Thursday, November 28, 2013

USULTANI WAZIDI KUVITAFUNA VYAMA VYA SIASA NCHINI

http://azizicompdoc.blogspot.com/
Hali ya kisiasa katika kambi ya upinzani nchini, imekuwa ya kupanda na kushuka. Hii inatokana na migogoro inayoonekana kuvikumba vyama vya upinzani hasa katika nyakati za kushika kasi kuelekea kwenye mafanikio ya kweli.
Migogoro hii mingi  huhitimishwa kwa kufukuzana na kusimamishana uanachama na mara nyingine kupelekana mahakamani.
Vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na TLP vina historia hiyo. Matukio hayo yamevifanya vyama hivyo kuporomoka umaarufu wake, heshima iliyojijengea katika jamii na hata nguvu.
NCCR-Mageuzi walipokuwa katika mgogoro walihitimisha kwa kumfukuza na kumvua uanachama Mbunge wa Uvinza, David Kafulila na mgogoro ndani ya CUF uliishia kumvua uanachama mbunge wake wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid Mohamed. Wote hawa mashauri yao yapo mahakamani.
Sasa ni zamu ya Chadema ambacho kimetangaza kuwavua vyeo waliokuwa viongozi wake wa ngazi za juu, Zitto Kabwe, ambaye amevuliwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu na ile ya Naibu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pamoja na Dk. Kitila Mkumbo ambaye amevuliwa nafasi ya Ujumbe wa kamati kuu.
Matukio hayo ya kufukuzana uanachama kwa vyama hivyo vikubwa vya siasa, ndiyo yanayosababisha kuwepo kwa maswali yanayokosa majibu kuhusu nafasi ya kambi ya upinzani nchini.
Maswali yanayokosa majibu ni endapo uamuzi huu mgumu wa Chadema utasababisha kukijenga chama hicho au utakifanya chama hicho kikuu cha upinzania nchini kufuata nyayo za CUF, NCCR-Mageuzi na TLP na swali la pili ni iwapo hali hiyo ni kiashiria cha upinzani kukua au kudidimia. Wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa pamoja na wanasiasa wanajibu swali hili kama ifuatavyo.
Profesa Gaudence Mpangala
Msomi na mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Profesa Gaudence Mpangala anasema uamuzi unaofanywa na vyama wa kuwafukuza au kuwasimamisha viongozi wake unaweza kuwa halali kulingana na sababu zilizosababisha kufikia uamuzi huo.
“Inaweza kuwa ni hatua halali kama waliosimamishwa kweli walifanya mambo yanayohatarisha uhai wa chama,” anasema Profesa Mpangala.
Anasema chama kama Chadema ni kikubwa kinachoweza kushinda uchaguzi mkuu ujao, hivyo kinapaswa kuwa na viongozi walioshikamana na kuwa na nia moja. Endapo kuna viongozi wanaoonekana kwenda kinyume, chama kina haki ya kufanya uamuzi wa namna yoyote wenye lengo la kukinusuru.
“Chadema ni chama kikubwa kinachoweza kushika dola…kinahitaji mshikamano mkubwa kwa viongozi wake na kuhakikisha hawatokei wasaliti….kama ni kweli waliosimamishwa ni wasaliti ni halali kabisa,” anasema Profesa Mpangala.
Anaendelea “Nidhamu kwa wanachama na nidhamu kwa viongozi ni kitu muhimu sana…kama viongozi hawana nidhamu ni rahisi sana chama kusambaratika,” anasema.
Anaongeza kueleza kuwa ni lazima Chadema kiwe imara ili kiweze kushika dola na hiyo itawezekana endapo viongozi watakuwa na msimamo mmoja wa kukijenga chama na siyo kukisaliti.
Kuhusu endapo uamuzi huo unaweza kukidhoofisha chama, Profesa Mpangala anasema, “Kama hizo tuhuma siyo za kweli kinaweza kudhoofika (Chadema) maana viongozi hao wanao ushawishi mkubwa kwa watu wanaokiunga mkono chama hicho, hivyo lolote linawezekana,” anasema. Masuala ya usaliti ndani ya vyama vya siasa yapo duniani kote na kwamba haishangazi kama hilo limetokea Chadema au ndani ya chama chochote kingine.
Dk  Charles Kitima
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT) Dk  Charles Kitima, anasema bado kunaonekana kuwa na pengo la demokrasia ndani ya vyama vya siasa nchini.
Anaendelea kuna pengo la uelewa wa demokrasia ndani ya vyama vya siasa nchini, vyama vitambue kuwa demokrasia ni  kusahihishana na kujisahihisha.
Dk Kitima alisema kuwa na mitazamo tofauti siyo usaliti ni demokrasia na kusema ni vyema busara zitumike katika kutofautisha kati ya usaliti na mawazo tofauti ya wanachama na viongozi pamoja na misimamo ya vyama.
Anasema hata hivyo endapo mtu au kiongozi anafanya kitendo cha usaliti kinachoonekana pia ni kuvunja Katiba ya nchi huyo moja kwa moja anakuwa mkosaji na ni sahihi kukabiliana naye.
“Wote wanaotuhumiwa na waliovuliwa vyeo ni wasomi wazuri na sidhani kama nia yao ni kuhujumu… pengine wanayo nia ya kujenga na viongozi wenzao wanapaswa wawe tayari kupokea mabadiliko…wapokee mawazo ya kujengwa yanayoletwa ndani ya vyama vyao hata kama ni mawazo yanayotumiwa na wapinzani wao,” alisema.
“Katika harakati za kujenga unaweza kukosea au ukapatia...na kuwa na mtazamo tofauti siyo usaliti, nadhani demokrasia iheshimiwe, hujuma zibainishwe na mahakama ndiyo iwe na mamlaka ya kutamka hizi ni hujuma na huu ni usaliti na siyo mambo haya kutazamwa juu juu” alisema Dk Kitima.
Hamad Rashid
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohammed, anasema matukio ya kufukuzana na kutuhumiana baina ya viongozi yanayofanywa na watendaji wakuu wa vyama yatasababisha upinzani kudumaa.
Hamad anasema vyama vya siasa vimekuwa na usultani wa kuonekana kuwa vinapaswa kuongozwa na baadhi ya watu huku wanachama wengine wenye uwezo na mawazo mapya na yasiyopendwa na wakubwa wakitafutiwa mbinu ya kuondolewa.
“Hili linalotokea Chadema sasa ni matokeo ya mfumo mbovu wa uongozi ndani ya vyama vya siasa nchini….vingi haviongozwi kama taasisi, tunahitaji vyama kukaa na kujengwa kama taasisi, viwe na mfumo wa mabadiliko ya uongozi utakaosaidia vyama kukua” alisema
Alisema hali hii ikiachwa vyama vya upinzani vitaendelea kudumaa na kubakia historia kwani wafuasi wao walio wengi ambao ni vijana watavikimbia kutokana na kuona hawana nafasi ya kuleta mabadiliko ndani ya vyama vya upinzani.
“Vijana wanakosa matumaini ya kushika madaraka katika ngazi za juu ndani ya vyama vya upinzani…hawaoni matumaini ya fursa ya kuongoza vyama hivi kutokana na mfumo wa uongozi uliopo…viongozi waliopo wanaonekana hawataki challenge, hawataki watu wenye uwezo nje ya wao.
Anasema ili demokrasia ikue viongozi wanapaswa wakubali mawazo ya wengine na mtu mwenye mawazo tofauti asionekane kuwa msaliti au mkosaji anayepaswa kuwekwa pembeni.
Hamad Rashid anaongeza kuwa hata wafuasi wa vyama vya upinzani ambao wengi wao ni vijana wameanza kuvikimbia vyama vya upinzani na kurejea CCM baada ya kukosa imani na vyama vya upinzani ambavyo vinaonekana kutokukubaliana na mawazo mapya ya vijana.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About