lami
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,  ameushukuru Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi  (Abu Dhabi Fund for Development) kwa kuonyesha matumaini ya  kugharamia ujenzi wa barabara ya Uvinza-Malagarasi yenye urefu wa kilomita 51 kwa kiwango cha lami, kwa gharama ya shilingi bilioni 31.869.

 Aidha, Rais Kikwete pia ameushukuru Mfuko huo kwa kugharamia ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Uvinza yenye urefu wa kilomita 76.6 kwa kiwango cha lami, ujenzi ambao umekamilika kwa asilimia 100, kwa gharama ya Shilingi bilioni 78.241.
 Mfuko huo tayari umeonyesha matumaini ya kukubali maombi ya Serikali ya fedha za ujenzi wa barabara hiyo  ya Uvinza-Malagarasi yalilowasilishwa mwezi Machi mwaka huu. Kilichobaki sasa ni bodi ya mfuko huo kuidhinisha mpango huo wa maendeleo ya miundombinu katika siku chache zijazo.

 Rais Kikwete ametoa shukurani hizo alipokutana na Mrithi wa Kiti cha Ufalme cha Abu Dhabi ambaye pia ni Naibu Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Mohamed bin Zayed bin Sultan al Nahyan, Jumatatu, Novemba 18, 2013, mjini Abu Dhabi.
Rais Kikwete ameonana na Mrithi huyo wakati aliposimama kwa muda Dubai akitokea Colombo, Sri Lanka, alikohudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).

Rais Kikwete ambaye pia alikutana na kutoa shukurani zake kwa   Mkurugenzi Mkuu wa Abu Dhabi Fund for Development Bw. Mohamed Saif Al Suwaidi, ameelezea furaha yake kwa kuwapo na matumaini ya kupatikana kwa fedha hizo, amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi za juhudi za Serikali za kuunganisha kwa lami mkoa wa Kigoma na Dar es salaam ndani ya miaka miwili ama mitatu ijayo.
 Hivi sasa tayari Serikali ya Korea inagharamia ujenzi wa Barabara ya Kigoma-Kidahwe yenye urefu wa kilomita 48.

 Rais Kikwete amesema: “Nafarijika sana kwa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kuonyesha matumaini ya kugharamia ujenzi wa barabara ya Uvinza-Malagalasi. Mfuko umekubali ombi letu la fedha kilichobaki ni Bodi yake kuuridhia katika siku chache zijazo.”
 “Ujenzi wa barabara hiyo ya Uvinza-Malagarasi ukikamilika pamoja na ule wa ujenzi wa barabara ya Tabora-Urambo, Tabora-Nyahuwa, pamoja na ujenzi wa barabara ya Manyoni-Chanya unaogharamiwa na serikali ya Korea Kusini, kilomita zipatazo 200, zitakuwa zimejengwa na usafiri kutoka Kigoma hadi Dar es salaam utakuwa katika barabara ya lami.

 Rais Kikwete, ambaye yuko njiani kuelekea Warsaw, Poland, kuhudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya hali ya hewa duniani, alipata nafasi pia kushuhudia maonyesho ya  mwaka huu ya Dubai Airshow 2013 katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Al Maktoum eneo la Dubai World Central.
 Maonyesho hayo, ambayo ni ya tatu kwa ukubwa duniani, yanashirikisha zaidi ya makampuni 1000 kutoka sehemu mbalimbali yakihusisha kila aina ya ndege za kivita, za abiria, za mizigo na  za michezo.