Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na
Kamishna Mpya wa Polisi Zanzibar Bwana Hamdan Omar Makame aliyefika
Ofisini kwake katika jengo la Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mbweni
kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Kamishna
wa Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame akibadilishana mawazo na Mamaku
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ofisini kwake Mbweni nje kidogo
ya Mji wa Zanzibar.
(Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ).
JESHI la Polisi Nchini
limetakiwa kuongeza ushirikiano wa karibu zaidi na Ofisi ya Mkurugenzi
Mashtaka ili kuona imani ya wananchi kwa jeshi hilo inaendelea kubakia
wakati wote hapa Nchini.
Wito huo umetolewa na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na
Kamishna Mpya wa Jeshi la Polisi Zanzibar Kamishna Hamdan Omar Makame
aliyefika kujitambulisha rasmi hapo katika Ofisi yake iliyopo kwenye
jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif amesema wananchi
wamekuwa wakilalamikia matatizo yanayojitokeza kwenye kesi mbali mbali
zinazowahusu baadhi ya watu ambazo huleta athari ndani ya jamii na
baadhi yake hufifia bila ya wahusika kutiwa hatiani kwa madai ya
kukosekana kwa ushahidi.
Amesema hali hiyo ikiachiliwa
kuendelea ambayo iko chini ya dhamana ya uwajibikaji wa vyombo hivyo
viwili inaweza kuleta sura mbaya na matokeo yake itafikia wakati
wananchi kujichukulia hatua mikononi mwao.
“ Tumeshuhudia matukio mbali
mbali yenye kutia wasi wasi kwa jamii katika maeneo yao vikiwemo
vitendo vya mauaji, udhalilishaji, ujambazi na hata hili lililoibuka la
watu kumwagiwa tindi kali. Lakini matokeo yake uchunguzi huo hufifia
bila ya jibu muwafaka wanalolipata wananchi “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliutaka Uongozi wa Jeshi hilo kuzidisha mashirikano yake na
wananchi pamoja na taasisi zote ili kuona usalama wa raia na mali zao
unaendelea kupatikana hapa nchini.
Balozi Seif alimueleza Kamishna
huyo mpya wa Polisi Zanzibar kwamba Ofisi yake kwa vile ndiyo
inayoratibu masuala yote ya Muungano hapa Zanzibar itakuwa tayari wakati
wote kumpa ushirikiano utakaomuwezesha kutekeleza vyema jukumu
alilokabidhiwa na Taifa yeye na askari wake.
“ Ofisi yangu ndio iliyopewa
jukumu la kuratibu masuala yote yanayohusu mambo ya Muungano kwa hapa
Zanzibar. Hivyo nakuhakikishia kwamba mlango wa Ofisi yangu utakuwa
wazi wakati wowote unapopata tatizo la kiutendaji usione tabu kunifuata
“. Alisisitiza Balozi Seif.
Hata hivyo Balozi Seif
alimueleza Kamishna Hamdan Omar Makame kwamba ipo changa moto hasa
wakati wa muelekeo wa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 jambo ambalo
jeshi hilo linapaswa kujipanga mapema katika kuhakikisha amani ya jamii
inaendelea kuwepo Nchini.
Mapema Kamishna wa Polisi
Zanzibar Hamdan Omar Makame alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba atatekeleza vyema majukumu aliyokabidhiwa na Taifa
katika misingi ya haki na uadilifu.
Kamishna Hamdan aliyepewa
jukumu la kusimamia Kamisheni ya Polisi Zanzibar alieleza kwamba
anachokitarajia katika muda wote wa utumishi wake ni kupata ushirikiano
wa karibu kutoka pande zote mbili zile za viongozi pamoja na raia wa
kawaida.
Kamanda Hamdan Omar Makame
alipandishwa cheo na Jemedari Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete na kuwa Kamishna wa Polisi Tarehe
3/12/2013 na baadaye kuteuliwa kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Nafasi hiyo ya Ukamishna
Zanzibar ilikuwa ikishikiliwa na Bwana Mussa Ali Mussa ambaye kwa sasa
ameteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho
Kikwete kuwa Kamishna wa Polisi Jamii.
0 comments:
Post a Comment