Waziri
wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (mbele) akikagua moja na
makalvati makubwa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua
maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Nzega hadi Puge mkoani
Tabora.
Injinia
Haile Tadase (aliyenyoosha mkono) kutoka Kampuni ya SMEC inayosimamia
ujenzi wa mradi wa barabara ya Nzega – Puge akimpa maelezo Waziri wa
Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (mwenye suti) wakati alipofanya
ziara ya kushtukiza kukagua maendeleo ya mradu huo.
Waziri
wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na wananchi wa mji wa
Nzega waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wakati alipofanya ziara ya
kushtukiza kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Nzega
hadi Puge mkoani Tabora.
Wananchi
wakimsalimia Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (mwenye
suti) mara baada ya kumaliza kuwa hutubia katika mkutano uliofanyikia
viwanja vya stendi mjini Nzega.
Mkandarasi
anayejenga barabara inayotokea Nzega hadi Puge mkoani Tabora amejikuta
matatani baada ya Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
kufanya ziara ya kushtukiza kukagua maendeleo ya Mradi huo.
Mradi
huo ambao ni sehemu ya barabara inayounganisha miji ya Tabora na Nzega,
unajengwa na Mkandarasi China Communications Construction Company Ltd
(CCCC) kutoka Jamhuri ya Watu wa China. Kimkataba mkandarasi huyo
alipaswa kuwa amekamilisha kazi hiyo mwezi Mei mwaka huu wa 2013 lakini
hadi Waziri Magufuli anatembelea mradi huo kulikuwa na asilimia 30 tu ya
kazi zilizokamilika.
Kwa
mujibu wa Meneja wa Barabara mkoa wa Tabora Injia Damian Ndabalinze,
mradi huo ulisainiwa mwezi Julai 2010 ukiwa umepangwa kukamilika katika
kipindi cha miezi 27.
Naye
Meneja wa Kampuni ya CCCC inayojenga barabara hiyo Injinia Zhou Ming
Tao, akijitetea kuhusu kuchelewa kukamilika kwa mradi huo alizitaja
baadhi ya sababu zinazo sababisha mradi huo kusuasua kuwa ni tatizo la
upatikanaji wa maji kwa ajili ya kazi za ujenzi pamoja na kusubiri kwa
muda mrefu malipo kwa madai yao waliyowasilisha Tanroads.
Wakati
akihutubia wananchi katika viwanja vya stendi mjini Nzega, Mheshimiwa
Magufuli alizikataa hoja hizo na kumtaka mkandarasi huyo kuhakikisha
kuwa anakamilisha kilomita zote 59 za mradi huo kwa kiwango cha lami
ndani ya kipindi cha miezi 7 ijayo. “Nimefanya ziara ya kushtukiza na
nimeona mkandarasi amekwishajenga makalvati na madaraja madogo 65 kati
ya 68 hivyo kazi iliyobaki inaweza kukamilika ndani ya miezi saba endapo
mkandarasi ataongeza kasi ya kazi na sitakuwa tayari kupokea visingizio
vyovyote ambavyo vitasababisha ongezeko jingine la muda” alisisitiza
Waziri Magufuli huku akimtahadharisha Msimamizi wa mradi huo kuhakikisha
kuwa viwango vya ubora vinazingatiwa.
“Visingizio
vya kutokuwepo kwa maji havikubaliki kwani mkandarasi alipata fursa ya
kukagua mazingira ya mradi huo kabla ya kuwasilisha zabuni yake”
alifafanua Waziri Magufuli na kuongeza kuwa hata hayo madai
anayozungumzia mkandarasi ni visingizio visivyokubalika kwani kampuni
yoyote inapoomba mradi mkubwa kama huo hutakiwa kuwa na mtaji wa
kutosha.
Aidha,
wakati akijibu maswali mbali mbali kutoka kwa wananchi, Mheshimiwa
Magufuli aliwahakikishia wananchi hao kuwa ingawa barabara hiyo itapita
nje kidogo mwa mji wa Nzega, pia kutakuwepo na barabara ya kiwango cha
lami itakayounganisha barabara hiyo mpya na mji wa Nzega kwa kuifuata
barabara inayotumika kwa sasa.
Wakiongea
katika nyakati tofauti, Mheshimiwa Patrick Mbozu ambaye ni Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya pamoja na Bw. Abrahman Mndemi ambaye ni
Mkurugenzi wa Hamashauri ya mji wa Nzega walielezea kuwa, kasi iliyoanza
kuonekana katika siku za karibuni inatoa imani kuwa Mkandarasi huyo
ataweza kuikamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi hicho cha miezi saba
kilichoelekezwa na Waziri wa Ujenzi.
Ujenzi
wa barabara ya Nzega hadi Tabora umegawanywa katika sehemu mbili.
Sehemu ya kwanza inaanzia Nzega hadi Puge na sehemu ya pili inatokea
Puge kuelekea Tabora zote kwa pamoja zikiwa na urefu wa kilometa 114.5
Mheshimiwa
Magufuli aliifanya ziara hiyo ya ghafla akitokea mikoa ya Mwanza na
Geita alikokuwa akikagua shughuli mbali mbali za maendeleo.
0 comments:
Post a Comment