Sunday, November 17, 2013

SERIKALI YA TANZANIA YACHARUKA KUHUSU KUCHUKUA HISA ZA KILA MGODI TANZANIA

IMG_2438
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kwamba kuanzia sasa hakuna mgodi utakaoanzishwa bila ya serikali kuwa na hisa.
Kauli hiyo imetolewa leo na  Profesa Muhongo wakati wa  utiaji  saini hivi karibuni katika makubaliano ya kukabidhi mgodi wa dhahabu wa Tulawaka kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kutoka kwa Kampuni ya Uchimbaji wa Madini  ya Afrikan Barrick  Gold (ABG) katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo jijini Dares Salaam.
Utiaji saini huo ulifanywa na Mkurugenzi Mkuu wa  STAMICO, Gray  Mwakalukwa  na Makamu wa Rais wa  ABG, Deo  Mwanyika.

 “STAMICO   itachimba katika mgodi huo kwa niaba ya Watanzania, hivyo serikali  itaiwezesha kiutendaji, kifedha,kiutalaamu  na kuwa na rasimali watu, amesema Profesa Muhongo.
 Aliongeza kuwa baadaye   shirika hilo  litauza hisa  kwa Watanzania.   
Amesema STAMICO imenunua mgodi huo kwa dola za Marekani milioni 4.5, ambapo kati ya fedha dola milioni 3.5 zimeshalipwa moja kwa moja.
Akizungumzia kuhusu uuzaji wa mgodi huo, Mwanyika  amesema  kulingana na sera zao uchimbaji huo hautakuwa na faida  kwao , hivyo eneo hilo  linafaa kuendelezwa na  wachimbaji wa kati.

 Amesema STAMICO itachukua mdogi huo na baaadhi ya leseni za utafutaji wa madini zinazozunguka eneo hilo kwa gharama hiyo na kukubali kutoa asilimia 2 ya mrabaha iwapo uzalishaji utazidi wakia 500,000 zikiwa na kikomo cha dola za Marekani 500,000.
 Mwanyika alifafanua kwamba STAMICO itachukua umiliki na usimamizi wa mfuko wa fedha za ukarabati wa mazingira ikiwa kama sehemu ya mpango wa ufungaji wa mgodi huo na itakuwa na dhamana ya majukumu yaliyopita na ya baadae yanayohusiana na kufunga mgodi na ukarabati wa mazingira.

 Aidha itawajibika kulipa fidia kwa wahusika wengine wa mkataba huo iwapo majukumu yao yalioainishwa hayakutekelezwa na ABG itailipa STAMICO salio lililobakia kwenye mfuko wa kukarabati mazingira ambayo kwa sasa ni dola za Marekani milioni 17.6,ambapo bei pia ya mauzo kwenye makubaliano itapunguzwa kutoka kwenye salio.
Katika hatua nyingine Profesa Muhongo amesema  watu wenye maeneo makubwa ya  vitalu  vya madini  ambayo hawajayafanyia kazi  yatachukuliwa kulingana na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na watapewa wachimbaji wadogo.

Amesema STAMICO itakuwa inawasimamia wachimbaji wadogo, itawasaidia kupata mikopo kiurahisi kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), kutoa elimu ya uchimbaji na kuhifadhi mazingira kupitia vyama vyao.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About