Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta kukiri kuchezewa kwa saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Msekwa amesema, ‘mzungumzaji huyo ana lake jambo’.
Sitta akizungumza na mwandishi wetu juzi mjini Dodoma
alisema ni kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22 ya
1964, iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa.
Alifafanua kuwa saini ya Nyerere imeongezwa herufi
‘us’ kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa kumeandikwa neno
‘Msekwa’ kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema walioongeza
maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini
walifanya makosa.
Msekwa akizungumza na mwandishi weu jana alisema:
“Saini iliyo katika hati original (halisi) ni ya kwangu mimi, lakini
huyo anayesema zimechezewa muulizeni atakuwa na lake jambo. Kama
kompyuta imekosea ni leo kwa kuwa kipindi hicho kompyuta hazikuwapo.”
Aliongeza: “Ana lengo gani la kutilia shaka, ana
lengo gani la kusema imechakachuliwa, kinachotakiwa ni hati original
ambayo iko ofisi ya Katibu wa Bunge itolewe, kwanini tuendelee kuandikia
mate wakati wino upo?”
Mjumbe wa Bodi ya Kituo cha Taarifa kwa Wananchi
Umma (TCIB), Hebron Mwakagenda alisema yote hayo yanatokea ni kuvuruga
hoja iliyopo mezani.
Alisema kitendo cha kupoteza muda kuzungumzia
suala la kuchezewa kwa saini halitakiwi kwani kama maudhui yake
hayakuchezewa basi hoja ya muundo wa Muungano uamuliwe na wananchi
wenyewe.
“Tusianze kupoteza muda kwa mambo ambayo hayapo
cha msingi wananchi wenyewe waulizwe wanaupenda Muungano au la lakini
tusianze kumtafuta mchawi kuwa saini zimechezewa wananchi waamue wenyewe
kuhusu Muungano,” alisema Mwakagenda.
Utata huo ulianza wiki hii baada ya kamati za
Bunge Maalumu la Katiba kuanza vikao vyake vya kujadili sura ya kwanza
na ya sita ya Rasimu ya Katiba, zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na muundo wake.
Hali hiyo ilitokana na kutopatikana kwa hati ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ile ya Sheria ya Baraza la
Mapinduzi ya kuridhia Mkataba wa Muungano.
Aprili 2 mwaka huu, Kamati namba 2 ilimwalika, Spika Mstaafu wa
Bunge la Muungano, Pius Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, lakini
uhalali wa saini zake uliibua malumbano makali. Msekwa aliitwa kutokana
na kwamba ndiye aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha,
alithibitisha kutokea utata huo na kwamba walilazimika kumuita Msekwa
ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa na Msekwa alisema saini zilizopo
katika hati hiyo ni ya kwake.
Nahodha alisema kwa maelezo ya Msekwa, inaonekana
hati ya Muungano ipo Umoja wa Mataifa (UN), kwani kabla ya Muungano,
Tanganyika ilikuwa na kiti chake UN na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hali
kadhalika.
Aliongeza kuwa baada ya UN kuomba uthibitisho wa Muungano, ndipo walipelekewa hati hiyo na kwamba haijawahi kurejeshwa.
Kwa upande wake Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya
Hamis Hamad alisema hati hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu, hivyo
siyo rahisi kuipeleka bungeni Dodoma.
0 comments:
Post a Comment