kova1
Kamanda wa Kanda Maalum Dsm, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) Suleiman Kova.
.Mtuhumiwa huyo ni  wa kumi kukamatwa kuhusiana na tukio hilo
Siku moja baada ya nguli ya sheria za katiba nchini, Dakta Sengodo Mvungi kuaga dunia nchini Afrika Kusini, Jeshi la Polis Kanda Maalum Ds, linamshikilia mtuhumiwa mmoja John Ikondia Mayunga (56) kwa kosa la kushiriki kikamilifu kwenye mauaji ya mwanasheria huyo na mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

 Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda Maalum Dsm, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) Suleiman Kova amesema mtuhumiwa huyo ni mkazi wa kiwalani walipata taarifa kwa raia wema kwamba alishiriki kikamilifu kwenye tukio hilo lilosababisha kifo cha Dakta Sengodo Elibariki Mvungi.
“mnamo tarehe 12/11/2013 Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia mwema kwamba kuna mtu ambaye amehusika na tukio la mauaji ya Dakta Mvungi na kwamba kipindi hicho mnamo saa 12 jioni mtuhumiwa alikuwa maeneo ya mtaa wa Twiga Jangwani akiwa anaangalia Televisheni,” amesema Kamishina Kova.
1454628_650916231627891_1324435004_n
Marehemu Dakta. Sengodo Mvungi.

Kova amesema kwamba mtuhumiwa alitambuliwa na kukamatwa kisha kuhojiwa na Polisi na alikubali kwamba alihusika na akwaongoza Askari hadi nyumbani kwake Kiwalani Migombani.


Alifafanua kwamba taratibu za upekuzi zilifanyika na katika upekuzi vilipatikana silaha ambayo ni Bastola aina ya REVOLVER N0. BDN 6111 pamoja na risasi ishirini na moja.

Kova amesema kuwa mtuhumiwa alikiri kwamba katika vitu vitu vilivyoibwa nyumbani kwa Dakta Mvungi ni pamoja na bastola hiyo aidha siku ya tukio hilo walitumia milipuko kutishia ili kufanikisha uporaji huo.

Kamanda Kova alisisitiza kwamba mtuhumiwa huyo ni wa kumi kukamatwa kuhusiana na tukio hilo na bado operesheni kali inaendelea ili kuhakikisha kuwa yeyote aliyehusika na tukio hilo anakamatwa kwa nguvu za dola.