Thursday, February 20, 2014

CHADEMA YATENGUA MAAMUZI YA WAPIGA KURA ZA MAONI JIMBO LA KALENGA

http://azizicompdoc.blogspot.com/
Moja ya sifa za mwanasiasa ni kuwa mvumilivu na kukubaliana na mabadiliko hata kama yatachelewesha kasi ya kutimiza ndoto yake.
Wiki iliyopita Kamati Kuu ya Chadema ilimtangaza Grace Tendega kuwa ndiye atakayepeperusha bendera ya chama hicho kuchuana na wagombea wa vyama vingine kuwania ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa.
Uchaguzi huo mdogo utakafanyika Machi 16, 2014 kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu, Dk William Mgimwa aliyefariki dunia Januari 1, 2014 katika Hospitali ya Mediclinic Kloff, Afrika Kusini alikokuwa akipata matibabu.
Uteuzi wa Tendega umetangazwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema kuwa kwa mujibu wa taratibu ndani ya chama hicho, jina la mgombea hupitishwa na Kamati Kuu baada ya kujiridhisha kuwa ametimiza vigezo vinavyotakiwa.
Kauli hiyo ‘ilitengua’ matokeo ya kura za maoni zilizopigwa na wanachama wa Chadema wa jimbo hilo, na kumpa ushindi Lucas Mwenda kwa kura 132 huku Tegenda akiibuka wa pili akiwa na kura 122.
Mbowe anasema kuwa matokeo ya kura za maoni yaliyotangazwa awali hayakuwa na ‘baraka’ za Kamati Kuu, hivyo hayakuwa rasmi, hivyo akawataka wapigakura wampokee mgombea aliyepitishwa na chama.
Mbowe anaongeza kuwa: “Bwana Sinkala (Mwenda) bado ni kijana mdogo, mwanasheria wetu na tunahitaji kumkuza zaidi, basi vyombo vyote vimeshauri nafasi hii apewe mama Tendega kwa sababu ana sifa za kutosha.”

Baadaye azizicompdoc.blogspot.com ilipata nafasi ya kuzungumza na Mwenda, ambaye pia alihudhuria mkutano wa Mbowe na wanahabari jijini Dar es Salaam, na wakati wote alionekana kuwa kimya huku akimsikiliza kwa makini mwenyekiti wake.
Nilitaka kujua anajisikiaje baada ya Kamati Kuu kumtangaza mgombea aliyekuwa ameshika nafasi ya pili, jambo ambalo lina historia ya kuleta msuguano katika historia ya siasa za Tanzania.
Mwenda anasema: “Kama panya ameingia kwenye kihenge (hifadhi ya chakula), hatuwezi kujali rangi ya paka kuondoa wale panya. Sio lazima mimi niwe mbunge, akichaguliwa mtu yeyote mwenye kutaka kuleta mabadiliko nitamkubali.
Anaongeza: “Kuteuliwa kwa mgombea mwingine kutawashtua sana wapiga kura, lakini tutajitahidi kuwaambia Wanakalenga kuwa shida yao siyo aina ya mtu bali ni mabadiliko.”

Mwenda anasema kuwa alifahamiana na Tendega wakati walipokuwa wote kwenye Chama cha Jahazi Asilia, ambapo alimsaidia kuwania Jimbo la Kalenga mwaka 2005 na kufanikiwa kuibuka namba mbili.
“Mabadiliko haya nimeyapokea kwa moyo mzuri kwa sababu dada Grace ninamfahamu tumeanza kupambana naye tangu Jahazi Asilia, nilimsapoti sana, akapotea kidogo mimi nikaendeleza mapambano, amekuja tena Kamati Kuu imetumia vigezo vyake kumchagua,” anasema. Anasema wananchi wa Kalenga wanahitaji mbunge atakayewaletea maendeleo kwa sababu jimbo hilo linaongoza kwa umaskini mkoani Iringa.
“Wananchi wa Kalenga hawasomewi mapato na matumizi, hawajui hata kama fedha za ruzuku zimekuja kwenye vijiji vyao,” anasema.
Anasema kuwa tatizo kubwa lililopo Kalenga ni mfumo mbovu wa kupeleka maendeleo kwa wananchi ambao unasimamiwa na CCM, hatua iliyolifanya jimbo hilo kuongoza kwa umaskini katika Mkoa wa Iringa.
“Kama tunahitaji mabadiliko hatuhitaji rangi ya mtu, jinsi au kabila lake, tunachohitaji ni kuona maendeleo yanapatikana baada ya kukosekana kwa miaka 52,” anasema Mwenda.
Ujasiri wa kupokea uamuzi wa Kamati Kuu ya chama aliouonyesha Mwenda huenda ukasaidia kupingana na maneno aliyowahi kusema mpigapicha maarufu wa Marekani, Mark Cohen, kwamba: “Hakuna kinachoweza kumkwaza mpigakura zaidi ya kumbadilishia mshindi wake.”

Tendega, mwajiriwa wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) tangu mwaka 2006 na msomi mwenye Shahada ya Uzamili katika sanaa ya saikolojia ya jamii, anasema anaamini uteuzi wake utapokewa kwa shangwe na wakazi wa Kalenga kwa kuwa wanaifahamu historia yake ya utendaji kazi.
Tendega anasema chama chake kimethibitisha kukomaa kidemokrasi kwa kufanya mambo yake kwa uwazi, ndiyo maana wagombea wenzake wote 14 wameunga mkono uteuzi huo.
“Mgombea mwenzangu ameupokea uteuzi wangu kwa moyo mweupe na ndiyo maana yupo hapa, kwa hiyo hakuna namna yoyote wagombea kugawanyika katika hili,” alisema Tendega.  Tendega ambaye amewahi kuwa mjumbe wa nyumba kumi wa CCM katika Mtaa wa Kichangani, Kihesa, Iringa Mjini kati ya mwaka 1996 hadi 1998, amewahi pia kufanya kazi katika Wizara ya Kilimo na Chakula.
Akizungumza kwa simu kutoka Iringa kwa masharti ya kutokutajwa jina ktk Blog kwa kuwa siyo msemaji wa Chadema, mmoja wa viongozi wa chama hicho jimboni humo, anasema kuwa uamuzi uliofikiwa na Kamati Kuu utaungwa mkono na wanachama wengi kwa kuwa Tendega ana nguvu ya ushawishi ndani na nje ya chama.
“Hawa watu walitofautiana kura kumi tu, uamuzi utakuwa uliochukuliwa utakuwa ni sahihi kwa sababu kwenye kura ya maoni tuliangalia tu idadi ya kura, wakati wao wanataka sifa za ziada,” anasema.

Tayari Chama cha Wananchi (CUF) kimeshatangaza kutomsimamisha mgombea katika uchaguzi huo, huku CCM kikimnadi Godfrey Mgimwa, mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo.
Quantity : Add to Cart

No comments:

Post a Comment

Labels

Blogroll

Labels

About