Mjumbe huyo ambaye ni Waziri wa Makazi na
Maendeleo wa Miji na Vijiji nchini China, Jiang Weixin aliwasili
Zanzibar ili kumwakilisha Rais Xi Jinping katika Maadhimisho ya Miaka 50
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ikulu
ya Zanzibar, inaeleza kuwa Dk Shein alimweleza mgeni huyo kuwa katika
miaka 50 ya Mapinduzi China imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na watu
wa Zanzibar katika harakati zao za kujiletea maendeleo.
Alitolea mfano ushirikiano wa Zanzibar na China
mara baada ya Mapinduzi ambapo nchi hiyo ilisaidia katika uanzishwaji wa
viwanda mbalimbali, misaada katika kuendeleza kilimo cha kisasa,
michezo, sekta ya habari pamoja na uimarishaji wa sekta ya afya ambayo
ilikuwa nyuma sana humu nchini.
Aliongeza kuwa kwa Zanzibar kuzungumzia maendeleo
ya sekta ya afya haiwezekani bila ya kutambua mchango mkubwa Serikali ya
watu wa China na wataalamu kutoka nchi hiyo ambao walianza kufanya kazi
nchini mara tu baada ya Mapinduzi.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na
Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Dk Shein alisema kitendo
cha Rais Xi Jinping kumtuma Mjumbe wake Maalum kushiriki maadhimisho
hayo ni uthibitisho wa urafiki wa kweli uliodumu kwa miongo mingi kati
ya Serikali na wananchi wa nchi mbili hizo.
Alimweleza Mjumbe huyo kuwa wananchi wa Zanzibar
wamefarijika sana kupokea salamu za kuwatakia heri katika maadhimisho ya
miaka 50 ya Mapinduzi..
Alisisitiza kuwa kitendo cha Jamhuri ya Watu wa
China kuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza kuyatambua Mapinduzi ya
Zanzibar kitabaki katika kumbukumbu za historia ya ukombozi wa watu wa
Zanzibar.
Alieleza kuwa kitendo hicho hakiwezi kusahaulika
kwa kuwa miaka 50 iliyopita wananchi wa Zanzibar walipokataa kutawaliwa
na kuamua kujitawala wenyewe walihitaji kuungwa mkono na wanachi wenzao
kote ulimwenguni na ndipo China bila ya ajizi ikayatambua Mapinduzi mara
moja.
Dk. Shein alimueleza Mjumbe huyo Maalum wa Rais Xi
Jinping kuwa ushirikiano kati ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla na
Serikali na wananchi wa China umekuwa ukiimarika.
Kwa upande wake, Bwana Jiang alieleza kuwa ni
heshima kubwa kwake kuwasilisha Salamu za Pongezi na za Kirafiki kutoka
kwa Rais Xi Jinping na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China kwa Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na wananchi wa Zanzibar
wakati huu wa kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi.
0 comments:
Post a Comment