HALI imeendelea kwenda halijojo ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, baada ya Mchungaji Philemon Mollel kufukuzwa kazi na kuvuliwa kutoa huduma za kichungaji katika kanisa hilo nchini.
Wiki iliyopita, Bodi ya Dayosisi hiyo chini ya uenyekiti wa Israel Ole Karyongi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa KKKT, ilimtimua kazi Meneja wa Hoteli ya Corridor Springs inayomikiwa na Dayosisi hiyo, John Njoroge kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za hoteli hiyo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao kilichofanyika juzi chini ya Karyongi, zilisema kuwa Mchungaji Mollel ameamuriwa afukuzwe kazi na avuliwe wadhifa za kiroho za kichungaji.
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya kikao hicho vilieleza kuwa hatua hiyo ni kutokana na Mchungaji Mollel kushindwa kutekeleza mambo matatu aliyotakiwa na Tume maalumu ya watu watatu walioteuliwa na Menejimenti ya Dayosisi hiyo na alipewa siku tatu kuomba radhi, lakini hakufanya hivyo.
Habari zilieleza kuwa walioteuliwa Desemba 14, mwaka huu na kwenda kumwona Mchungaji Mollel kutekeleza hayo ni pamoja na Msaidizi wa Askofu Mchungaji Solomoni Massangwa, Katibu Mkuu wa Jimbo Arusha Magharibi, Mchungaji Godwini Lekashu na Katibu Mkuu Karyongi.
Taarifa za ndani zilisema Mchungaji Mollel aliandikiwa barua Desemba 17, mwaka huu kufanya mambo matatu kabla ya kufika Desemba 23, mwaka huu.
Habari zilisema katika mambo matatu aliyotakiwa kufanya ni kumwandikia barua ya kuomba radhi kwa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Thomas Lazer kueleza ni kwa nini alimkashifu na kumdharau.
Pili, alitakiwa atoe tamko katika Mtaa wa Azimio ibadani Desemba 23, mwaka huu kuomba radhi kwa yale aliyotamka; na tatu achukue hatua ifikapo Desemba 23, mwaka huu na kumwarifu Katibu Mkuu kwa barua baada ya kuyatekeleza na awe amefanya hivyo kabla ya Desemba 24, mwaka huu.
Vyanzo vya habari vilisema kuwa baada ya Mchungaji Mollel kukaidi hayo, kikao cha watu watatu chini ya Karyongi kiliamua kumfukuza kazi na kumvua uchungaji.
Hata hivyo, habari za uhakika zilisema kuwa Mchungaji Mollel hakufanya hivyo kwa madai kuwa yeye ni mtumishi wa mungu aliyetukuka kufuata maadili na kamwe hawezi kufanya hivyo kwani hakumkashifu mtu wala kiongozi yeyote, bali alieleza ukweli juu ya nani wa kuwajibika katika deni la Sh bilioni 11.
Mbali ya uchungaji, Mollel alikuwa Kiongozi wa Usharika wa Ngateu katika Jimbo la Arusha ni miongoni mwa wachungaji walioamua kuishupalia katika kikao Bodi ya Hoteli hiyo, kuwajibika kwa kufanya ubadhirifu wa mali ya kanisa hilo.
Hata hivyo, Mchungaji Mollel alipopigiwa simu kama amepata nakala ya barua hiyo ya kufukuzwa kazi na kuvuliwa uchungaji, alikiri kuipata, lakini alisema hayuko katika nafasi nzuri ya kulizungumza kwa sasa.
Mchungaji Mollel alisema uamuzi huo umechukuliwa kwa chuki na fitina, lakini haukuangalia madhara ya deni la Sh bilioni 11 iwapo kanisa litashindwa kulipa.
“Nipe muda ndugu yangu, ntakutafuta mimi mwenyewe na nitawaeleza waumini tatizo liko wapi na nani ni tatizo ndani ya Dayosisi hii na kwani nini mimi nimefanywa mbuzi wa kafara,” alisema Mchungaji Mollel.
Awali, Mollel alisema kwa nguvu zote kuwa madai aliyotuhumiwa nayo ni kusema ukweli juu ya madeni ya miradi ya Dayosisi hiyo na ndio chanzo cha barua ya kutaka ajieleze na huo ndio uliokuwa msimamo wake katika kikao hicho cha wachungaji na wakuu wa majimbo.
“Niliweka wazi msimamo wangu katika tulichofanya Desemba 15, mwaka huu kwamba Bodi lazima iwajibike kwa haya yote na kuwataka wenzangu (Wachungaji na wakuu wa majimbo) tusitafune maneno kwa sababu ukweli uko wazi na dhahiri,” alisisitiza Mchungaji Mollel na kuongeza: “Niliwaambia wajumbe wazi kwamba msitufanye wajinga mbele ya washirika, nikasema sipo tayari kuwaambia washirika ndio kwa jambo lisilowezekana na hiyo ndiyo sababu ya kuandikiwa barua hii na nitaweka kila kitu hadharani.”
Kuhusu Njoroge, habari kutoka ndani ya hoteli hiyo zinasema kuwa alitimuliwa kazi wiki mbili zilizopita kutokana na shinikizo la wachungaji wa kanisa hilo kutokana na hali mbaya ya kifedha ya hoteli hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hoteli hiyo, Karyongi alithibitisha kutimuliwa kwa meneja huyo akidai kuwa ni hatua ya kupisha uchunguzi ili kubaini ukweli wa ubadhirifu wa hoteli hiyo na mambo mengine.
“Ni kweli Meneja ametimuliwa ili kupisha uchunguzi wa kina ufanyike kujua ukweli wa hali halisi na sasa timu ya wakaguzi inaendelea na kazi ya kupitia mahesabu ya hoteli hiyo,” alithibitisha Karyongi.
Hata hivyo, habari za ndani za hoteli hiyo na Dayosisi zinasema, hatua ya kufukuzwa kwa meneja huyo ni janja ya viongozi waandamizi wa Dayosisi ambao inasemekana walishirikiana naye kuifilisi kifisadi.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonesha kuwa Njoroge ambaye ni raia wa Kenya, amefichwa Dubai na viongozi hao waandamizi wa Dayosisi (majina yanahifadhiwa kwa sasa) ili wasiumbuke kutokana na kadhia hiyo.
Inasemekana hata mali alizokuwa akimiliki Njoroge ikiwamo Klabu ya usiku inayoitwa Brazil iliyokuwa maeneo ya Nanenane Njiro, ameiuza kabla ya kuondoka nchini kinyemela.
0 comments:
Post a Comment