Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akihutubia mkutano wa Mawaziri kutoka nchi
za Mashariki na Kusini mwa Afrika kuhusu elimu ya afya ya uzazi kwa
vijana wa nchi hizo. Mkutano huo wa siku mbili unafanyika nchini Afrika
Kusini katika Mji wa Cape Town.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akipiga picha na Mkurugenzi Mtendaji wa
UNAIDS, Bwana Michel Sidibe wakionyesha umuhimu wa dhana nzima ya
mkutano wa High Level Group ( YOUNG PEOPLE TODAY, TIME TO ACT NOW)
kuhusiana na masuala ya elimu ya afya ya uzazi kwa vjijana katika nchi
za Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Na Anna Nkinda- Cape Town , Afrika ya Kusini
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka viongozi wa Serikali, Taasisi za
kijamii, washirika wa maendeleo na wahisani kutoka nchi za ukanda wa
Afrika ya Mashariki na Kusini kushirikiana na kuandaa programu za
pamoja ambazo zitaongeza elimu ya afya ya ujinsia na huduma za afya ya
uzazi kwa vijana kwani wao ni nguvu kazi ya maendeleo ya taifa.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA)ameutoa wito huo leo wakati akifunga mkutano wa kamati maalum ya
viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia
kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya
Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
uliofanyika katika Hoteli ya The Westin iliyopo mjini Cape Town
nchini Afrika ya Kusini.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA pia aliwapongeza wajumbe wa kamati hiyo kwa kushiriki
mijadala kwa umakini na kuchangia katika maazimio ambayo yataweza
kuongoza juhudi za kuandaa mazingira salama na wezeshi kwa makuzi ya
vijana katika nchi wanazotoka.
Mama
Kikwete alisema, “Leo tumeshuhudia dhamira yetu katika kuimarisha elimu
ya ujinsia na afya ya uzazi kwa vijana katika eneo la Mashariki na
Kusini mwa Afrika. Maazimio tuliyoyatayarisha na kuyakabidhi kwa
mawaziri wetu yamezingatia mahitaji ya elimu na huduma ya afya ya uzazi
kwa vijana katika eneo letu, hali kadhalika mila na desturi katika jamii
zetu.
Maazimio
haya yanahimiza elimu na huduma jumuishi ya afya ya uzazi na ujinsia
ili kuwezesha afua za mabadiliko ya tabia inayochagiza desturi za
kuacha kufanya tendo la ndoa hadi wakati muafaka, kupunguza idadi ya
wapenzi na kuishi maisha ya uadilifu kwa wale wanaoishi na Virusi Vya
Ukimwi (VVU).
Mama
Kikwete ambaye naye ni mjumbe wa kamati hiyo ambaye aliteuliwa kama mke
wa Rais anayejitoa kufanya kazi ya kuisaidia jamii yake wakiwemo kina
mama na watoto wa kike alisema kupitia maazimio hayo wamedhamiria
kuandaa msingi wa elimu bora ya afya ya uzazi kwa kuandaa mitaala na
kutoa mafunzo katika kipindi kifupi hadi kufikia mwaka 2015 .
Katika
mpango wa muda mrefu pamoja na mambo mengine wamedhamiria kuongeza
matumizi ya huduma ya afya ya uzazi, kutokomeza maambukizi mapya ya VVU
kwa vijana na kuzuia ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2020.
Kwa
upande wake waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi
alisema katika mkutano huo mambo mengi yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na
kuongeza jitihada za ziada katika kupambana na tatizo la maambukizi
mapya ya ugonjwa wa Ukimwi kwa vijana na watoto pia waliangalia njia
mbalimbali moja wapo ikiwa ni kutoa elimu kwa vijana hasa waliopo
mashuleni .
“Wizara
za Afya na Elimu zimekutanishwa kwa pamoja kwa madhumuni ya kuja na
mikakati mipya ambayo itapelekea kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa
vijana kupitia mitaala ya kufundishia mashuleni pia watoto wote na kina
mama wajawazito ambao wanamaambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi wapewe dawa
bila tatizo lolote”, alisema Dk. Mwinyi.
Naye
Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dk.
Fatma Mrisho alisema ingawa katika Dunia vifo vinavyotokana na ugonjwa
wa Ukimwi vimepungua kwa asilimia 30 kwa watu wazima lakini kwa vijana
wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 vifo vimeongezeka kwa asilimia
50.
Hivyo
basi wao wanachukua takwimu hizo kama changamoto na wameshalipa suala
hilo kipaombele na kuongeza chachu zaidi ya utendaji wa kazi,
wataendelea kufanya kazi na vijana na kuwasikiliza matatizo yao ili
mahitaji yao yaweze kufanyiwa kazi.
Aidha
Afisa anayeshughulikia Elimu ya Afya na Ukimwi kutoka Shirika la Umoja
wa Mataifa linaloshughulikia Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania
Mathias Herman alisema ili kutekeleza maazimio hayo ushirikiano wa
pamoja kati ya Serikali na wadau wa Elimu na Afya unatakiwa kwa upande
wao watahakikisha kuwa vijana wanapata elimu ya ujinsia na uzazi ambayo
itawasaidia kujitambua na hivyo kujiepusha na Ukimwi na mimba za
utotoni.
Katika
mkutano huo kulikuwa na mijadala mbalimbali ambayo iliibua mambo muhimu
ya kuzingatia wakati wa kutekeleza maazimio ambayo wajumbe walijiwekea
baadhi ya mijadala hiyo ni umuhimu wa kuandaa bajeti pamoja na mikakati
ya kupata fedha na mpango wa utekelezaji wa mikakati, kutayarisha
mipango inayozingatia umri wa watoto, mila na desturi wakati wa kupeleka
elimu ya afya ya uzazi katika mazingira ya shule.
Kupungua
kwa rasilimali na msukumo kwenye miradi ya kuzuia maambukizi ya VVU,
hivyo kusababisha kupungua kwa upatikanaji na matumizi ya kondomu katika
baadhi ya jamii, matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa janga kubwa
ilinalosababisha madhara kwa vijana na umuhimu wa kuandaa mikakati
inayozingatia mahitaji ya vijana wenye ulemavu.
Mawaziri
wa Afya na Elimu kutoka nchi 21 za EAC NA SADC walikubali mbele ya
kamati hiyo kuwa wataenda kuyafanyia kazi maazimio hayo ambayo
yatawasaidia vijana kupata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia
jambo ambalo litawasaidia kufahamu zaidi ugonjwa Ukimwi.
Mkutano
huo wa siku mbili uliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) , UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia watoto (UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WHO) na
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Sayansi na Utamaduni
(UNESCO).
0 comments:
Post a Comment