Mkurugenzi wa zamani wa Fedha wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Elisa Issangya amejikuta akitupiwa vyombo vyake nje na Kampuni ya Udalali ya Mwafrika kwa kile kilichoelezwa kutakiwa kuondoka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi.
Nyumba hiyo iliyoko Mtaa wa Ruhinde Block 2 Plot
294 eneo la Ada Estate wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam,
inaelezwa kuwa inamilikiwa na BoT.
Akizungumza nyumbani kwake baada ya kutupiwa nje
vifaa vyake, Issangya alisema: “Nimeshtukizwa na maofisa wa Kampuni ya
Udalali ya Mwafrika kuingia ndani kwangu na kuniomba nishirikiane nao
kutoa vitu vyangu nje.
“Maofisa hao wa Kampuni ya Mwafrika walifika
nyumbani kwangu asubuhi na kunionyesha barua kutoka BoT ya kunitaka
kuvitoa vyombo vyangu nje, sikukubaliana nao, nikaamua kwenda polisi
kutoa taarifa,” alisema.
Alisema wakiwa polisi na ofisa mmoja wa kampuni
hiyo aliyemtaja kwa jina moja la Gama ambaye alikuwa akimweleza kuwa,
watamuelewesha suala hilo baada ya kuondoa vyombo hivyo , lakini
waliporejea nyumbani kwake, walikuta vyombo vyote vimetupwa nje.
Issangya alisema kitendo cha kutupiwa vifaa nje ni
udhalilishaji kwani walitakiwa kwenda nyumbani kwake wakiwa na barua ya
mahakama ya kuwaruhusu kufanya hivyo.
“Nimeshangaa hatua hiyo wakati mpaka sasa kesi
yangu ya kudai haki zangu ipo mahakamani, wangesubiri mpaka hukumu
ikitolewa ndipo waje na uamuzi huu,” alilalamika Issangya aliyeteuliwa
kushika nafasi ya Mkurugenzi wa Fedha wa BoT mwaka 2000 kabla ya
kusimamishwa 2008.
Alipoulzwa sababu za kufanya hivyo wakati suala la
mlalamikaji bado liko katika vyombo vya sheria na uamuzi wa shauri
haujafikiwa, Ofisa wa Kampuni hiyo ya Udalali, Joseph Gama alisema kuwa
wanatekeleza maagizo ya tajiri wao na si vinginevyo.
“Sisi tunafanya kazi kwa amri ya tajiri wetu,
hatuwezi kufanya mambo kinyume na maelekezo, tumeelekezwa na huu ni
utekelezaji wake,” alisema.
0 comments:
Post a Comment