Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akipokea cheti maalum cha ulezi wa heshima wa
Chama cha wenza wa mabalozi wa nchi za Afrika walioko nchini Ubelgiji
(Honory Patronese of the Association of the Spouses of African
Ambassadors in Belgium) kutoka kwa Mke wa Balozi wa Cameroon nchini
Ubelgiji Mama Christiane Eloundov de Evina wakati wa chakula cha mchana
walichowaandalia wake wa Marais wa Afrika jijini Brussels tarehe
2.4.2014.
Mke
wa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mama Adelaida Kamala akimkabidhi
Cheti Maalum cha ulezi wa heshima cha wenza wa mabalozi wa Afrika
walioko Ubelgiji, Mke wa Rais wa Cameroon Mama Chantal Biya wakati wa
chakula cha mchana walichowaandalia wageni hao kwenye hoteli ya Sheraton
tarehe 2.4.2014.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wake wa
Marais na Wakuu wa nchi za Afrika pamoja wa wenza wa Mabalozi wa nchi
hizo mara baada ya kupata chakula cha mchana kilichoandaliwa na wenza
hao tarehe 2.4.2014.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete amepewa cheti na Umoja wa wake wa Mabalozi
wa Afrika waishio katika nchi za Jumuia ya Ulaya kwa kutambua na
kuthamini mchango wake na kazi anazozifanya za kuwasaidia wanawake,
wasichana na watoto wa Tanzania.
Cheti
hicho amekabidhiwa jana katika hafla fupi ya chakula cha mchana
kilichoandaliwa na wake hao wa mabalozi katika ukumbi wa mikutano uliopo
Hoteli ya Sheraton mjini Brussels.
Mama
Kikwete ni mmoja kati ya wake wa Marais wa tano wa Afrika
waliokabidhiwa vyeti hivyo vya heshima kutokana na kazi zao
wanazozifanya za kuisaidia jamii na kuhakikisha kuwa inapata mahitaji ya
muhimu kama huduma ya afya na elimu.
Akiongea
kabla ya kuwakabidhi wake hao wa marais vyeti hivyo Mke wa Balozi wa
Equatorial Guinea ambaye pia ni rais wa umoja huo Mama Mangue de Nvono
Nca alisema nia ya kuanzishwa kwa umoja wao ni kulitambulisha bara la
Afrika ambalo linajulikana kuwa na changamoto za njaa, magonjwa,
kutokuwa na haki na usalama wa kutosha katika nchi za Ulaya.
“Siyo
kama Bara letu la Afrika linakabiliwa na changamoto peke yake bali pia
limejaliwa kuwa na umoja, mshikamano na ukarimu na haya yote
yamejidhihirisha kwetu leo hii kutokana na kitendo cha wake wa marais
wetu kushiriki pamoja nasi katika hafla hii na kubadilishana mawazo”,
alisema Mangue de Nvono Nca.
Alisema
umoja huo unatambua kazi kubwa inayofanywa na wake wa Marais wa Afrika
kwa jinsi wanavyowaunga mkono wenza wao kwa kufanya kazi ambazo
malengo yake makubwa ni kuwasaidia wanawake, wasichana , watoto na watu
ambao wako katika makundi hatarishi ndani ya jamii.
Akiongea
kwa niaba ya wenzake mara baada ya kutunukiwa vyeti hivyo Mke wa Rais
wa Congo Brazzavile Mama Antoinette N’Guesso aliwashukuru wake hao wa
mabalozi kwa kazi wanayoifanya ya kulitangaza bara la Afrika kuwa ni
nchi ya umoja, mshikamano na ukarimu jambo ambalo litaondoa dhana
iliyopo miongoni mwa watu kuwa kitu pekee kilichopo barani Afrika ni
matatizo.
Wengine
waliokabidhiwa vyeti hivyo ni pamoja na Malkia wa Swaziland
Inkhosikati Zena Seraya Mahlangu , Mke wa Rais wa Madagascar Mama Lalao
Rajaonarimampianina, Congo Brazzaville Mama Antoinette N’Guesso na
Cameroon Mama Chantal Biy.
Wake
hao wa Marais wameambatana na wenza wao ambao ni Marais wa Afrika
wanaohudhuria mkutano wa nne wa wakuu wa nchi za Afrika na Jumuia ya
Ulaya unaofanyika nchini humo.
0 comments:
Post a Comment