Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi amesema hajawahi
kuomba upendeleo wa kupewa vitalu vya gesi na kwamba, siku zote
anapigania masilahi ya Watanzania.
Mengi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam,
alipokutana na waandishi wa habari kujibu baadhi ya maelezo ambayo kwa
nyakati tofauti Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
aliyatoa.
“Mwanzoni mwa Septemba, Prof Muhongo alinukuliwa
na vyombo va habari akisema: “Mengi hana uzawa bali ubinafsi. Anataka
kufanya udalali wa vitalu vya rasilimali zetu. Waelezeni Watanzania
ukweli huu.”
Ukweli ni kwamba, mimi siyo mbinafsi na pili
sijawahi kuomba upendeleo wa kupewa kitalu cha gesi bali ninapigania
Watanzania kwa jumla,” alisema Mengi.
Alisema pia kuwa, hamiliki migodi mingi ya madini
kama inavyodaiwa “Ukweli ni kwamba, mimi namiliki kwa ubia na Watanzania
wenzangu mgodi mmoja wa uchimbaji wa madini ya Tanzanite wenye eneo
lisilofikia hata kilomita moja ya mraba,” alisema Mengi.
Alisema kuwa, ameshapata nafasi kubwa ya
kujiendeleza kibiashara na kwamba anachofanya sasa ni kupigania
Watanzania wengine waweze kushiriki kama ilivyo kwenye Sheria ya Taifa
ya Uwekezaji Kiuchumi ya mwaka 2004.
Sheria hii pamoja na mambo mengine, inatoa upendeleo maalumu kwa Watanzania katika rasilimali zao.
Alisema ana matumaini kuwa mkutano ambao Rais
Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuufanya leo na watu wa sekta binafsi,
utasaidia kupata mwafaka wa kuwawezesha Watanzania kwenye nyanja
mbalimbali za kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment