Rais Jakaya Kikwete (wa pili kushoto), akizungumza na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa baada ya kuhutubia mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa Dar es Salaam jana. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad na
Rais Jakaya Kikwete ametangaza kuwa Bunge Maalumu la Katiba litaanza Februari 18 mwaka huu huku akiwataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuweka mbele masilahi ya Taifa na siyo ya vyama vyao.
Rais Kikwete alisema wajumbe 640 wa Bunge hilo
wengi ni wafuasi wa vyama vya siasa, hivyo wanatakiwa kukubaliana kwa
hoja badala ya kila upande kuvutia kwake.
Aliwaonya pia wanasiasa kutokazania suala la
muundo wa Muungano peke yake, bali waangalie na masuala mengine yaliyomo
kwenye rasimu hiyo ambayo ni muhimu kwa Taifa.
Bunge la Katiba linafanyika baada ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kukamilisha kazi yake ya miezi 20 kukusanya maoni
ya wananchi na kuandaa Rasimu ya pili Katiba ambayo ilitolewa Desemba
30, mwaka jana.
Akizungumza na viongozi mbalimbali wa vyama hivyo
jana katika mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Rais Kikwete
alisema kama wanasiasa wakikubaliana, hakuna mwananchi yeyote
atakayepinga uamuzi utakaopitishwa na Bunge hilo.
“Nimeshauriana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohammed Shein kuwa Bunge Maalumu la Katiba lianze vikao Februari 18,
mwaka huu. Bunge hili litafanyika kwa siku 70 na kama mambo yatakuwa
hayajamalizika zinaweza kuongezwa siku 20,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: “Nyinyi ndiyo wenye jukumu la kuipatia
nchi yetu katiba nzuri inayojali masilahi ya watu wake ndani ya pande
zote za Muungano, kuanzia watu wanapoishi, wanapotoka na asili yao.
Msije mkafanya uamuzi utakaowaingiza katika uadui na chuki.”
Katika hotuba yake ya dakika 70, Rais Kikwete
alisema yapo mambo mengi ya kujadili katika Bunge hilo, siyo muundo wa
Muungano pekee.
“Mnakwenda kuijadili Katiba kuhusu masuala
mbalimbali yenye masilahi ya nchi yetu, siyo mambo ya Muungano tu.
Wekeni utaratibu ili muweze kukubaliana hata katika masuala ambayo kila
mmoja ana msimamo wake,” na kuongeza:
“Kuna suala la ukomo wa kugombea ubunge kuwa
vipindi vitatu. Hii maana yake ni kuwa kama umeshakuwa mbunge kwa
vipindi vitatu huwezi kugombea hata urais,” alisema na kuongeza;
Kwa mujibu wa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, Ibara ya
75 (e) mgombea urais alitakiwa kuwa na sifa za kugombea ubunge, ikiwamo
ya kutowahi kuwa mbunge kwa vipindi vitatu. Hata hivyo kwenye Rasimu ya
Pili itakayojadiliwa na Bunge hilo, ibara ya 79 inayozungumzia sifa za
kuwania urais, hailazimishi mgombea urais kuwa na sifa za kuwania
ubunge.
Rais Kikwete alisema wanasiasa wana dhamana ya
kuwapatia Watanzania Katiba itakayodumu kwa miaka 50 ijayo na kuimarisha
Muungano, umoja, amani na utulivu, siasa safi na kuongeza kasi ya
maendeleo na ustawi wa wananchi.
“Mnatakiwa kuisoma vizuri Rasimu ya Katiba na kujua
yaliyopendekezwa na wananchi. Chambueni kinachofaa na kisichofaa lakini
kwa kuzingatia masilahi ya Taifa na siyo na vyama vyenu,” alisisitiza
Rais Kikwete.
Alisema mafaniko ya mchakato wote wa Katiba yanategemea kauli, mwenendo na matendo mema ya vyama vya siasa.
“Vyama vya siasa vinatakiwa kujenga na siyo
kubomoa. Mkiamua Katiba Mpya ipatikane tutaipata, mkiamua isipatikane
hatutaipata. Katiba Mpya ni kwa masilahi ya watu wote,” alisema na
kuongeza;
“Siyo lazima wazo la chama fulani lipitishwe,
vyama vinatakiwa kutambua kuwa wapo wenzao wenye mawazo mazuri kuliko
wao. Siyo kila unachokitaka wewe na wenzako wanataka hicho hicho.
Muongozwe na nguvu ya hoja siyo hoja za nguvu zilizotolewa na mjumbe wa
chama chako.”
Alisema kuwa lengo lake siyo kuwazuia wajumbe
kutoka vyama vya siasa kutoa maoni katika Bunge hilo. Lengo ni
kuwakumbusha kuwa msimamo wa chama fulani kuhusu jambo lolote, usigeuzwe
kuwa amri ndani ya Bunge hilo.
“Itakuwa aibu kwa chama kwenda katika Bunge bila
kuwa na msimamo wake lakini pamoja na hali hiyo, mtakuwa tayari
kusikiliza mawazo ya wenzenu?” alihoji Rais Kikwete.
Uteuzi wa wajumbe
Rais Kikwete alisema leo atatangaza majina 201 ya wajumbe wa Bunge hilo kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.
Akizungumzia uteuzi huo alisema, “Majina
yaliyowasilishwa na makundi hayo yalikuwa 3,774. Kazi ya uteuzi
imeshakamilika na kilichobaki sasa ni kuhakiki tu majina, kuangalia
uwiano wa wajumbe kimkoa na jinsia.”
Alisema taasisi zisizo za kiserikali zilizoomba
zilikuwa 1,647 na wameteuliwa watu 20, taasisi za dini waliomba 329 na
kuteuliwa 20, vyama vya siasa waliomba 198 na kuteuliwa 42, taasisi za
elimu waliomba 130 na kuteuliwa 20, makundi ya walemavu waliomba 140 na
kuteuliwa 20.
Wengine ni vyama vya wafanyakazi waliomba 102 na
kuteuliwa 19, vyama vya wafugaji wameomba 47 na kuteuliwa 10, vyama vya
wavuvi waliomba 57 kuteuliwa 10, vyama vya wakulima waliomba 157
kuteuliwa 20 na makundi yenye mrengo unaofanana walioomba 727 na
kuteuliwa 20.
Ofisi ya Msajili wa Vyama
Alisema jambo jingine muhimu ambalo Serikali inaendelea
kulifanya kazi ni kuboresha muundo wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa nchini ili iweze kutekeleza ipasavyo majukumu yake.
“Tutaangalia jinsi ya kuongeza bajeti ya ofisi hii ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake,” alisema.
Akizungumzia sheria ya vyama vya siasa alisema
kuwa ina adhabu moja tu ambayo ni kukifuta chama kinachofanya makosa,
kusisitiza kuwa sheria hiyo haitoi nafasi ya kutosha kulea vyama, hivyo
inatakiwa kutazamwa upya.
“Mchakato wa kupitia sheria hiyo na ile ya gharama
za uchaguzi umeanza. Naamini marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa
itasaidia kuboresha matatizo ya shughuli za kisiasa nchini,”
“Bila kuingilia uhuru wa vyama vya siasa na ile ya uchaguzi kusaidia wananchi kuchagua watu kwa ubora wao na vyama vyao.”
Alisema jambo ambalo mpaka sasa halijaanza
kushughulikiwa ni kutenganisha biashara na siasa, “Jambo hili
limeonekana kuwa gumu kweli kushughulikiwa ndani ya mfumo wa Serikali,
sijui limekwama wapi.”
Alisema lazima kuwepo na misingi ya maadili ya
uongozi na kwamba mfanyabiashara anayejitosa katika siasa lazima afuate
utaratibu fulani kama inavyofanyika nchi mbalimbali duniani, ikiwamo
Marekani huku akimtaka msajili wa vyama vya siasa kulishughulikia suala
hilo ili liweze kumalizika.
Wakizungumzia hotuba ya Rais Kikwete, Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alisema,
“Rais anatakiwa kudhibiti kauli zinazotolewa na viongozi wa chama chake,
ambao wanapinga masuala mbalimbali yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba
ikiwamo serikali tatu.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk
Willibrod Slaa alisema, “Hakugusia kabisa wabunge wa Bunge hilo
kuzingatia maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu hiyo.”
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema, “Nadhani
mmesikia alichokisema Rais. Tutazingatia yote aliyoyasema kwa sababu
Katiba hii ni kwa ajili ya masilahi ya Taifa.”
Wakati huo huo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Alhaj Issa Salum alizua kioja wakati akijitambulisha baada ya
kujipambanua kuwa ni muumini wa Muundo wa serikali mbili, kauli ambayo
iliwafanya baadhi ya wajumbe wa mkutano huo kumwangalia kwa mshangao
0 comments:
Post a Comment