Monday, December 9, 2013

MAMA SALMA AWATAKA VIONGOZI WA WA EAC NA SADC KUHAKIKISHA ELIMU YA UZAZI INATOLEWA KWA VIJANA

IMG_0129
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akihutubia mkutano wa Mawaziri kutoka nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kuhusu elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wa nchi hizo. Mkutano huo wa siku mbili unafanyika nchini Afrika Kusini katika Mji wa Cape Town.
IMG_0112
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipiga picha na Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Bwana Michel Sidibe wakionyesha umuhimu wa dhana nzima ya mkutano wa High Level Group ( YOUNG PEOPLE TODAY, TIME TO ACT NOW) kuhusiana na masuala ya elimu ya afya ya uzazi kwa vjijana katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Na Anna Nkinda- Cape Town ,  Afrika ya Kusini
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka viongozi wa Serikali, Taasisi za kijamii, washirika wa maendeleo na wahisani kutoka nchi za ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kusini kushirikiana  na kuandaa programu za pamoja ambazo zitaongeza elimu ya afya ya  ujinsia na huduma za afya ya uzazi kwa vijana  kwani wao ni  nguvu kazi ya maendeleo ya taifa.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)ameutoa wito huo leo wakati akifunga mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika  katika Hoteli ya The Westin iliyopo mjini Cape Town  nchini Afrika ya Kusini.
Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwapongeza wajumbe wa kamati hiyo kwa kushiriki mijadala kwa umakini na kuchangia katika maazimio ambayo yataweza kuongoza juhudi za kuandaa mazingira salama na wezeshi kwa makuzi ya vijana katika nchi wanazotoka.

Mama Kikwete alisema, “Leo tumeshuhudia dhamira yetu katika kuimarisha elimu ya ujinsia na afya ya uzazi kwa vijana katika eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika. Maazimio tuliyoyatayarisha na kuyakabidhi kwa mawaziri wetu yamezingatia mahitaji ya elimu na huduma ya afya ya uzazi kwa vijana katika eneo letu, hali kadhalika mila na desturi katika jamii zetu.
Maazimio haya yanahimiza elimu na huduma jumuishi ya afya ya uzazi na ujinsia ili kuwezesha afua za mabadiliko  ya tabia inayochagiza desturi za kuacha kufanya tendo la ndoa  hadi wakati muafaka, kupunguza idadi ya wapenzi na kuishi maisha ya uadilifu kwa wale wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Mama Kikwete ambaye naye ni mjumbe wa kamati hiyo ambaye aliteuliwa kama mke wa Rais anayejitoa kufanya kazi ya kuisaidia jamii yake wakiwemo kina mama na watoto wa kike  alisema kupitia maazimio hayo wamedhamiria  kuandaa msingi wa elimu bora ya afya ya uzazi kwa kuandaa mitaala na kutoa mafunzo katika kipindi kifupi hadi kufikia mwaka 2015 .

Katika mpango wa muda mrefu pamoja na mambo mengine wamedhamiria  kuongeza matumizi ya huduma ya afya ya uzazi, kutokomeza maambukizi mapya ya VVU  kwa vijana na kuzuia ndoa za utotoni  ifikapo mwaka 2020.
Kwa upande wake waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi alisema katika  mkutano huo mambo mengi  yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na  kuongeza jitihada za ziada katika kupambana na tatizo la   maambukizi mapya ya ugonjwa wa  Ukimwi kwa vijana na watoto pia waliangalia   njia mbalimbali moja wapo ikiwa ni kutoa elimu kwa vijana hasa waliopo mashuleni .

“Wizara za Afya na Elimu  zimekutanishwa kwa pamoja kwa madhumuni ya kuja na mikakati mipya ambayo itapelekea kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa vijana kupitia mitaala ya kufundishia mashuleni pia watoto  wote na kina mama wajawazito ambao wanamaambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi wapewe dawa bila tatizo lolote”, alisema Dk. Mwinyi.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dk. Fatma Mrisho alisema ingawa katika Dunia vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi vimepungua kwa asilimia 30 kwa watu wazima lakini kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 vifo vimeongezeka kwa asilimia 50.

Hivyo basi wao wanachukua takwimu hizo kama changamoto na wameshalipa suala hilo kipaombele na kuongeza chachu zaidi ya utendaji wa kazi, wataendelea kufanya kazi na vijana na  kuwasikiliza  matatizo yao ili mahitaji yao yaweze kufanyiwa kazi.
Aidha Afisa anayeshughulikia Elimu ya Afya na Ukimwi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania Mathias Herman alisema ili kutekeleza maazimio hayo ushirikiano wa pamoja  kati ya Serikali na wadau wa Elimu na Afya unatakiwa kwa upande wao  watahakikisha kuwa vijana wanapata elimu ya ujinsia na uzazi ambayo itawasaidia kujitambua na hivyo kujiepusha na Ukimwi na mimba za utotoni.

Katika mkutano huo kulikuwa na mijadala mbalimbali ambayo iliibua mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kutekeleza maazimio ambayo wajumbe walijiwekea baadhi ya mijadala hiyo ni umuhimu wa kuandaa bajeti pamoja na mikakati ya kupata fedha na mpango wa utekelezaji wa mikakati, kutayarisha mipango inayozingatia umri wa watoto, mila na desturi wakati wa kupeleka elimu ya afya ya uzazi katika mazingira ya shule.
Kupungua kwa rasilimali na msukumo kwenye miradi ya kuzuia maambukizi ya VVU, hivyo kusababisha kupungua kwa upatikanaji na matumizi ya kondomu katika baadhi ya jamii, matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa janga kubwa ilinalosababisha madhara kwa vijana na umuhimu wa kuandaa mikakati inayozingatia mahitaji ya vijana wenye ulemavu.

Mawaziri wa Afya na Elimu kutoka nchi 21 za EAC NA SADC walikubali mbele ya kamati hiyo kuwa wataenda kuyafanyia kazi maazimio hayo ambayo yatawasaidia  vijana kupata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia jambo ambalo litawasaidia  kufahamu zaidi  ugonjwa Ukimwi.
Mkutano huo wa siku mbili uliandaliwa  na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) , UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About