Wakati watu saba wakiwa bado hawajaonekana baada ya boti ya Kilimanjaro II, kupatwa na dhoruba na abiria kuzama baharini, nahodha wa chombo hicho alitoa taarifa za uongo kuhusu ajali hiyo imefahamika.
Akizungumza nasi Mkurugenzi wa Mamlaka
ya Usafiri Baharini (ZMA), Mhandisi Abdi Omar Maalim, alisema taarifa
iliyotolewa na nahodha katika kituo cha mawasiliano zilikuwa za uongo na
hivyo kusababisha kazi ya uokozi kuchelewa.

“Nahodha alitoa taarifa za uongo na kusababisha
zoezi la uokoaji kutokufanyika kwa wakati mwafaka, baada ya kutokea
ajali hiyo,” alisema Mhandisi Maalim.
Alisema ajali hiyo ilitokea saa 3:30 asubuhi
lakini kazi ya uokoaji ilianza alasiri baada ya kupokea taarifa kutoka
kwa abiria kuwa wenzao wamezama baharini baada ya meli kupigwa na wimbi.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Rashid Seif
Suleiman amesema nahodha wa chombo hicho alianza kuhojiwa na polisi
juzi. Alisema kazi kubwa inayofanyika sasa ni kutafuta watu ambao bado
hawajaonekana na baada ya kukamilika ataamua kama kuna haja ya kuunda
tume ya kuchunguza ajali hiyo.
Alisema baada ya uhakiki wa majina ya abiria
waliosafiri na boti hiyo wamegundua kuwa jumla ya watu 15 walizama
baharini baada ya boti kupigwa na wimbi na kusababisha injini kuzimika.
Waziri Seif alisema hadi jana maiti tano zimepatikana na watu watatu wameokolewa.
Msimamizi Mwandamizi wa chumba cha kuhifadhia
maiti katika Hospitali ya Mnazimmoja, Vuai Jabir Hassan aliwataja
marehemu kuwa ni Rashid Said Ali (11) mkazi wa Ilala Dar es Salaam,
Akram Khamis Issa (11) wa Mwanakwerekwe, Masoud Hamad (30) wa Wete
Pemba, Nushra Khamis (9) na Fatma Asir Khamis (18) wa Magogoni Wilaya ya
Magharibi Unguja.
Aliwataja waliookolewa kuwa ni Ali Maulid Haji (Mwanakwerekwe), Ali Salum Ali (Pemba) na Mahir Ali Issa (Mwanakwerekwe).
Wakati huohuo, huduma za usafiri kati ya Unguja na
Pemba zimesitishwa kwa muda kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa
katka Bahari ya Hindi. Habari zilisema hatua hiyo ni ya kiusalama.
0 comments:
Post a Comment