kunatokea kutegemea na aina ya kivuli cha Mwezi kinachofikia Dunia.
Kama ni kivuli cha giza
zito (lijulikanalo kama umbra), hutokea kupatwa kabisa na mwanga wote wa Jua
huzibwa. Kusema kweli huu ni miongoni
mwa mwonekano wa kustaajabisha katika maumbile kwa sababu mchana ghafla hugeuka
kuwa usiku, angalau kwa mda mfupi. Huu ni wakati pekee ambapo mtu anaweza kuona
anga la juu la Jua, linalojulikana kama Corona, ambalo ni muonekano unaofaa
kuona mwenyewe. Wanasanyansi wengi wanatumia fursa ya kupatwa kabisa kwa Jua, kufanya
utafiti wa Jua na Corona yake na jinis inavyosababisha mabadiliko katika hali
ya hewa ya Dunia.
Kupatwa kwa Pete, hutokea wakati kivuli mchanganyiko cha
Mwezi kinafikia uso wa Dunia. Kinachotokea hasa ni kwamba Mwezi unakuwa mbali
zaidi kutoka Duniani, kwa kipenyo chake dhahiri, ni kidogo kuliko kile cha
kipenyo dhahiri cha Jua kwa hiyo ukingo wa Jua unaachwa wazi na pete ya mwanga
wa Jua inaonekana.
Tarehe 1 Septemba 2016, Tanzania itakuwa kitovu cha tukio
la Dunia wakati kupatwa kwa Jua kwa pete
kutapitia Afrika ya kati na kitovu chake kitakuwa kusini mwa Tanzania. Litakuwa ni tukio kubwa kwa Watanzania wote, na kila mtu nchini tujiandae kuwapokea
watalii Watanzania pamoja na kutoka nchi za nje kuja kushuhudia tukio hili.
Kupatwa tutakaoona siku ya Jumapili Novemba 3, itakuwa ni
kupatwa sehemu tu ya Jua. Sehemu ya Jua itafunikwa na Mwezi. Hakikisha kuwa una miwani maalum ya kuangalizia
kupatwa. Aidha, unaweza kutumia kioo
Namba 14 kinachotumiwa na wanaochomea
chuma. Kwa usalama kamilifu, njia bora
zaidi ni kutoliangalia Jua moja kwa moja kwa muda mrefu. Jua ni
gimba linalotoa mwanga mkali mno kupita kiasi.
TAFADHALI USIANGALIE
JUA MOJA KWA MOJA, AU KWA DARUBINI - UTAPOFUKA PAPO HAPO.
Kuanzia saa 8:05 mchana, kwa kutumia njia salama ya kuangalia
kupatwa kwa Jua, utaona uKingo wa Jua ukianza kufunikwa na Mwezi. Hali hii itadumu pole pole mpaka saa 9:50
alhasiri wakati kiasi kikubwa cha Jua kitafunikwa. Kwa sehemu za kaskazini ya
Tanzania, zaidi ya asilimia 80% ya Jua itafunikwa na mnamo saa 10 jioni wakati
watu wa kusini mwa Tanzania wataona asilimia 60% la Jua litakuwa limefunikwa.
Jijini Dar es salaam, tunatarajia zaidi ya theluthi mbili za Jua litafunikwa mnamo
saa 10 alasiri. Wakati huo, kwa kutumia miwani maalumu, Jua
litaonekana kama vile ni Mwezi mwandamo.
Baada ya kupatwa kwa kiwango cha juu, mnamo saa 10, ukubwa
wa Jua kama Mwezi mwandamo utaongezeka hadi
ukingo wa mwisho wa giza utakapotanzuka saa 11:25 jioni. Mabadiliko ya Jua
yatatokea pole pole kwa kipindi cha zaidi ya saa 3 kwa hiyo hakuna haja ya
kuangalia kupatwa huko mfululizo na waweza kushirikiana kwa urahisi miwani ya
kupatwa kati ya watu wengi.
Licha ya kutumia miwani ya kupatwa na kioo cha giza namba
14, unaweza kuangalia jini kupata kunaendelea kupatwa kwa Jua kwa kutumia njia
ya mwonekano. Utakuwa umegundua kuwa mwanga wa Jua unapo ingia kwenye kitundu
kidogo chochote kwa mfano katika kipande
kikubwa cha kadibodi, utaona mduara wa mwanga ukiangazwa upande wa ndani katika
kivuli cha kadibodi. Mduara huo ni
taswira ya Jua, na njia hii inaitwa njia ya tundu ya kuangalia kupatwa kwa Jua.
Kwa hiyo wakati Jua linapopatwa sehemu tu, utaona umbo kama Mwezi mwandamo
badala ya mduara. Utaweza kufatilia kwa urahisi maendeleo ya kupatwa kwa Jua
kwa kutumia njia ya mwonekano. Hata mwanga unaopenya kwenye minyare ya kati ya
majani ya miti utaonesha Miezi miandamo mingi sakafuni.
Jiandae kwa fursa hii ya kipekee ya kuona tukio la kusisimua
Jumapili hii. Kwa maelezo zaidi na taarifa za hivi karibuni,
tembelea tovuti: http://www.astronomyintanzania.or.tz
HAKIKISHA KWAMBA UNAKINGA MACHO YAKO KWA MIWANI MAALUM UNAPOANGALIA
KUPATWA KWA JUA SIKU YA JUMAPILI 03/09/2013
Na Dkt. N. T. Jiwaji
ntjiwaji@yahoo.com
0 comments:
Post a Comment