Unapozungumzia uchumi na uwekezaji katika Tanzania huwezi kuiweka kando Bakhresa Group of Companies, kampuni inayomilikiwa na mfanyabiashara mzalendo Said Salim Bhakresa.
Siyo uchumi na uwekezaji pekee, bali kampuni hiyo
pia ni soko la ajira kwa Watanzania wenye utaalamu katika fani
mbalimbali, hata wale wasio wataalamu ambao hufanya kazi kwa muda na
kupata ujira wao unaowawezesha kuendesha maisha ya kila siku.
Kimuundo Azam Bakhresa Group Companies inajumuisha
kampuni mbalimbali ambazo kibiashara zinatumia jina la Azam. Kampuni
hizo zote zipo chini ya mwavuli mmoja ambao msingi wake ni uwekezaji
katika sekta ya chakula na vinjwaji, vifungashio, Usafirishaji abiria
majini, usafirishaji na majengo.
Baadhi ya kampuni hizo ni Azam Bevarages, Azam
Marines, Azam Tv, Azam Football na SSB Flour, inayojihusisha na
utayarishaji, usambazaji na uuzaji wa unga wa ngano na mahindi ndani na
nje ya Tanzania.
Katika mahojiano maalumu na Blog hii, Meneja
masoko wa SSB Flour, Omar Kuwe pamoja na mambo mengine anaeleza kuhusu
utendaji, mikakati, ubora wa unga wa kampuni hiyo na changamoto
wanazokumbana nazo sanjari na mchango wake katika kukuza uchumi wa
taifa.
Anasema kuwa kuundwa kwa Azam Bakhresa Group
Companies, kumetokana na ubunifu wa mwenyekiti mtendaji wa kampuni hizo,
Saidi Salim Bakhresa anayemwelezea kuwa mjasiriamali anayependa
kujifunza.
Kuwe anaeleza kuwa yeye ni mmoja wa watendaji
wazalendo katika kampuni hizo akisimamia masoko ya unga wa ngano wa Azam
akisema kuwa kazi yake kubwa ni kuhakikisha bidhaa hiyo inawafikia
walaji ikiwa katika hali ya ubora wa hali ya juu. Anabainisha kuwa unga
wa ngano na sembe za Azam ni bidhaa zinazozalishwa kwa kuzingatia na
kufuata taratibu na kanuni za kiafya kimataifa.
“Tunazalisha bidhaa kwa kufuata viwango
vilivyowekwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Taifa la
Viwango (TBS), pamoja na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) kwa kuwa
bidhaa hizo pia husafirishwa nje ya nchi. Mfano sembe yetu tunauza hata
Uingereza ingawa siyo wakati wote,” anasema Kuwe.
Anafafanua kuwa asilimia 85 ya bidhaa inayozalisha
kampuni yake ni unga wa ngano kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo na
asilimia iliyobaki (15) huzalisha Sembe.
“Tunazalisha unga wa ngano bora, hata sembe bora
inayokubalika na kupata soko hata nje ya nchi, tumewekeza katika
kuhakikisha Watanzania wanatumia unga halishi, pia tunalenga kuzalisha
unga wenye virutubisho na thamani zaidi kwa mlaji, vilivyo salama bila
kuwa na madhara kwa watumiaji,”anasema Kuwe akiongeza: “Watanzania na
watumiaji unga wa ngano wetu wakumbuke, Azam ndiyo nyumbani.”
Anaweka wazi kwamba uwezo na aina ya mitambo
inayotumika kuzalisha bidhaa hiyo ni vya hali ya juu vikiwa vya kisasa,
vyenye ubora wa kimataifa.
Anabainisha kuwa kutokana na mahitaji makubwa na
uzalishaji mdogo nchini, kampuni yake hulazimika pia kuagiza ngano
kutoka nje ya nchi ili kukidhi haja ya soko, mbali na ile inayonunuliwa
hapa nchini katika baadhi ya mikoa ikiwamo Arusha na Manyara.
Anataja baadhi ya nchi ambazo SSB Flour huagiza ngano kuwa ni
pamoja na Canada, Australia, Urusi na Afghanistan akibainisha hatua
mbalimbali inazopitia kabla ya kusagwa unga.
“Ngano ikishafika bandarini na kupakuliwa hupitia
hatua mbalimbali, hatua hizo hufanyika pia kwa mahindi. Yote huchekechwa
kutoa uchafu, kisha sumaku kubwa hutumika kubaini na kutoa vitu kama
sindano au waya kabla ya kusafishwa na kupepetwa tena,” anasema Kuwe na
kuongeza:
“Ikiwa safi, husagwa na kutengenezwa kulingana na
mahitaji na ubora, hata muda wa matumizi pia hutegemea ubora na aina ya
unga. Mfano unga wa sembe huweza kudumu na ubora wake hadi miezi sita
tangu ilipotengenezwa, dona hukaa hadi miezi mitatu.”
Meneja masoko huyo anaeleza kuwa Azam pia
inazalisha ngano yake katika nchi za Malawi, Msumbiji, Uganda na Rwanda
kupitia viwanda vyake vilivyojengwa katika nchi hizo za Afrika.
Akizungumzia mchango wa kampuni yake kwa pato la
taifa Kuwe anasema: “Mchango wetu ni mkubwa kwa pato la taifa bila shaka
wanapotajwa walipa kodi wakubwa kampuni yetu Azama haikosi, hilo
linadhihirisha tunavyochangia pato la taifa.”
Anaongeza: “Lakini pia tunatoa ajira katika
taaluma mbalimbali hasa kwa vijana hivyo kuchangia taifa kupunguza
tatizo la ajira na kupitia hao pia pato la taifa linaongezeka kwani nao
ni walipa kodi. Kwa wastani wafanyakazi wote wa Azam wanafikia 6,000.”
Kuhusu changamoto Kuwe anasema kwamba katika
biashara ni lazima kuwepo changamoto kwani bila hivyo biashara inaweza
kuanguka. Anataja changamoto wanazokumbana nazo ni upande wa masoko na
mazingira ya biashara akisema tatizo analoliona ni kutokuwepo kwa sera
halisi hasa ya uzalishaji wa unga wa mahindi.
“Hata hivyo tunafanya kazi karibu na Serikali,”
alisema Kuwe akifafanua kwamba pamoja na changamoto hizo kampuni hiyo
imeweza kufikisha bidhaa zake na huduma maeneo mbalimbali ya nchi hata
vijijini, huku unga wake wa ngano, mahindi na bidhaa nyingine
zikikubalika kutokana na ubora wake.
Kwa mujibu wa maelezo binafsi ya kampuni hiyo,
Bakhresa Group ni moja ya kampuni zinazoongoza Tanzania na Afrika
Mashariki, ikiwa na historia ya kipekee kwa mmiliki wake kuanzia na
biashara ya mgahawa mdogo Jijini Dar es Salaam katika miaka ya sabini,
ambapo iliendelea kukua na kuongezeka hata kupata umaarufu kama familia
ya kibiashara katika ukanda huo.
Shughuli za kampuni hiyo kwa sasa zimeenea nchini
Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi hata Zambia. Pia inafanya
shughuli zake katika nchi za Malawi na Msumbiji huku ikiwa na malengo ya
kupanua zaidi wigo wa biashara zake katika nchi nyingine.
Maelezo hayo yanaonyesha kuwa kiuchumi Azam
Bakhresa Group inajivunia mapato yanayofikia Dola 600 milioni za
Marekani kila mwaka, ambazo ni sawa na takriban Sh960 bilioni, huku pia
ikijivunia kutoa ajira kwa watu wa kada mbalimbali wanaofikia 500,000.
Katika salamu zake kwa mwaka uliopita wa 2013,
Mwenyekiti wa Azam Group Companies, Said Salim Bakhresa aliuelezea mwaka
2012 kuwa mwaka wenye Baraka kwa kampuni yake hata kuibuka na kuwa
mmoja wa washindi wa tuzo za ubunifu wa kibiashara maarufu ya ‘G20
Challenge on Inclusive Business Innovation,’ iliyotangazwa na wanachama
wa kundi hilo Juni mwaka 2012.
Alisema kuwa katika mwaka 2012, kampuni hiyo iliweka rekodi mpya
ya kusambaza tani 750 za ngano kwa siku jijini Dar es Salaam, na tani
250 kwa siku za unga huo katika mji wa Nacala,nchini Msumbiji.
Bakhresa alisema kuwa wana mpango wa kuanzisha
miradi katika nchi ya Burundi pia kupanua shughuli zake zaidi nje ya
Ukanda wa Afrika Mashariki.
0 comments:
Post a Comment