Wednesday, November 20, 2013

JK AWASASILI POLAND KUHUDHURIA MKUTANO WA TABIA YA NCHI

pol3
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili jijini Warsaw, Poland, kuhudhuria mkutano wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Nchi zilizosaini protokali ya  Kyoto kuhusu mabadiliko ya Tabia Nchi ulioanza jana Jumanne Novemba 19, 2013. PICHA NA IKULU.
pol1
Rais Kikwete akisalimiana na mmoja wa wajumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Warsaw, Poland, asubuhi ya, Jumanne, Novemba 19, 2013, kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi ambako analiwakilisha Bara la Afrika.
Rais Kikwete amewasili Poland akitokea Dubai, alikosimama kwa muda akiwa njiani akitokea Colombo, Sri Lanka, ambako aliungana na viongozi wengine wa Jumuiya ya Madola kushiriki Mkutano wa Viongozi wa Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo uliomalizika mwishoni mwa wiki.

Kwenye Mkutano huo wa Mabadiliko ya Tabia Nchi unaojulikana kama Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Tabia Nchi -Conference of Parties on the Convention na Mkutano wa Tisa wa Nchi Wanachama wa Itifaki ya Kyoto – Meeting of the Parties of the Kyoto Protocal – COP 19/CMP -9, Rais Kikwete anawasilisha Bara la Afrika.
Rais Kikwete ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Marais wa Afrika kuhusu Tabia Nchi (CAHOSCC) ambayo ndiyo inatoa msimamo na mwelekeo wa kisiasa wa Bara la Afrika kuhusu masuala ya Tabia Nchi.
Rais Kikwete alichaguliwa na wenzake kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo wakati wa Mkutano wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia, mwanzoni mwa mwaka huu.
Rais Kikwete alichukua nafasi ya Hayati Meles Zenawi wa Ethiopia ambaye alifariki dunia Septemba mwaka jana, 2012.

Mkutano huo wa COP19/CMP-9 unafunguliwa mchana wa leo kwenye Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Warsaw na Rais Kikwete ni mmoja wa viongozi wanaozungumza kwenye ufunguzi huo.
Wengine ambao wanazungumza kwenye ufunguzi huo ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon, Waziri Mkuu wa Poland Mheshimiwa Donald Tusk na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu, Mheshimiwa Balozi William Ashe.

Kwenye Hoteli ya Bristol mjini Warsaw, Rais Kikwete amepokelewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Mheshimiwa Theresia Huvisa ambaye amekuwa anaongoza ujumbe wa awali wa Tanzania katika vikao vya maandalizi ya COP-19-CMP 20.
Mara baada ya kuwasili hotelini, Rais Kikwete amepewa maelekezo kuhusu Mkutano huo na Waziri Huvisa na baadaye kupewa maelezo na ujumbe wa AU ukiongozwa na Mheshimiwa Rhoda Tumusiime, Kamishna wa AU na Bwana Emmanuel Dlamini, Mwenyekiti wa Wataalam wa Majadiliano wa Kundi la Afrika.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About