Tuesday, January 7, 2014

SERIKALI YAAHIDI KUTEKELEZA AHADI ZA DR MGIMWA JIMBONI KWAKE

http://azizicompdoc.blogspot.com/

Wakati Rais Jakaya Kikwete jana akiongoza mamia ya wakazi wa Mkoa wa Iringa na mikoa ya jirani kwenye mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameahidi kuwa Serikali itatekeleza ahadi alizotoa jimboni kwake.
Dk Mgimwa, ambaye alikuwa Mbunge wa Kalenga, alizikwa jana saa 10 jioni katika kijiji cha Magunga kilichoko Kata ya Maboga mkoani Iringa.
Dk Mgimwa aliyefariki Januari mosi mwaka huu nchini Afrika Kusini, kutokana na tatizo la figo, alizikwa katika shamba la makaburi lililopo karibu na nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji hicho.
Akitoa ujumbe wa Serikali katika mazishi hayo, Pinda alisema wataziangalia ahadi alizotoa marehemu na kuzifanyia kazi zile ambazo hazijakamilika.
“Katika kumuenzi marehemu Mgimwa, sisi Serikali tunamuenzi kwa kutekeleza mema yote aliyotuachia,” aliongeza Pinda.
Pinda alisema Serikali imepoteza waziri aliyetegemewa katia wizara husika na taifa kwa jumla.
“Zimetolewa sifa nyingi zikimwelezea Waziri Mgimwa juu ya uaminifu wake. Mimi nimesimama hapa kuthibitisha hilo, kwa muda mfupi alioteuliwa amefanya kazi kwa uadilifu na weledi mkubwa na sisi katika Serikali tukasema sasa wizara imempata waziri anayestahili,” alisema Pinda.
“Kati ya Oktoba 4-15 sisi serikalini tulimtuma Mgimwa aende Marekani akafanye kazi moja na ndipo ilipogundulika kuwa alikuwa na tatizo lakini yeye alivumilia hadi kazi ilipoishi ndipo akarudi na alipofika akasema ngoja aende Afrika Kusini akaangalie afya yake,” alisema Pinda.
Kwa upande wake, mtoto wa marehemu Godfrey Mgimwa ambaye alisimama kutoa shukrani kwa Serikali na wananchi waliofurika katika mazishi hayo, aliiomba Serikali kutekeleza ahadi kadhaa alizoziacha baba yake kama njia pekee ya kuwafariji wanafamilia na wananchi wa Jimbo la Kalenga.
“Siku 10 kabla ya kufariki dunia, baba aliniambia kuwa wakazi wa Jimbo la Kalenga ninawapenda sana katika kipindi hiki ambacho hali yangu si ya kuridhisha ningependa niwapelekee mabati 1,200. Ametutoka bila ya kutekeleza ahadi hiyo, watoto na wanafamilia tunaomba Serikali kutekeleza ahadi hizo kama njia pekee ya kutufariji,” alisema Godfrey.
Godfrey alitaja miradi minne ambayo baba yake alimweleza kuwa alikuwa anataka kuwatekelezea wakazi wa jimbo hilo kuwa ni pamoja na umeme, minara ya simu, uanzishaji wa ushirika wa kuweka na kukopa na barabara.
Akitoa mahubiri yake katika ibada ya misa ya mazishi ya marehemu Mgimwa, Msaidizi wa Makamu wa Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Iringa, Padri Julius Kingalawe, alisema taifa limefikia hatua mbaya ya watu kutokuaminiana.
“Watu hawaaminiani, mtu akimwona mwenzake anakuwa na hofu ya kama atamfanya nini kwani watu wamefikia hatua hata ya kufanyiana mambo mabaya ili wapate nafasi ama fedha. Siku hizi hata katika vikao muhimu kumekuwa na malumbano,” alisema Kingalawe.
Akizungumza kwa niaba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mchungaji Peter Msigwa alisema kifo cha Mgimwa ni pengo kwa Serikali, jimbo lake na hata upinzani kwa kuwa alikuwa kiongozi wa tofauti na wengine .“Sisi tunasema Mgimwa alikuwa kiongozi mwadilifu, msikivu tena mchapakazi, upinzani tunasema ni pigo sababu yeye amekuwa tofauti na viongozi wenzake wa kisiasa bungeni ambao wanapotekeleza majukumu yao ya kisiasa wanaegemea katika itikadi za chama chao,” alisema Msigwa ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema).
Ibada hiyo ya mazishi iliyoanza saa nne kamili, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi akiwamo Makamu Mwenyekiti, Phillip Mangula na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
Pia baadhi ya mawaziri na manaibu mawaziri na hata Chifu wa Wahehe, Mtwa Mfwimi wa pili, Abdul Adamu Sapi, ambaye alisifia utendaji wake wa kazi.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About