Dar es Salaam. Suala la gesi lilizua balaa jana wakati wa
mkutano wa wadau wa sekta hiyo baada ya malumbano makali kati ya Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Mwenyekiti wa
Mfuko wa Sekta Binafsi (TPSF), Dk Reginald Mengi.
Maswi na Mengi walitofautiana juu ya suala la
nafasi ya wawekezaji wazawa kwenye sekta hiyo ya gesi katika kongamano
la pili la wadau wa mafuta na gesi jana jijini Dar es Salaam.
Malumbano hayo yalichochewa zaidi na kauli
iliyotolewa juzi na Waziri wa Nishani na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, ambaye alisema kuwa wazawa wana uwezo mdogo wa kuwekeza katika
sekta hiyo.
Mengi arusha kombora
Mengi ndiye aliyeanza mashambulizi pale alipotaka wazawa wapewe kipaumbele kwenye uvunaji wa mafuta na gesi.
“Tunaambiwa sisi hatuna fedha. Eti hela zetu ni
kwa ajili ya kufanyia biashara ya matunda. Lakini tunayo ardhi, Tanzania
siyo nchi maskini, gesi ni mtaji wetu, tuweke mkakati wa kugawana hii
rasilimali,” alisema Mengi na kuongeza;
“Huku ni kuwa maskini wa fikra na tutakuja
kuulizwa na Mwenyezi Mungu. Kama Serikali haina sera itauzaje rasilimali
zetu kwa wageni? Tusingependa kuyazungumza haya hadharani, lakini
tunasema tu. Mtu mwenye hekima pale wizarani wa kutusikiliza ni Maswi
peke yake.” Mengi alisema anataka kuona Serikali ikitumia mfumo wa taifa
la Nigeria kwa kutoa kipaumbele kwa wazawa.
“Mimi katika masuala ya uwekezaji kwa kweli `role model’ (kivutio) ni nchi ya Nigeria,” alisema Mengi.
Mwakilishi wa taasisi
za dini ashindilia
Baada ya Mengi kukaa, alisimama Mwenyekiti wa
Kamati ya Maadili na Haki za Jamii, Mchungaji William Mwamalanga alisema
Serikali inatakiwa kukubaliana na hoja za Watanzania katika uwekezaji
wa sekta hiyo.
Mchungaji Mwamalanga aliongeza kuwa huu siyo wakati wa kuendelea kuwaachia wawekezaji hatua zote katika rasilimali ya Tanzania.
“Lazima tujifunze kwa mataifa kama Nigeria, serikali yao imetoa
nafasi ya mwananchi kusimamia, yaani mwekezaji akiingia lazima apitie
kwa mwekezaji wa ndani kabla ya kufanya mazungumzo na serikali. Kwa nini
tusifanye hivyo pia? “alihoji Mchungaji Mwamalanga.
Mbali na hilo Mchungaji Mwamalanga alisema Serikali inatakiwa kukiri dhambi ya kuingia mikataba bila kuwapo kwa sera ya gesi.
Maswi ajibu mapigo
Baada ya Mengi na wajumbe wengine kutoa maoni ya
kuilaumu Serikali, Maswi alitakiwa kutoa maelezo ya Serikali kuhusiana
na suala hilo.
Maswi alionyesha wazi alikuwa amepandwa na jazba
kufuatia maoni ya kuiponda Serikali na hakuchelewa kuanza kuwakosoa
Mengi na wadau wengine.
“Katika andiko letu tumeandika, nawahimiza
mkalinunue, tumewagusia wazawa ambao watahusishwa katika ununuzi wa
vitalu. Hakuna aliyesema kuwa sekta binafsi haitashirikishwa,” alisema
Maswi huku akifoka.
Maswi alisema kuna mambo mengi ambayo Watanzania
wanayo fursa ya kushiriki katika uwekezaji wa sekta hiyo na siyo kukaa
majukwaani na kuzungumza kwa unafiki.
Aidha, aliongeza kuwa mpaka sasa hajaona kampuni
yenye uwezo mkubwa hapa nchini katika ushiriki wa moja kwa moja katika
uwekezaji wa sekta hiyo.
“Tusijidanganye kwa vikampuni vidogovidogo
tulivyonavyo, tukadhani kama vinaweza kuingia kwenye ushindani wa moja
kwa moja. Vikampuni vyenyewe vimejaa rushwa tu za kuhonga, hakuna lolote
tuache ubabaishaji, “ alisema Maswi. Aliukosoa pia mtindo wa uwekezaji
wa Nigeria ambao Mengi ameupendekeza:
“Mengi kaka yangu, hakuna suala la mjomba katika
masuala ya uwekezaji. Huo mtindo wa Nigeria siyo mzuri, huwezi kuwapa
watu wachache rasilimali wakati wengi wakiwa kwenye umaskini. Nigeria
imejaa vurugu na hatuwezi kuichukulia kama mfano mzuri,” alisema Maswi
na kuongeza:
“Jukumu letu kama wizara na kila ninapokutana na
ninyi, nakutana kama Katibu Mkuu, siyo Maswi. Lengo letu ni kuwaeleza
kinachoendelea na jinsi ya kuwawezesha wazawa.”
Akijibu hoja ya Mchungaji Mwamalanga, Maswi aliwataka viongozi hao kushirikiana na Serikali badala ya kuinyooshea kidole.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iko tayari
kukutana na kundi lolote. Mkitaka tuonane, leteni barua tu. Tuko tayari
na hatufichi kitu,” alisema na kuongeza: “Tatizo la nchi yetu watu ni
kulalamika tu, fanyeni kazi... Mkitusaidia maaskofu, tutatoka hapa
tulipo, siyo kutunyooshea tu vidole.
Maaskofu wenyewe wanakula rushwa, wanafanya vitu
vya ajabu, mbona sisi hatuwanyooshei? Au tuwataje? Kwa sababu msione tu
Serikali ni watu wabaya, `no, let’s work as a team’,” alisema Maswi.
Aliendelea kusisitiza kuwa fursa ya uwekezaji ipo kwa watu wote bila kujali wa ndani au wa nje.
“Hakuna mtu anayekuja hapa ambaye ni mjomba wenu. Sasa kama nyie mnakaa nyuma nyuma, hebu muwekeze basi.
Hivyo vitalu tumetoa, nani ametaka `document’
tumemkatalia? Watu wanakuja wanaleta hela, sasa tuzikatae?” Kuhusu sera
na sheria ya gesi na mafuta, Maswi alisema sheria ipo ila sera
itakamilika ifikapo Mei mwakani.
“Nawaahidi hadi mwisho wa mwaka huu tutakuwa na
sera ya wazawa, hivyo nawaomba mshiriki kutoa maoni. Kama tunayo sheria
tangu mwaka 1970 na 1980 tunataka nini tena? Tunataka sera au sheria?
Nadhani sheria ni kubwa zaidi, huwezi kwenda kinyume na sheria. Hata
hivyo, sera tunayo tangu Oktoba mwaka huu, lakini bado iko kwenye
mchakato. Itakamilika ifikapo Mei, 2014,” alisema Maswi.
0 comments:
Post a Comment