Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ameingilia kati vita ya kuwania urais mwaka 2015 kwa kukemea kwa baadhi ya makada wa chama hicho kuanza kampeni mapema.
Kadhalika, ameziagiza Kamati za Maadili na Usalama
za chama hicho kuwachukulia hatua stahiki viongozi na wanachama wake
wanaomwaga fedha ili kupata uongozi.
Rais Kikwete alizungumzia masuala hayo kwa nyakati
mbili tofauti; juzi wakati alipokutana na Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa
Mbeya na jana kwenye kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 37 ya
kuzaliwa chama hicho.
Kauli yake imekuja wakati kukiwa na vita ya maneno
baina ya makada wa chama hicho, kutokana na kauli iliyotolewa na Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye alitangaza kuanza rasmi kwa
safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo amesema itatimiza
ndoto za Watanzania kupata elimu bure, majisafi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya mwaka
mpya aliyowaandalia marafiki na jamaa zake, Januari Mosi, mwaka huu
huko Monduli mkoani Arusha.
Tamko hilo lilileta hisia kuwa ametangaza nia ya
kugombea urais mwaka 2015 kupitia CCM na kusababisha malumbano baina ya
wazee, vijana, viongozi na makada wa chama hicho wakimtuhumu kuwa
anakivuruga chama kwa kutangaza nia hiyo kabla ya muda wa kampeni
kuanza.
Akizungumza wajumbe wa Halmashauri ya CCM ya Mkoa
wa Mbeya kwenye Ukumbi wa CCM, Mbeya, Rais Kikwete alisema kuanza kwa
kampeni kabla ya wakati wake ni moja ya mambo yanayosikitisha.
“Hili ni moja ya mambo yanayosikitisha. Lakini
suala zima tumelikabidhi kwa Mzee Mangula (Phillip - Makamu Mwenyekiti
wa CCM Bara), ambaye atalisimamia na kulishughulikia,” alisema.
Rais Kikwete alikuwa akijibu swali na Mwenyekiti
wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi ambaye alimtaka kufafanua kama
kampeni zimeanza ndani ya CCM au bado.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja
wa Sokoine, Mbeya jana, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM,
alisema kutoa fedha kunaharibu taswira ya chama hicho na kukiweka katika
hatari ya kupoteza ushindi katika chaguzi zinazokuja.
“Agizo la CCM la miaka mingi iliyopita ni kwamba
kila ngazi kuwa na shughuli za kuwaingizia mapato sambamba na kuwa na
mfuko wa uchaguzi. Agizo hili bado halijatekelezwa na ndiyo linakiathiri
chama,” alisema Rais Kikwete.
Alisema hali hiyo imekiathiri CCM: “Hivi sasa viongozi
wanachukua fedha chafu kutoka kwa watu wenye sifa mbaya na nia chafu.
Hata wanaotoa rushwa hupokewa kishujaa.”
Alisisitiza wanaotoa fedha chafu kwa ajili ya
kuimarisha chama lazima wahojiwe akisema wema huo wameutoa wapi ilhali
walikuwapo siku zote. Alisema taswira ya chama hicho ikiwa nzuri,
kitaungwa mkono na ikiwa mbaya kitachukiwa na watu.
Aliwataka viongozi na wanachama wa CCM kulipa
uzito unaostahili suala la uadilifu na kwamba bila kufanya hivyo chama
kinaweza kuwa imara na kutekeleza majukumu yake lakini kisiungwe mkono
na wananchi.
“Tusipoungwa mkono na wananchi tunaweza kupoteza
ushindi. Ndiyo maana chama kikaunda Kamati ya Usalama na Maadili kufanya
kazi ya kuwabana watu wanaokiuka maadili, naomba kamati hizo zifanye
kazi yake ipasavyo,” alisema.
Alisema kamati hizo zisipokuwa makini zitaathiri hadhi na kukubalika kwa CCM katika jamii.
“Vitendo hivi vibaya lazima tuvikatae na tuvipige
vita kwa nguvu zetu zote. Tusiwaache watu wachache wanaotaka uongozi wa
gharama yoyote waharibu sifa nzuri ya CCM.”
Alisema watu hao wakiachwa itajengeka dhana potofu kwamba uongozi ndani ya CCM ni wa kununua.
Akizungumzia mvutano unaohusishwa na mbio za
urais, Mangula alisema jana kuwa Kamati ya Maadili ya CCM itawahoji
wanachama wake kadhaa wakiwamo, Lowassa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa
Shinyanga, Hamis Mgeja kwa kutoa matamko ambayo yanaonekana kukiuka
kanuni na maadili ya chama hicho.
Mangula ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, alisema si hao wawili pekee watakaoitwa kwenye kamati yake, bali wapo wengi.
Alisema kazi hiyo itafanyika kabla ya kikao kijacho cha Kamati Kuu ambacho hata hivyo, hakusema kitakutana lini.
Malumbano kuhusu ‘safari’ ya Lowassa yalianza kwa baadhi ya
wenyeviti wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Geita, Joseph
Kasheku `Msukuma’ kukana kauli ya Mwenyekiti wa CCM wa Singida, Mgana
Msindai kuwa wenyeviti wote wa CCM wa mikoa walikuwa wanamuunga mkono
Lowassa. Hata hivyo, Msindai alikanusha suala hilo.
Makamu Mwenyekiti wa zamani wa CCM, John Malecela
na Mkuu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM, Paul
Makonda pia walimtuhumu Lowassa kwamba anakivuruga chama hicho kwa
kuanza kampeni mapema za urais.
Hata hivyo, kauli zao zilipingwa vikali na makada
wengine wa chama hicho akiwamo Mgeja, Mwenyekiti wa zamani wa CCM wa Dar
es Salaam, John Guninita na viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM wa
Morogoro.
0 comments:
Post a Comment